Wote aliowataja kwa ubaya wametumbuliwa na Rais Magufuli

0
890

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

USITHUBUTU jina lako kutajwa kwa ubaya na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na ziara zake kuonekana kuacha maumivu kwa watendaji mbalimbali wa Serikali, wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wanaoonekana kwenda kinyume na kasi ya Serikali.

Karibu maeneo yote ambayo Majaliwa amefanya ziara na kuonyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa watumishi katika eneo husika, Rais Dk. John Magufuli amekuwa akichukua hatua za kuwaondoa katika nafasi zao mara moja.

Wakati moto aliouwasha katika ziara yake mkoani Morogoro hivi karibuni ukiwa bado haujazima sawasawa, mara hii Waziri Mkuu ameonyesha kuchukizwa na tabia ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdallah, anayedaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na watendaji wengine wa wilaya hiyo hali inayosababisha watumishi 14, wakiwamo makatibu tawala na madereva 10 kuhamishwa baada ya kusema hawafanyi kazi ipasavyo.

Asia anadaiwa kuwakataa madereva wapatao 10 walioajiriwa kuendesha gari lake pamoja na watumishi wengine wanne waliohamishwa jambo linaloibua utata kuhusu nani mwenye kasoro kati yao.

Kutokana na hali hiyo Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, kufuatilia utendaji kazi wa ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo.

Kukosekana kwa mshikamano kati ya Asia na watendaji wengine wa halmashauri hiyo, inadaiwa kusababisha hata kazi nzuri wanazozifanya zisionekane.

“Hata aliyekuwa Katibu Tawala wa wilaya hii alihamishwa kwa sababu za kutoelewana na DC, na hata huyu Katibu Tawala wa Wilaya aliyepo sasa hana raha, anataka kuhama kwa sababu hizo hizo.

“Lazima tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi, lazima kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya. Tujue mbovu ni nani. Mkuu wa Mkoa tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai!” alisema Majaliwa.

Kauli hiyo ya Majaliwa inaacha maswali miongoni mwa wafuatiliaji wa siasa nchini, iwapo itamwacha salama Mkuu huyo wa Wilaya, hasa ikizingatiwa kuwa katika ziara yake ya hivi karibuni Morogoro ilisababisha kutenguliwa uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Mkoa, Stephen Kebwe, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Mussa Mnyeti.

Kama ilivyo kwa Asia, Waziri Mkuu aliwanyooshea vidole watendaji hao baada ya kubaini kasoro kadhaa za kiutendaji ikiwa ni pamoja na viongozi hao kutokuelewana.

Kutokana na kubainika kwa kasoro hizo, Waziri Mkuu alimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji wa wateule hao.

Mgogoro kati ya viongozi hao ulidaiwa kusababisha kushindwa kusimamia vema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ya kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara licha ya Serikali kutoa fedha huku wawili hao wakidaiwa kugombania miradi na hata kuchakachua mingine.

Hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli dhidi ya wateule wake hao, zinaonyesha kuwa amekuwa akifuatilia kwa karibu ziara za msaidizi wake na mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali na inapotokea ameonyesha kutoridhishwa, yeye huchukua hatua mara moja.

Baadhi ya matukio ambayo Rais Magufuli amepata kuchukua hatua baada ya Waziri Mkuu kuonyesha shaka kwa watendaji baada ya ziara, ni pamoja na kutenguliwa uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulru.

Nkulru aliondolewa katika nafasi aliyokuwa akiishika muda mfupi baada ya kumpokea Majaliwa aliyekwenda mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi.

Hata kuondolewa kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba na Waziri wa Biashara, Charles Mwijage, wakati wa sakata la uuzaji wa korosho, kulikuja baada ya Majaliwa kufanya ziara katika mikoa inayozalisha zao hilo na kisha baadaye kutishia kuwafutia leseni wafanyabiashara watakaokaidi utaratibu uliopangwa wa bei ya korosho.

Baada ya ziara hiyo ya Waziri Mkuu ya mwishoni mwa Oktoba, mwezi uliofuatia, Novemba 10 Rais alitengua uteuzi wa mawaziri hao na nafasi zao kuchukuliwa na Japhet Hasunga (Kilimo) na Joseph Kakunda (Viwanda, Biashara na Uwekezaji).

Pia katika ziara zake hizo, Waziri Mkuu amekuwa akichukua hatua kali kwa baadhi ya watendaji ambao haridhishwi na utendaji kazi wao. Miongoni mwa waathirika ni pamoja na Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Same, Mussa Msangi, aliyemsimamisha kazi kwa kosa la kumdanganya kuhusu mradi wa maji Kata ya Hedaru.

Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwapo tatizo kutokana na wananchi kuzomea wakati wa utambulisho kwa viongozi mbalimbali aliokuwa ameambatana nao.

Jambo hilo lilimfanya Majaliwa kumwita mhandisi huyo aelezee ukweli wa madai ya wananchi kwamba maji yalitoka siku hiyo kutokana na ziara yake.

Awali mhandisi alipokuwa akitoa salamu kwa Waziri Mkuu, alidai kuwa upatikanaji wa maji eneo hilo umefikia zaidi ya asilimia 80 huku makusanyo yatokanayo na mauzo yakiwa Sh milioni 7 kwa mwezi.

Hali hiyo iliibua shaka kwa Waziri Mkuu ambaye alidai kuwa haiwezekani kama maji yanatoka, makusanyo yawe Sh milioni 7 tu na kusema kuwa ama maji hayatoki au wanakusanya fedha zinaliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here