24.6 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara ichukue hatua uharibifu huu wa misitu

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA

UNAWEZA ukajiuliza maswali mengi sana na pengine ukashindwa kupata jibu sahihi kutokana na kitendo cha ukatili wa misitu kilichofanyika Desemba 27, 2018, eneo la Nyamhongolo panapofanyikia  maonesho ya Sikukuu ya Wakulima maarufu ‘Nane nane’,  katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza.

Kitendo cha ukataji wa miti ovyo iliyokuwa imepandwa katika bustani inayomilikiwa na Kampuni ya Apex Holding & Ducorp Group, kilistaajabisha kila mtu aliyekuwa akipita katika barabara kuu ya Mwanza – Musoma.

Wengi tulihoji sababu ya uharibifu huo wa misitu hiyo ambayo ni sehemu ya kupumzikia kwa wakazi wa Mwanza hususan wa Kata ya Igoma na Kisesa.

Ukataji huo wa miti naweza kuutafsiri kama sehemu ya ukatili wa misitu na kwenda kinyume na maelekezo ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye muda wote amekuwa akihamasisha wananchi kupanda miti maeneo yao kwa lengo la kutunza mazingira yanayowazunguka.

Kwa mujibu wa maelezo ya wasimamizi wa bustani hiyo, Kampuni ya Apex Holding & Ducorp Group inayojishughulisha na uuzaji wa vipuri na usafirishaji, waliamua kutengeneza bustani ya miti hiyo mbele ya ofisi yao kama sehemu ya kutekeleza maelekezo ya Serikali, pia bustani hiyo ilikuwa ikitumiwa na watu wote kupumzika bila kutozwa fedha.

Jambo la kushangaza na linahojiwa na watu wengi juu ya zoezi hilo lililofanywa na Halmashauri ya Ilemela chini ya usimamizi wa mgambo wenye silaha kukata miti na kuharibu bustani hiyo ya Kampuni ya Apex Holding &Ducorp Group, ni kwamba kwanini kitendo hicho kifanyike eneo hilo wakati kuanzia Buzuruga hadi Kisesa kuna miti imepandwa pembezoni mwa barabara na haikukatwa.

Kwa yeyote aliye na akili timamu anapofika eneo hilo ni lazima atagundua kuna kitu kimefanyika kinyume na maadili ya kazi, ndio maana kampuni ya Apex Holding & Ducorp Group imelalamikia suala hilo na kuiomba Serikali kupitia vyombo vyake ichunguze sakata hilo, kwani inahisi kuna vitendo vya rushwa vimetendeka kwa watumishi wa Ilemela. 

Kwa mujibu wa barua ya Halmashauri kwenda kampuni ya Apex Holding &  Ducorp Group ya Desemba 21, 2018 yenye kumbukumbu namba IMC/F.40/1/12 ambayo ilisainiwa na Kaimu Mkurungezi wa Halmashauri wa Ilemela, Bakari Vuri, ilisema itaendesha zoezi la kupunguza matawi ya miti mbele ya ofisi ya kampuni hiyo lakini kilichofanyika ni kukata miti chini ya shina.

Sababu zilizotolewa na halmashauri kupunguza matawi katika eneo hilo ni kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa kwao na kituo cha mafuta cha Petro Afrika, kwamba miti hiyo inazuia madereva kuona vizuri wakati wa kutoka na kuingia kituoni hapo.

Hata hivyo, kampuni hiyo inadai kwamba huenda kuna mchezo mchafu umefanyika kuharibu bustani hiyo ambayo lengo lake kuu ni kutunza mazingira ambayo ndiyo kilio cha taifa hivi sasa.

Aidha, sakata hilo la ukatwaji huo wa msitu linakwenda mbali zaidi kwa kulihusisha na mmoja wa viongozi wa Halmashari ya Ilemela ambaye aliwahi kuomba msitu huo kuweka mizinga ya nyuki na kukataliwa na uongozi kwa kuelezwa kuwa nyuki wanaweza kuhatarisha usalama kwenye ofisi hizo.

Aidha, siku chache baadaye kigogo huyo alirejea na kudai miti hiyo imepandwa  kwenye hifadhi ya barabara hivyo inapaswa kuondolewa.

Hata hivyo, jambo la kushangaza zile mamlaka zinazohusiana na hifadhi za barabara kuu, barabara za vijijini na mjini zote zilipoulizwa zilidai hazina taarifa ya zoezi hilo.

Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilemela, John Wanga, alipotafutwa kwa njia ya simu alidai hayupo Mwanza na kukataa kuzungumzia suala hilo huku akihoji kama kukatwa kwa miti katika bustani hiyo ni habari ya kuandikwa na kutangazwa?

Binafsi niiombe Serikali kupitia vyombo vyake kuchunguza suala hilo linalopingana moja kwa moja na sheria ya mazingira inayohimiza kila mtu, taasisi kupanda miti kadiri iwezekanavyo.

Kitendo cha kukatwa miti ya bustani iliyotunzwa kwa miaka mingi bila kutolewa sababu za msingi na mamlaka yenye dhamana, kinapaswa kuhojiwa na hata kupingwa kwa namna iwayo yote.

[email protected],0692925352

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles