29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wingu jeusi kifo cha Balali

Na mwandishi wetu.

IKIWA ni takriban miaka sita sasa tangu aliyekuwa Gavana wa Benki ya Tanzania  (BoT), Daudi Balali, afariki dunia nchini Marekani, duru za uchunguzi wa gazeti la MTANZANIA zimebaini kuwa jopo la madaktari bingwa waliokuwa wakimtibu liliwadokeza ndugu zake wa karibu kuhusu kuwepo kwa hali ya utata iliyosababisha kifo chake.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa zaidi ya miezi mitatu ndani na nje ya nchi kuhusu hali ya kutilia shaka kifo hicho iliyoonyeshwa na makundi mbalimbali ya jamii ya Watanzania, zimethibitisha pasipo chembe ya doa kuwa Balali alifia mikononi mwa mke wake, dada zake wawili waliokuwa wakimuuguza na alizikwa nchini Marekani katika maziko yaliyohudhuriwa na watu wachache.

Kuvuja kwa taarifa hizi hivi sasa, kumekuja baada ya baadhi ya ndugu zake wa karibu kukubali kuhojiwa na timu ya waandishi wa habari za uchunguzi wa gazeti hili ambayo ilikuwa ikitafiti ukweli wa kifo chake, mahali kaburi lake lilipo, mazingira ya kuondoka kwake nchini, ugonjwa aliokuwa akiugua, matibabu yake, kifo chake na kisa cha serikali kujitenga mbali naye siku za mwisho wa uhai wake na hata wakati wa maziko yake. Pia taarifa za familia kuzuia baadhi ya watu waliofika Marekani kumwona wakati akiwa hospitali na nyumbani kwake huko Boston, Marekani. Uchunguzi huu wa gazeti la MTANZANIA unachapwa kila siku kwenye gazeti hili ambapo pamoja na mambo mengine, unatarajia kuibua maswali tata na majibu yake, hivyo kukata kiu ya wasomaji wetu kuhusu nini hasa kilimfika Balali.

Balali, aliyefariki dunia Mei 16, 2008 huko Boston, nchini Marekani, wakati ambao alikuwa akiaminika kuwa shahidi muhimu wa kashfa ya wizi wa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), tangu wakati huo hadi sasa MTANZANIA linapoandika ripoti hii maalumu, kumekuwa na kauli zinazoashiria kuwapo hali ya kutiliwa shaka kuhusu ukweli wa kifo chake, sentensi ambayo inaitesa na kuikasirisha familia yake, hususan mke, dada na kaka zake aliozaliwa nao tumbo moja.

Elizabeth Balali, mmoja wa dada zake marehemu Balali, ambaye alizungumza mara kadhaa na MTANZANIA kupitia simu ya kiganjani kabla ya kukutana ana kwa ana na timu ya waandishi wa habari wa gazeti hili, alieleza kwa ukali mshangao wake kuhusu ukweli wa kifo hicho kuanza kufuatiliwa sasa, huku akitaka apewe muda wa kutafakari kabla ya kutoa kauli yoyote dhidi ya jambo ambalo alikiri kumuumiza na kumharibia maisha yake.
Awali akizungumza kupitia simu ya kiganjani kabla waandishi wa gazeti hili hawajafika kwenye makazi yake huko Boko, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, mahali ambako Balali alijenga kabla ya kufikwa na mauti, alihoji kwa sauti ya ukali kitu ambacho kinatafutwa na waandishi miaka sita baada ya kutokea tukio hilo aliloliita la kusikitisha.

“Miaka sita imepita sasa tangu kaka yangu afariki dunia, what do you want (mnataka nini?) Mimi maisha yangu yameshaharibika kutokana na kumpoteza kaka yangu na mama yangu, nilikuwa nikiishi Marekani sasa hivi nimerudi, mnachotaka nini kutoka kwangu?

“Wewe ndiye Mullinda, eeh Charles eeh? Na huyo mwenzio unasema ni Ratifa. Mnataka nini katika familia hii? Wewe Mullinda umenipigia simu tumeongea na hukusema kama unakuja hapa nyumbani, mnanifanyia surprise eeh? Hakika mimi siwapendi waandishi wa habari, mnataka kuuza news tu hamjali maumivu yetu ya moyoni.

“Mullinda and Ratifa, Balali amekufa miaka sita iliyopita, mlikuwa wapi? Nasema no, no, no, no, no. Ondokeni hapa nyumbani upesi msinitibue kabisa. Na sikilizeni, hata kama mmetumwa na Serikali au Rais Kikwete kawatuma, upesi ondoka hapa siko tayari kuwasikiliza.

“Sina kaka na mama yangu nimemzika hapo, (huku akionyesha pembeni kidogo ya nyumba iliyo kwenye shamba la Balali huko Boko), haiwasaidii kitu hata kama mkijua Balali alikufa au hajafa. Get out please,” alisema kwa ukali Elizabeth.

Hata hivyo, baada ya timu ya waandishi wa MTANZANIA kumsihi awape nafasi ya kuwasikiliza na kueleza kuwa kazi yao haihusiani na Serikali wala Rais Kikwete, kwa sauti ile ile alisema: “Wewe Mullinda tunaongea, unayo namba yangu ya simu na mimi ninayo ya kwako, nipigie baada ya siku tatu au nne naweza kuwa vizuri labda, tutaongea.”

Kabla ya kuzungumza na Elizabeth, MTANZANIA lilimhoji mtoto wa kaka yake Balali aliyejitambulisha kwa jina moja la Sarah nje ya geti la nyumba yao huko Boko, ambaye alithibitisha kuwa ni kweli baba yake mdogo alikufa na yeye ni mmoja wa watu waliohudhuria mazishi yake huko nchini Marekani.

Sarah alisema hawezi kuliongelea kwa undani suala hilo kwa sababu hana ruhusa hiyo na kushauri atafutwe Elizabeth, kuwa ndiye mwenye mamlaka hayo.

Alipoombwa kueleza kile alichokishuhudia katika mazishi hayo, kwa sauti ya chini alisema: “Tulikuwa tunampenda baba yetu mdogo, tulikuwa tunampenda sana. Tulisikitishwa na jinsi alivyokufa, walimtendea vibaya sana sana. Nilikuwepo kwenye mazishi yake, nilishuhudia akizikwa. Mtafuteni shangazi Elizabeth, mkiweza kuongea naye mtapata jambo zito sana kuliko huu uzushi unaosambazwa kuwa hajafa.”

Uchunguzi zaidi uliofanyika mahali alikozaliwa Balali, eneo la Liganga, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, umeonyesha kuwa ndugu zake walitaarifiwa kuhusu kuugua kwake katika mazingira ya kutatanisha na utata ulioelezwa na madaktari wa kifo chake.

Dada mdogo wa marehemu Balali, aliyejitambulisha kwa jina la Maula Balali, alilieleza MTANZANIA kuwa familia nzima ya Balali ina uhakika wa kifo hicho kutokea kwa sababu aliuguzwa hadi mauti yanamkuta akiwa mikononi mwa baadhi ya wanafamilia.

“Sisi kama familia tunaamini kwa sababu tuna uhakika Balali alikufa. Hayo maneno kwamba alikufa au hajafa tunayasikia na hatuyapendi kwa sababu yanatutia uchungu, kwani tulikwishampoteza kaka yetu,” alisema Maula kwa masikitiko.

Maula alisema dada zake wawili aliowataja kwa majina ya Magreth na Elizabeth, ambao walikuwa Marekani wakati Balali akiugua hadi kufariki, ndio waliotoa taarifa za kifo cha kaka yao kwa wanafamilia waliokuwa hapa nchini.

“Wakati kaka anaugua Dada Elizabeth alikuwa akiishi Marekani. Lakini pia Dada Magreth naye alikwenda kumuangalia wakati akiwa amelazwa hospitalini, hivyo hadi anafariki dunia Magreth na Elizabeth walikuwa naye na walimshuhudia,” alisema Maula.

Hata hivyo, uchunguzi wa MTANZANIA unaonyesha kwamba baada ya Balali kuambiwa kwamba alikuwa na muda mfupi wa kuishi, aliomba aruhusiwe kufia kitandani kwake, kwenye nyumba yake.

Akieleza jinsi taratibu za msiba huo zilivyofanyika hapa nchini, alisema baada ya kutaarifiwa kuhusu kifo hicho, familia kwa mujibu wa mila na desturi iliweka msiba huo nyumbani kwake (Balali) eneo la Boko, jijini Dar es Salaam, ambako ndugu wote walikusanyika hapo.

Ni mahali hapo ndipo mama yake mzazi Balali (Rachel Balali) alipokuwa akiishi.

Mahojiano yaliyofanywa na MTANZANIA kutoka kwa watu walio karibu na familia hiyo na baadhi ya wana ndugu waliohudhuria msiba huo huko Boko zimeonyesha kuwa mama mzazi wa Balali hakuweza kuhudhuria mazishi ya mwanaye nchini Marekeni kwa sababu ya umri mkubwa aliokuwa nao ambao ulikuwa umempotezea uwezo wa kuwa na kumbukumbu.

Katika mahojiano hayo, ilielezwa kuwa wakati wa msiba, mama yake Balali ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa akiuliza mkusanyiko mkubwa wa watu nyumbani kwa mtoto wake ulikuwa wa nini, swali linaloelezwa kuwa alikuwa akiliuliza kila mara kwa sababu alikuwa haelewi kuwa mtoto wake amekufa kutokana na kupoteza kumbukumbu.

Wakati MTANZANIA likibaini ukweli uliojificha katika wingu jeusi kuhusu kifo cha Balali, aliyefariki huko Marekani Mei 16, 2008, kumbukumbu zilizopo kutoka serikalini zinaonyesha kuwa kifo hicho kilitokea wakati sekeseke la kashfa ya EPA likiwa limepamba moto, huku Marehemu Balali akidaiwa kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakijua kwa ufasaha njama na taarifa muhimu za namna upotevu wa fedha hizo ulivyofanyika na nani walikuwa wahusika wakuu.

Kumbukumbu hizo zinaonyesha kuwa tangu kutokea kwa kifo hicho, Serikali imekuwa katika wakati mgumu wa kuaminika mbele ya jamii juu ya utata uliojitokeza kwenye kifo cha Balali, hasa baada ya kutoa taarifa za kutatanisha kuhusu kuugua kwake hadi kifo chake.

Watanzania wengi walishangazwa na kauli ya Serikali kuwa ilikuwa haijui hospitali aliyolazwa wala eneo hasa alilokuwa akiishi nchini Marekani na hiyo ilikuwa ni muda mfupi baada ya kupatikana kwa taarifa nyingine za kutatanisha kuhusu kufukuzwa kwake kazi na Rais Jakaya Kikwete kutoka katika utumishi wa BoT ambako alikuwa na wadhifa wa gavana.

Kabla ya hapo, Serikali ilitoa taarifa ya kuthibitisha tetesi zilizokuwa zimezagaa nchini, ikikiri kuwa Balali alikuwa mgonjwa mahututi aliyelazwa kitandani akipatiwa matibabu nchini Marekani, lakini katika kile kilichowashangaza wengi, ilikataa kueleza jimbo alilokuwa na wala haikutoa taarifa ya maendeleo ya hali yake hadi taarifa za kifo chake zilipopatikana.

Pamoja na kudaiwa kufikwa na mauti yake Mei 16, 2008, Serikali, baada ya maswali mengi na usumbufu kutoka kwa waandishi wa habari, ilitoa taarifa juu ya kifo cha Balali siku tano baada ya kuwa kimetokea, hali iliyoibua maswali mengi tata ya kwa nini haikuwa ikijua mahali alipokuwa mtu muhimu kwa taifa kama yule kwa wakati ule.

Kutoka nchini Marekani, duru za uchunguzi kutoka kwa watu waliokuwa karibu na Balali na hata kutoka ndani ya jopo la madaktari bingwa waliokuwa wakimtibu zimedokeza kuwa uchunguzi wa kitatibu aliofanyiwa kabla ya kufikwa na mauti ulionyesha kuwa baadhi ya sehemu za mwili wake, hasa tumboni zina madhara makubwa hivyo kusababisha kifo chake.

Zipo taarifa zilizokusanywa kutoka nchini Marekani zinazodai kuwa madaktari waliomfanyia uchunguzi Marehemu Balali waligundua baadhi ya viungo vya ndani ya tumbo lake vilikuwa vimeoza na iliwalazimu kukata sehemu ya utumbo wake katika jitihada za kuokoa maisha yake, lakini ilishindikana.

Ingawa haifahamiki hadi sasa mahali hasa mwili wa Marehemu Balali ulipata madhara yaliyosababisha kifo chake, taarifa hizo zinakwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa madaktari hao waliwaeleza baadhi ya ndugu zake wa karibu kuwa kutokana na madhara aliyokuwa amepata tumboni mwake, alikuwa hana uwezo wa kuishi kwa zaidi ya mwezi, taarifa ambayo ilithibitika baada ya kufariki Mei 16, 2008.

Taarifa toka ndani ya wanafamilia wa Balali, zinaeleza kuwa ni taarifa hizo ndizo ambazo ziliifanya familia kutomruhusu mtu yeyote kumuona au kuwa karibu na Balali.

Ni kwa muktadha huo, wakati wote akiwa anaugua nchini Marekani, Balali aliweza kufikiwa na watu wa karibu tu.

Taarifa zinaeleza kuwa, hata baadhi ya viongozi wa Serikali waliowahi kufika nyumbani alikokuwa akiishi nchini Marekani kwa nia ya kumjulia hali walishindwa kumuona Balali kutokana na hofu kubwa iliyojengeka ndani ya familia.

Usikose mfululizo wa ripoti maalumu zinazoendelea kila siku kwenye gazeti hili kuhusu uchunguzi ulioibua ukweli uliojificha kwenye utata wa kifo cha Daudi Balali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles