28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wimbi la watoto kuuawa laamsha hofu Njombe

Na ELIZABETH KILINDI

-NJOMBE

WIMBI la watoto kupotea na kuonekana wakiwa wameuawa huku wametolewa baadhi ya viungo vya mwili limezidi kukua wilayani hapa na kuibua taharuki kwa jamii.

Kwa kipindi cha miezi miwili, zaidi ya watoto watano  wamekutwa wameuawa na watu ambao bado hawajafahamika, huku matukio hayo yakihusishwa na imani za kishirikina.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri, alisema matukio hayo yamemshtua kwani hadi sasa watoto sita wameripotiwa kupoteza maisha katika maeneo tofauti wilayani hapa.

“Hizi ni habari za kusikitisha, sio habari nzuri, hadi sasa ni watoto sita wamepoteza maisha katika maeneo mbalimbali, tunazungumza kwa huzuni kubwa na ikizingatiwa kwamba mtoto ni tegemeo la mzazi na taifa kwa ujumla,” alisema Ruth huku akiwataka wazazi kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wa kwenda na kurudi shule.

MTANZANIA lilifanya mahojiano na familia ya Gordeni Mfugale (43) mkazi wa Mtaa wa Joshoni, Njombe, ambaye mtoto wake wa kiume aitwaye Goodluck Mfugale (5) alipotea na baadaye kukutwa ameuawa.

Akisimulia tukio hilo, Mfugale alisema Januari 4 mwaka huu, mtoto wake alipotea akiwa anacheza jirani na nyumbani kwao na baadaye mwili wake ulionekana Januari 10 pembezoni mwa Mlima Njombe, Mtaa wa Joshoni karibu na Shule ya Sekondari Njombe.

“Mimi nilikuwa nimeenda katika shughuli zangu za kila siku, sijui ilitokeaje, mtoto alikuwa anacheza na wenzake, lakini mama yake aliporudi hakumuona ndipo tulipoanza kumtafuta bila mafanikio,” alisema Mfugale.

Aliongeza kuwa siku ya saba walipigiwa simu na polisi ili wakatambue mwili wa mtoto ambao ulikuwa umetupwa katika eneo la Shule ya Sekondari Njombe.

“Tulifika pale na nilitambua kuwa ni mwili wa mwanangu, lakini awali katika maeneo hayo tulishapita wakati tukimtafuta, cha kushangaza tena akaja kuonekana eneo hilo hilo,” alisema Mfugale kwa masikitiko.

Aidha Mfugale aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina wa makundi ya kihalifu ili kuwanusuru watoto kwani nao wana haki ya kuishi kama watu wengine.

Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Joshoni, Amon Swale, alisema tukio hilo ni la kwanza na limesababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa mtaa huo.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Joshoni, Warda Salehe, alisema; “Tukio hili limeshtua jamii kwa kiasi kikubwa.

“Ingawa upelelezi unaendelea, naiomba jamii kuwa watulivu na wazazi kuwapeleka na kuwarudisha watoto wao shule maana hali inatisha,” alisema Warda.

Tukio jingine lilitokea Desemba 8, mwaka jana katika Kijiji cha Mfereke, Kata ya Utelingolo, Halmashauri ya Mji wa Njombe ambako mtoto Oliver Ng’ahala (5) alipotea wakati akirudi kutoka shule.

Mtoto huyo aliyekuwa anasoma darasa la awali katika Shule ya Msingi Kambarage, mwili wake ulipatikana siku ya pili katika msitu wa miti ya kupandwa akiwa ameuawa kwa kunyongwa shingoni na kuchomwa kitu chenye ncha kali.

Akisimulia tukio hilo, baba mkubwa wa marehemu aitwaye Lusungu Ng’ahala, mkazi wa Kijiji cha Mfereke, alisema alipata taarifa za kupotea mtoto huyo saa mbili usiku na ndipo walipoanza kumtafuta bila mafanikio.

“Siku ya ya pili tukiwa tunaendelea kumtafuta, mtendaji alipiga simu kutwambia kuna mwili wa mtoto umeokotwa, kwahiyo sisi tulikwenda na kuutambua mwili wa mtoto akiwa amenyongwa shingoni, huku sehemu za siri akiwa na majeraha.

“Awali tulidhani amebakwa, lakini baadaye taarifa za hospitali zilisema aliingizwa kitu chenye cha kali,” alisema Ng’ahala.

Aidha alisema tukio hilo limesababisha familia ya mtoto huyo kuingiwa na woga na kulazimika kukihama Kijiji cha Mfereke mjini Njombe. Hata hivyo hakutaja eneo ambalo familia hiyo imehamia.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi, Rashidi Ngonyani, alithibitisha matukio hayo na kusema kuwa upelelezi unaendelea na hakuna mtuhumiwa yeyote aliyekamatwa.

“Kwa matukio haya tunaomba ushirikiano kwa wananchi ili kuweza kuwabaini wahalifu, ni wazi matukio yote yanahusishwa na imani za kishirikiana.

“Niwaombe viongozi wa mtaa pamoja na kata kubaini wageni wote wanaoingia,” alisisitiza Kamanda Ngonyani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles