25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wiki mpya majipu matano

magufuli 23TUNU NASSOR NA FROLIAN MASINDE, DAR ES SALAAM

WAKATI Watanzania wakiingia katika juma jipya kwa ajili ya majukumu ya ujenzi wa taifa, mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli, wameendelea kutumbua majipu bila ganzi kwa watendaji wa Serikali.

Jana kwa nyakati tofauti Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, ametangaza kutumbua watendaji watatu, huku mwenzake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, akitumbua watendaji wawili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN).

Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri Kairuki alitangaza kumsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Said Nassoro kutokana na utendaji usioridhisha.

Pia amewasimamisha kazi Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Tabora, Silvanus Ngata na Dk. Joseph Mbwiro wa tawi la Dar es Salaam kutokana na ubadhirifu wa fedha.

Waziri Kairuki aliwaambia waandishi wa habari kuwa Nassoro ameshindwa kuwasimamia watumishi na kusababisha matumizi mabaya ya fedha.

Alisema kutokana na makosa ya kiutendaji, Nassoro aliotoa mwanya kwa viongozi wa matawi kufanya ubadhirifu wa mali za umma kwa masilahi binafsi.

“Kwa mfano aliyekuwa mkuu wa tawi la Mtwara, Silvanus Ngata alizidisha fedha za gharama za ujenzi tofauti na zilizoainishwa.

“Pamoja na tuhuma hizo, Nassoro hakuchukua hatua yoyote zaidi ya kumbadilisha kituo cha kazi na kumpeleka mkoani Tabora,” alisema Kairuki.

Kuhusu Dk. Mbwiro, alisema kuwa alitumia vibaya fedha za ada na kusababisha hasara ya shilingi bilioni moja alipokuwa anakaimu kitengo cha fedha.

“Pamoja na tuhuma hizi, bado aliteuliwa kuwa mkuu wa chuo wa tawi la Dar es Salaam nafasi ambayo alikuwa akiitumikia hadi sasa,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zilionyesha kuwapo ubadhirifu huo.

 NAPE NA JIPU TSN

Nayo Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), imemsimamisha kazi Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo, Gabrieli Nderumaki, kupisha uchunguzi kutokana na utendaji usioridhisha ndani ya kampuni hiyo.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Profesa Moses Warioba, alisema hatua ya kumsimamisha kazi Nderumaki imetokana na kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo na nafasi yake itachukuliwa na Naibu Mhariri, Tumma Abdallah.

“Kumekuwa na mambo mengi yanayofanyika bila kufuata utaratibu ndani ya kampuni hii ikiwamo wafanyakazi kutoelewana na menejimenti katika kulipwa stahili zao, pamoja na wafanyakazi kupewa  majukumu ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza,” alisema Prof. Warioba.

Alisema pamoja na hayo, pia bodi imetengua uteuzi wa Felix Mushi, ambaye alikuwa Meneja Mauzo na Masoko katika kiwanda cha uzalishaji kwa kukosa sifa na utendaji mbovu uliosababisha kampuni kushuka katika uzalishaji.

Hatua hiyo ya kuwawajibisha watendaji hao imetokana na ziara iliyofanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika kampuni hiyo, ambapo pia hakuridhiswa na utendaji mbovu uliosababisha wafanyakazi 21 kuacha kazi.

“Nataka bodi itafakari juu ya malalamiko yaliyopo kwa wafanyakazi na wachukue hatua kabla mimi sijakutana na wafanyakazi hao wiki ijayo ili kujua mapungufu yako wapi,” alisema Nape.

Hata hivyo, bodi hiyo ya wakurugenzi inaendelea kutafuta namna ya kuboresha utendaji ndani ya kampuni hiyo ili iendane na kasi iliyopo katika uzalishaji wa magazeti kwa kiwango kikubwa.

 MAJIPU YALIYOTUMBULIWA

Katika siku zaidi ya 100 za uongozi wa Rais Magufuli, watendaji zaidi ya 150 wamefukuzwa kazi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.

Katika mpango wake huo Rais Magufuli aliwang’oa vigogo wapatao 23 wa Mamkala ya Bandari (TPA) pamoja na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa makontena.

Bodi hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.

Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, ilitokana na kushindwa kuisimamia vyema TPA, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa katika Bandari ya Dar es Salaam bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli ambaye pia alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kutokana na ubadhirifu wa Sh bilioni 16 ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRL).

 JIPU LA RAHCO

Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito.

Uamuzi huo umelenga kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.

 JIPU LA TAKUKURU

Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Desemba 16, mwaka jana.

Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Rais Magufuli kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.

 JIPU LA NIDA

Januari 26, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza pia kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu.

Maimu alisimamishwa pamoja na maofisa wengine wanne wa NIDA kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.

Balozi Sefue alisema taarifa zilizomfikia Rais zinaonyesha kuwa NIDA hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh. bilioni 179.6 kiasi ambacho ni kikubwa.

 WALIOKIUKA AMRI YA KUSAFIRI NJE

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza  kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru ambao walisafiri nje ya nchi licha ya Serikali kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.

Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles