27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Wezi waiba swichi, milango ya zahanati

Na OSCAR ASSENGA – TANGAWATU wanaodhaniwa kuwa ni wezi, wameiba milango ya Zahanati ya Kwanjeka Nyota iliyojengwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga katika Mtaa wa Kwanjeka Nyota, Kata ya Mnyanjani.

Wizi huo uligundulika juzi wakati wa ziara ya Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbaruku (CUF) aliyekuwa akitembelea mradi wa mfereji wa maji machafu kutoka kwenye makazi ya watu kuelekea baharini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Mnyanjani, Thobias Haule, alisema wizi huo umefanyika kutokana na kutokuwapo kwa ulinzi katika zahanati hiyo.

Katika maelezo yake, Haule alimwambia mbunge huyo kwamba kuna uzembe umefanywa na halmashauri yao kwa kuitelekeza zahanati hiyo ambayo hadi wakati huo ilikuwa imeshajengwa kwa Sh milioni 147.

“Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila mtaa unakuwa na zahanati na kituo cha afya kiwe katika kila kata.

“Lakini ni jambo la kusikitisha kuona mtaa wetu umeshindwa kufikia lengo la Serikali la kuwa na zahanati baada ya mamlaka husika kuiacha zahanati yetu bila kuiendeleza na kusababisha vibaka kuiba milango.

“Mheshimiwa mbunge, hivi sasa ni takribani miaka mitatu tangu kuanza mchakato wa upatikanaji wa zahanati hiyo ambayo ingetusaidia wananchi wa maeneo haya kupata huduma kwa kuwa tumekuwa tukitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

“Kutokana na tukio hilo, nashindwa kuelewa na mara nyingi tukisema ukweli tunaonekana tunaleta siasa, lakini haya ni matokeo ya watendaji wetu kuwa na nguvu zinazopitiliza ambapo sasa unaona zahanati imekwisha, lakini bado samani za ndani hazipo.

“Kutokana na uzembe huu, vibaka wameiba milango na swichi za taa, nadhani wahusika hawachukui hatua kwa sababu fedha zilizotumika hapa ni za walipakodi,” alisema diwani huyo.

Awali akizungumzia suala hilo, Mbunge Mbaruku alisema alishazungumza na Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kuahidiwa kuitembelea zahanati hiyo ili kubaini chanzo kinachokwamisha isifunguliwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles