20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Wazo la Nundu wa TTCL linafikirisha

Na Jumanne Mwalusanya, Dar es Salaam

WIKI iliyopita, Kampuni ya simu ya TTCL ilitoa taarifa kwa wateja wake na Watanzania kwa ujumla kwamba inaendelea na mkakati wake maridhawa wa kuboresha huduma zake na kuzifanya za gharama nafuu kwa watumiaji wake.

Kwa watu ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa TTCL katika miaka ya karibuni, watabaini kwamba kati ya mwaka jana na mwaka huu pekee, kampuni hiyo imefanyia marekebisho mwonekano wa vituo vyake vya utoaji huduma nchini kote.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL, Omary Nundu, alisema kampuni hiyo iko katika mpango wa kuongeza huduma nyingine ili kukidhi haja ya soko la mawasiliano ambalo huwa linataka vitu vipya kila wakati.

Kuhusu mikakati ya mwaka huu, alisema kampuni yake inapambana na ushindani mkali kutoka kwa washindani wake sokoni na ndiyo sababu wanaumiza vichwa kila wakati ili kuchomoza na kuwa vinara.

Hata hivyo, alisema wana matarajio makubwa na ubunifu na uzalendo wa wafanyakazi wa TTCL aliosema kama watavitumia vizuri wanaweza kupeleka kampuni yao katika mafanikio makubwa zaidi.

Ni wazi kwamba Nundu alikuwa sahihi wakati akieleza kuhusu hali ya ushindani mkali iliyopo hapa nchini kwetu.

Kwa mujibu wa ripoti ya karibuni zaidi ya taasisi nguli ya masuala ya mawasiliano ya simu ya GSMA, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kampuni nyingi za simu zinazoshindana katika soko moja miongoni mwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Uwepo huu wa washindani wengi katika soko moja, kwa mujibu wa GSMA, ni mojawapo ya sababu zinazosababisha kupungua kwa faida miongoni mwa kampuni zinazoshindana katika soko hilo.

Kwa hakika kabisa, Nundu, alikuwa sahihi kuhusu hali halisi ya maendeleo na mafanikio ya teknolojia ya mawasiliano hapa nchini. Hata hivyo, Tanzania inahitaji kufanya kila linalowezekana kupunguza idadi ya kampuni washindani ili zibaki chache zitakazotoa huduma kwa kiwango cha juu zaidi.

Kimsingi, mkakati huo wa kuunganisha nguvu ni maarufu na unatumiwa na taasisi zinazohitaji uwekezaji mkubwa wa kimiundombinu ili kufikia malengo yake ya utoaji huduma.

Uwekezaji wa namna hii unahitaji fedha nyingi kufanikiwa na ndiyo sababu kila anapoongezeka mshindani mpya katika sekta husika, umuhimu wa mwingine kuwekeza zaidi huwa unapungua na uwezekano wa kurudisha gharama hizi ni mdogo kwa kila mwekezaji mpya anayeingia.

Kama taifa linahitaji kuvutia wawekezaji wakubwa wa namna hii, ni jambo la muhimu kuwaonyesha wenye mitaji kwamba bado kuna uwezekano wa kurejesha gharama zao na hatimaye kupata faida katika wanalotaka kulifanya.

Kwa maana hiyo, ingawa ni wazi kwamba sekta kama ya benki zinafaidika kwa kitendo cha kuunganisha nguvu pekee kwa sababu ya kuunganisha akili na ubunifu; sekta ambayo itafaidika zaidi na kuunganisha nguvu ni zile ambazo zinategemea miundombinu.

Hapa nchini Tanzania, sekta ambayo inaweza kuwa mfano wa hizi zinazotegemea miundombinu ni ile ya mawasiliano. Kwa sasa, sekta hiyo ina washindani wengi wadogo wadogo ambao unapata shida kuona wanapataje faida.

Kama kweli tunataka kupiga hatua za kutosha katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano inatoa mchango inaostahili katika maendeleo ya uchumi wetu, ni muhimu yakafanyika mabadiliko ya kimkakati.

Kwa mtazamo mwingine katika kutazama fursa za ukuaji mzuri wa uchumi wetu, ni wazi kwamba ziko sekta hapa nchini mfano mzuri ukiwa ni wa mawasiliano ambao kwa kweli zinahitaji kuunganisha nguvu ili zilete tija inayotakiwa.

Kwa bahati nzuri, baadhi ya jirani zetu wameanza kuona umuhimu wa hili na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa. Hatuna sababu ya kuachwa nyuma kwa vile ukweli uko wazi.

Ziko tafiti mbalimbali zinazoonyesha kwamba kuunganisha nguvu kumekuwa na mafanikio makubwa kokote duniani ambako yamefanyika na huu ndiyo mfumo ambao dunia inaenda nao kwa sasa.

Badala ya kubaki na kulalama kwamba mbona mambo hayaendi kama tunavyotaka, ni muhimu kuchukua hatua za makusudi na za kimkakati kuhakikisha sekta zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi, zinawekewa mazingira ya kufanya hivyo kwa haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles