27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Wazazi wachangishana fedha kutengeneza madawati Mbozi

Na Denis Sinkonde, Songwe

Wazazi wa Wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Nuru iliyopo kata ya Vwawa katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe wakishirikiana na diwani wa kata hiyo, George Kiwaya wamekubaliana kuchangishana fedha Sh milioni 12.5 ili kununua madawati 250 lengo likiwa ni kupunguza kero ya watoto kukaa chini wakiwa darasani.

Uamuzi huo uliafikiwa mbele ya diwani wa Kata ya Vwawa, George Kiwaya aliyefanya kikao cha wazazi wote pamoja na Ofisa Elimu Msingi wilayani humo, Bunka Matogolo kutafuta suluhu ya changamoto hiyo.

Diwani Kiwaya alisema baada ya kuonekana wanafunzi wanakaa chini wakiwa darasani wazazi hao waliamua kuunda vikundi vya watu watatu watatu ambao kila kikundi kitatengeneza dawati moja lenye ubora unaokubalika na Serikali.

George alisema shule hiyo inakadiliwa kuwa na wanafunzi 1,020 na madawati yanayotumika na wanafunzi hao ni 90, upungu wake ni madawati 250 ambapo uhitaji ni madawati 340, hali iliyowasukuma wazazi kufanya maamuzi ya kuchanga fedha ili kuwanusuru watoto kukaa chini ya sakafu.

“Wazazi na walezi wa wanafunzi hao wametambua mchango wa serikali katika kuchangia miradi ya maendeleo, hivyo uamuzi huo umefikiwa ili kusaidiana na serikali yao baada ya kuona Shule hiyo kuwa na wanafunzi wengi na kusababisha idadi kubwa wakae chini,” alisema Kiwaya.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo, Fauster Nzunda alisema serikali imejitahidi kuboresha shule hiyo na kwamba ni muda mwafaka kwa wazazi kuunga mkono.

“Kwa kutambua adha wanayokumbana nayo wanafunzi shuleni hapa wazazi waliamua kuunda vikundi vya watu watatu watatu ambao kila kikundi kitatengeneza dawati moja lenye ubora unaokubalika na serikali kwa gharama ya Sh 50,000 ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki,” alisema Nzunda.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wilayani humo, Bunka Matogolo amepongeza uamuzi wa wazazi hao na kwamba changamoto za elimu zitapungua endapo wataendeleza ushirikiano baina yao pamoja na viongozi wa serikali kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo.

“Serikali imeukubali uamuzi wa wazazi na kwamba kwa upande wake itaendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya shule hiyo na kwamba hivi sasa serikali imeipatia shule hiyo Sh milioni 12.5 kukarabati madarasa,” alisema Matogolo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles