25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Wazazi kuweni makini nyakati hizi za Sikukuu

Na JANETH MUSHI, ARUSHA

WAKRISTO nchini na duniani kote leo wanasherehekea Sikukuu ya Pasaka. Pamoja na mambo mengine, nyakati za sikukuu kumekuwapo na matukio mbalimbali hasa yanayowahusu watoto.

Licha ya Jeshi la Polisi kukumbusha wazazi pamoja na walezi na kupiga marufuku ya kufanyika kwa burudani za watoto ikiwemo disko toto katika kumbi mbalimbali za starehe,bado kuna baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakipuuzia suala hilo.

Baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na tabia ya kuwaacha watoto wakiranda mitaani na yanapotokea majanga katika sehemu hizo huanza kuinyooshea kidole Serikali.

Ni jambo jema watoto kufurahi siku za sikukuu lakini wazazi na walezi wanawajibu wa kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama wakati wote. 

Endapo wanataka kuwaruhusu kwenda kutembea ni vema waambatane na watu wazima ili wawalinde.

Pamoja na kuwalinda ni vema wazazi na walezi wafahamu watoto wao wanakwenda maeneo gani ya starehe kwani linapotokea tatizo ni rahisi kujua pia itasaidia kuripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili msaada wa haraka ufanyike.

Siku za sikukuu baadhi ya madereva huendesha magari pasipo kuchukua tahadhari pia vijana wengi mitaani huanzisha vurugu na wengine hufikia kupigana, matukio hayo husababisha watoto kuumia au kupotea. 

Nami natumia fursa hii kuwaasa wazaza na walezi kuwasihi kuwa waangalifu juu ya watoto, na watambue kuwa maeneo ya starehe yanayohusisha watoto si sehemu salama kwao.

Mbali na matukio mengine yakiwamo kuumizana disko toto huchangia mmomonyoko wa maadili kwa kuwa hakuna mtu anayewasimamia.

Tumeshuhudia baadhi ya wazazi bila kujali chochote huwaacha watoto wajilinde wenyewe, wakati mwingine huwachanganya watoto wasioweza kuongea kutokana na umri wao kuwa mdogo hivyo linapotokea tatizo inakuwa vigumu kuwafahamu wazazi.

Vitendo vya kikatili kwa watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti,ni miongoni mwa matukio yanayowaathiri watoto, nyakati kama hizi za sikukuu watu wenye nia ovu hutumia mwanya huo kuwalaghai watoto na kuwafanyia unyama huo.

Wazazi na walezi msisubiri maafa ama matukio yatokee ndipo muone umuhimu wa kuwalinda watoto, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikisha mtoto anakuwa salama hii itasaidia kupunguza ama kumaliza ukatili dhidi ya watoto.

Nawatakia Sikukuu njema,tusherehekee kwa amani na utulivu!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles