23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Waumini KKKT wasubiri ‘moshi mweupe’ kesho

JANETH MUSHI NA ELIYA MBONEA-ARUSHA

 MACHO na masikio ya waumini wengi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), yapo mkoani Arusha ambako kesho wanatarajia kupata Mkuu wa Kanisa hilo atakayeliongoza kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Mkutano Mkuu wa kanisa hilo, ulianza juzi Chuo Kikuu cha kanisa hilo cha Makumira mkoani Arusha.

Pamoja na kuwa Askofu Dk. Fredrick Shoo, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa kanisa hilo anapewa nafasi kubwa ya kumalizia miaka mingine minne ya kipindi cha pili, inaelezwa kuwa anaweza kukumbwa na upinzani.

Mara nyingi kwa utaratibu wa kanisa hilo, Kiongozi wa Kanisa akimaliza muhula wake wa kwanza wa miaka minne, hupewa nafasi nyingine ya kumaliza muhula wa pili wa miaka minne.

Hata hivyo, kwa upande wa Dk. Shoo, kutokana na misimamo yake mbalimbali, inaelezwa baadhi ya majina yanaweza kupita ili wapigiwe kura, huku ikielezwa kuwa kuna maaskofu nane ambao msimamo wao unajulikana kwamba wanataka mtu mwingine apatatikane kuongoza kanisa hilo.

Jana Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Solomon Masangwa, akizungumzia uchaguzi huo, alisema wajumbe wanapaswa kumuomba Mungu awape kiongozi anayependeza moyo wa Mungu.

 “Bado hatujafikia ajenda ya uchaguzi, ila wajumbe wa mkutano tunapaswa kumuomba Mungu atupe kiongozi anayeupendeza moyo wa Mungu,” alisema Askofu Dk. Masangwa na kuongeza:

 “Kuupendeza moyo wa Mungu ni kuwa na upendo kwa watu wake na ukombozi kwa watu wake, Mungu hapendi tupotee lakini tufikie ustawi mzuri kiroho, kiuchumi, kimwili, kisiasa pamoja na kijamii,” alisema.

Juzi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa 20, Dk. Shoo aliwataka Wakristo kutenda kwa upendo na kuacha kuwahukumu wengine ikiwamo kuwafanyia kile wasichopenda wao kufanyiwa.

Akizungumza kwenye ibada hiyo, Askofu Dk. Shoo alisema; “Wakristo tuendelee kutenda kwa upendo, tusihukumu wengine. Tusilotaka wengine watufanyie basi tusiwafanyie.

“Ni muhimu matendo yetu ya upendo sisi kwa sisi yawavute walio nje ya kundi letu wamwamini Yesu.”

 Akifungua mkutano huo kwa neno kutoka kitabu cha 1 Wakorintho. 16: 13-14, Askofu Dk. Shoo alisisitiza kwamba Wakristo wanapaswa kukesha, kusimama imara katika imani ya Kristo Yesu aliye msingi imara. 

“Tunapaswa kuwa hodari wenye akili na kuitetea imani yetu. Lakini pia kuwa imara katika kujibu sawasawa na neno la Mungu,” alisema Askofu Dk. Shoo aliyeongoza ibada hiyo akishirikiana na Askofu Dk. Elias Nassari ambaye ni Mkuu wa Dayosisi ya Meru.

Aidha, alisema Kanisa linakutana na changamoto zinazozuia Wakristo wasiishi imani yao ipasavyo. Hivyo aliwataka wasiyumbishwe bali wawe imara kuishuhudia imani na kuwa huru katika Yesu aliyewaita.

 “Lengo la Mkutano Mkuu wa 20 ni kuangalia jinsi talivyoenda pamoja na jinsi tutakavyoendelea mbele pamoja.

“Kanisa ni mahali watu wanaweza kuona neema ya Mungu na kuishi kwa umoja katika kulichunga kundi, kuaminiana na kusaidiana hata katika tofauti zetu za kieneo, mapokeo, na misimamo.

“Suluhisho la migogoro ni kupendana, kushauriana ili kusonga mbele. Waefeso 4 inasema wala tusimpe ibilisi nafasi. Tuenende kama wito tulioitiwa ulivyo katika upendo na umoja katika kifungo cha amani.

 “Niwaombe viongozi na washarika kwa ujumla kuwa makini na mafundisho potofu kutoka kwa yeyote, bali kudumu katika kweli ya Mungu na tusiwe watumwa wa ukanda na siasa, bali tuwe imara kutenda lililo jema bila kulipa kisasi,” alisema Askofu Shoo.

Baadhi ya maaskofu wanaotajwa kuchuana na Dk. Shoo ni Askofu wa Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile, Askofu Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk. Abednego Keshomshahara na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa.

 Dk. Shoo alichaguliwa Agosti 2015 baada ya kuwashinda maaskofu wenzake wawili ambao ni Dk. Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare.

 Katika uchaguzi huo, Dk. Shoo alipata kura 153, huku Dk. Munga akipata kura 67, ikiwa ni baada ya kurudiwa mara tatu kutokana na mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.

 Kanuni za uchaguzi za KKKT zinaeleza kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura zisizopungua theluthi mbili ya zote zilizopigwa na iwapo mshindi hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi ndiyo yatakayopigiwa tena kura.

 Iwapo theluthi mbili haitapatikana katika duru la pili, kura ya wingi au uchache itatumika kwa duru la tatu kumpata mshindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles