31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yataja vipaumbele vitano SADC

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, ametaja mambo ambayo Tanzania itayasimamia katika kipindi ambacho ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Kabudi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, alisema mambo hayo ni kutengeneza mpango kazi wa kila nchi utakaosaidia kutekeleza kaulimbiu na kubainisha miradi ya viwanda na uwekezaji ambayo inaweza kutumiwa na nchi nyingine.

Mengine ni kuhamasisha wataalamu wa lugha ya Kiswahili kujifunza lugha nyingine za kigeni waweze kuchangamkia fursa baada ya lugha hiyo kuwa rasmi katika jumuiya hiyo.

Mengine ni kusimamia suala la Burundi la kutaka kuwa mwanachama wa jumuia hiyo, kueneza kampeni Zimbabwe iondolewe vikwazo na kuondoa vikwazo visivyo vya forodha ili kuongeza biashara baina ya nchi wanachama.

Akizungumza jana wakati wa mkutano na wahariri na wakuu wa vyombo vya habari, Profesa Kabudi alisema kuna mambo mbalimbali ambayo wakimaliza uenyekiti watapaswa wazionyeshe nchi wanachama namna walivyoyatekeleza.

“Tuna mwaka mzima na kuanzia sasa kutakuwa na shughuli mbalimbali na mikutano ya kisekta isiyopungua 30, tutasimamia kaulimbiu ambayo sisi Tanzania tumeichagua.

“Ni lazima tuwe na mazingira wezeshi na shirikishi kwa lengo la kuwa na mkakati wa viwanda endelevu kusaidia kuongeza biashara kati yetu na kuchochea watu kufanya kazi,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema wanaunga mkono Burundi ipewe uanachama katika jumuiya hiyo kwa sababu imeshatimiza asilimia 70 ya vigezo na kwamba watahakikisha sekretarieti inaendelea kufanyia kazi mambo ambayo bado hayajakamilika ili yakamilike.

Kuhusu suala la Zimbabwe, alisema wataendelea kupiga kampeni kushinikiza jumuiya za kimataifa ziiondolee vikwazo nchi hiyo na Oktoba 25 nchi zote za SADC zitakuwa na matukio tofauti kuendeleza kampeni hiyo.

“Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa mwaka huu, Tanzania itasimama kuiambia dunia kwamba Zimbabwe haistahili kuwekewa vikwazo, wanaoumia ni watoto na wanawake wasiokuwa na hatia,” alisema.

Profesa Kabudi pia aliwataka wataalamu wa Kiswahili walioko nchini wajifunze lugha za kigeni kama Kireno na Kifaransa kwani anayeliwahi soko ndiye analimudu na kulimiliki.

Alisema waliwaeleza wajumbe kuwa Kiswahili si lugha ya kibantu, bali ni lugha ya ukombozi na kinachoitofautisha na lugha nyingine ni lugha pekee ya Waafrika wote.

“Udhaifu wetu Watanzania tunadhani sisi peke yetu ndiyo tunaohodhi Kiswahili, matokeo yake Kenya na DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) ndio wanapeleka wataalamu na walimu wengi nje, na Watanzania wachache walioko huko hawaji kuwatafuta wenzao.

“Mshindani wetu mkubwa katika Kiswahili ni DRC, kuanzia Boma hadi Lubumbashi ni wazungumzaji wa Kiswahili, hivyo tusipochangamkia watakaofaidika ni wengine na Serikali haiwezi kuja kukulazimisha ujifunze Kireno,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, suala jingine watakalolisimamia ni kuondoa vikwazo visivyo vya forodha ili kuongeza biashara baina ya nchi wanachama wa SADC.

“Moja ya vitu ambavyo vimefanya biashara kuwa ngumu kwa SADC ni vikwazo visivyokuwa vya forodha, tutakuja na mkakati wa kuviondoa ili kuhakikisha biashara zinafanyika kwa haraka. Mfano bidhaa ambazo TBS (Shirika la Viwango Tanzania) imethibitisha zisilazimike kwenda kupimwa tena sehemu nyingine.

“Turahisishe kanuni za uingizaji bidhaa baina ya nchi na nchi, bila kuondoa vikwazo jitihada zetu za kuongeza biashara SADC hazitafanikiwa… ni eneo ambalo ni muhimu tulifanyie kazi,” alisema Profesa Kabudi.

KILICHOWAVUTIA MARAIS

Profesa Kabudi alisema mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa kwani baadhi ya wageni walionyesha namna walivyovutiwa na mambo mbalimbali ikiwemo hotuba iliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli na vyakula.

“Marais wote waliomba wapewe nakala ya hotuba ya Rais Magufuli kwa sababu inaonyesha wapi Afrika inaelekea na kwenye chakula usiseme, wengine waliomba wapewe vitabu vya mapishi,” alisema.

Profesa Kabudi alivishukuru vyombo vya habari kwa kazi kubwa ya kuhabarisha umma wakati wa mkutano huo akisema vimeifanya Tanzania ionekane na isifike.

“Nilipewa kazi ya kusimamia SADC ndiyo maana leo (jana) nimekuja kuwashukuru, kila taifa duniani lina mambo yake makubwa na miongoni mwa mambo ambayo tulishikamana pamoja ni mkutano wa SADC, waliokuwa na shaka na nafasi ya Tanzania katika uongozi wa SADC sasa wameelewa,” alisema Profesa Kabudi.

Kwa upande wao, wahariri waliiomba Serikali kuendelea kuvishirikisha vyombo vya habari katika masuala mbalimbali ya kitaifa ili waweze kutoa mchango wao kwa manufaa ya taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles