23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

Watumishi watatu Mamlaka ya maji Igunga mbaroni

Na Allan Vicent, Igunga 

Jeshila Polisi wilayani Igunga mkoani Tabora linawashikilia watumishi watatu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira wilayani humo (IGUWASA) kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ubadhilifu na kuisababishia hasara ya Sh milioni 671.  

 Mkurugenzi wa IGUWASA, Hussein Nyemba ametaja watumishi wanaoshikiliwa kuwa ni Benedict Bayo(34) ambaye ni Ofisa Biashara wa Mamlaka hiyo, Alex Julius (33) wa kitengo cha ufundi na Daniel Matandiko (31) msoma mita.

Amesema watumishi hao walikamatwa kutokana na maazimio ya kikao cha wadau wa maji na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kilichoketi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Nyemba alieleza kuwa alipohamishiwa katika wilaya hiyo alikuta mamlaka hiyo ikiwa na changamoto nyingi za ubadhilifu ikiwemo wizi wa maji kwa baadhi ya wananchi wakishirikiana na baadhi ya watendaji wa IGUWASA.

Aliongeza kuwa baada ya kufanya uchunguzi walibaini wateja zaidi ya 810 mita zao zinasoma sifuri kwa miezi mitatu huku wakitumia maji na kuongeza kuwa kila mwezi Mamlaka inapoteza maji kwa asilimia 50 kutokana na hujuma hizo.

 Aidha, aliongeza kuwa uchunguzi ulibaini baadhi ya magati hayajaingizwa kwenye mfumo huku baadhi ya fedha za makusanyo zikitumiwa kinyume na utaratibu kwa matumizi binafsi.

Mkurugenzi amethibitisha kuwa kutokana na upotevu wa mapato hayo wanadaiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (KASHUWASA) zaidi ya Sh milioni 671 na tayari Mamlaka hiyo imetishia kuwakatia maji ifikapo Mei 25, mwaka huu kama hawatalipa fedha hizo.

 Amefafanua kuwa baada ya kuona hali hiyo alilazimika kuitisha kikao cha dharura cha wadau wa maji kikihusisha viongozi wa dini, wateja, vyama vya siasa na kamati ya ulinzi na usalama ambacho kiliongozwa na mkuu wa wilaya hiyo.

Ili kukabiliana na wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu katika wilaya hiyo alisema wamenunua pikipiki 10 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20 zitakazotumika kwenye ufuatiliaji na kubainisha kuwa hawatakuwa na huruma kwa mtumishi yoyote atakayebainika kufanya hujuma.

Mwenyekiti wa Chama cha UDP wilayani humo, Mbogo Athuman alimpongeza Mkurugenzi kwa kubaini ubadhilifu huo na kuitisha kikao cha wadau ambacho ndiyo kimeagiza kukamatwa watuhumiwa hao, alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufichua wezi wa maji.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Lucas Bugota alisikitishwa na hujuma iliyofanywa na watumishi hao huku akiwataka watendaji wote wa IGUWASA kubadilika na kuachana na hujuma hizo.

 Naye Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Anwary Kashaga alisema Chama hakiko tayari kuona watumishi wa umma wakihusika kuhujumu miradi ya wananchi, aliagiza kusakwa na kufikishwa mahakamani wahusika wote.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, ACP Safia Jongo alithibitisha kushikiliwa watumishi hao wa Mamlaka ya Maji IGUWASA na kuongeza kuwa uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili unaendelea.  

 Alitoa wito kwa watumishi na umma kuacha tabia za kujihusisha na vitendo vya uhalifu hivyo akawataka kuwa waadilifu na waaminifu katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,303FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles