25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi wa umma watengewa Sh bil 600

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

SERIKALI imesema imetenga Sh bilioni 600 kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi wa umma kwa mwaka wa fedha 2019/20, ikiwa ni moja ya mkakati wa kuleta nidhamu na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.

Hayo yalisemwa Dodoma  jana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipojibu swali la msingi la Mbunge wa Bumbwini, Muhammed Amour Muhammed, aliyetaka kujua ni lini Serikali italipa madeni ya watumishi wa umma kutokana na madeni hayo kuongezeka.

Alisema Serikali imetenga Sh bilioni 600 ambazo zimeidhinishwa na Bunge kugharamia malipo ya madeni mbalimbali ikijumuisha madeni ya watumishi kwa mwaka wa fedha 2019/20.

“Hadi kufikia Machi, 2020 jumla ya Sh bilioni 364.7 zimelipwa kama madai ya watumishi, wazabuni na wakandarasi ambapo kati ya hizo kiasi cha Sh bilioni 97.6 zimelipwa kama madeni ya watumishi pekee,” alieleza Dk. Kijaji.

Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2015/16 hadi 2019/20, Sh bilioni 375.7 zilitolewa kugharamia madeni mbalimbali, kati ya fedha hizo Sh bilioni 113.8 zilitumika kulipa madeni ya mshahara na Sh bilioni 261.9 madeni yasiyo ya mshahara.

Dk. Kijaji alisema kutokana na changamoto ya uwepo wa madeni hewa, Serikali ilizuia ulipaji wa madeni kabla ya kuhakikiwa lengo likiwa kuleta nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Alisema kutokana na takwimu hizo, Serikali inajisikia fahari na inahitaji kupongezwa kutokana na juhudi mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha madeni yote ya watumishi yanalipwa kwa wakati ikithibitika yana uhalali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles