24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

WATUMIAJI INTANETI WAFIKIA MILIONI 11

Na Mwandishi wetu


HALI ya mwenendo wa kubadilika badilika katika sekta ya mawasiliano ya simu ndiyo sababu ya msingi ya ubunifu na uboreshaji endelevu katika namna ambavyo waendeshaji wa mitandao ya simu wanavyoendesha biashara zao.

Katika sekta ambayo tegemeo lake kuu linazungukia katika ushindani mkali,  kampuni haziwezi kubakia katika mafanikio pasipo kutazama hatari itakayo jitokeza katika biashara yao.

Kwa hiyo ni muhimu kwa kampuni ya mawasilino kuimarisha teknolojia mpya na kuongeza ubunifu  kuhakikisha mipango yao inatimia.

Inatosha kusema kwamba, mahitaji ya wateja daima yatakuwa ndio msukumo muhimu utakaosababisha kampuni za simu kutoa kipaumbele katika uboreshaji endelevu wa huduma zao hasa mitandao yao.

Hivi majuzi Tigo Tanzania, ikiwa inaelezea vipaumbele vyake katika uboreshaji wa programu ya mtandao wao, walisema kwamba mwaka jana iliwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 75 katika uboreshaji wa miundominu ya mtandao wao.

Akizungumza na wahariri jijini Dar es salaam, Ofisa Mkuu wa Ufundi na Habari (CTIO) Jerome Albou, alitaja vipaumbele vya mpango wa kampuni katika kuboresha mitandao yao.

“Tigo imewekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 75 katika mradi mkubwa wa mageuzi ya mtandao unaolenga kuboresha kiwango cha mtandao ili kutoa huduma bora kwa wateja. Juhudi hizo zimesaidia kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaojiunga na vifurushi vya data ndani ya mwaka mmoja.”

Albou alifafanua kwamba moja ya malengo ya kimkakati ya Tigo ni kubadilisha huduma kwa wateja wa intaneti  yake kwa kutoa mtandao bora na wenye ufanisi kulingana na viwango ya sekta ya mawasiliano katika teknolojia ya 3G na 4G.

Albou anasema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Tigo imeweza kuongeza idadi ya wateja wake kufikia zaidi ya milioni 10, hivyo kuifanya kuwa kampuni ya pili ya uendeshaji wa mtandao Tanzania.

“Kadri tunavyoendelea kukua, upanuaji wa mtandao na uboreshaji kwa kuweka vifaa vya kisasa ni muhimu katika kutoa huduma za kiwango cha juu.  Kutoka mwaka jana 2016, tumefanya upanuzi mkubwa wa miundombinu yetu kwaajili ya kuongeza upatikanaji wa mtandao wetu na kuboresha uwezo; cha muhimu zaidi kuboresha huduma zetu katika huduma za broadband,” aliongeza Albou.

Kwa mujibu wa Albou, uwekezaji huu ni mwendelezo wa mpango wa kampuni kuboresha mtandao ikiwa ina lengo la kuwawezesha wateja wake kufurahia huduma bora.

“Katika kuwapatia wateja wetu furaha ya maisha ya kidigitali, hatujawekeza tu katika teknolojia ya kuboresha na kuongeza mikongo bali pia tumekuwa tukiboresha upanuzi wa huduma ambapo tumeshuhudia kuongezeka kwa uwezo wa 4G LTE hadi maeneo 95 yenye minara 300 yaliyoko katika maeneo maalumu mbalimbali ya nchi.

Tumeongeza 3G yetu kufikia maeneo 535, yenye minara 1,500 nchini kote wakati huo huo tukiboresha mingine,” anasema Albou.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya watu  milioni 31.86 ambao ni sawa na asilimia 67 ya idiadi ya watu wote Tanzania wanamiliki simu za mikononi.

Ripoti hiyo pia inaainisha kuwa watumiaji wa intaneti wameongezeka kwa asilimia 22 kufikia watu milioni 11.2 katika robo ya kwanza ya mwaka huu tangu 2013. Ongezeko hili la haraka kwa wateja wanaojiunga, imesababishwa na kuongezeka kwa kasi ya matumizi ya data, hali hii inaweza kuwa imelazimu kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa hisia za kuboresha upatikanaji na uboreshaji wa mitandao ya simu, na Tigo ikiwa mojawapo ya kampuni zilizoona umuhimu huo.

Inaonekana kwamba, uboreshaji wa mtandao wa Tigo umeanza kuzaa matunda kama ambavyo imeshuhudiliwa na baadhi ya wateja ambao wameshaanza kufurahia mtandao mpya.

Mhariri mmojawapo wa kituo maarufu cha TV hapa nchini, alitoa maoni yake na kusema kuwa kituo kimeshuhudia ufanisi mkubwa wa mtandao wanapokuwa wanatumia interneti ya Tigo kwaajili ya majukumu ya kiofisi na binafsi mjini na muhimu zaidi ni maeneo ya vijijini.

“Tofauti na mitandao mingine, sasa tunapata huduma yenye kasi, yenye ufanisi na utendaji safi hasa wakati tunapofanya matangazo ya moja kwa moja ya video kutoka katika ukumbi wa Bunge Dodoma,” alisema mhariri huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.

Peter Cephas, mwandishi mchapishaji mwenye maslahi ya kitaaluma nchini, naye alitoa maoni kama hayo akisema: “Tangu mwaka jana, nimeona mabadiliko makubwa kwenye mtandao wa Tigo; sasa ninaweza kupiga simu kwa urahisi na kutuma data kwa ufanisi pasipo usumbufu tofauti na mitandao mingine.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles