23.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Watu 12 wauawa shambulio la risasi Marekani

VIRGINIA BEACH, MAREKANI 

WATU wapatao 12 wameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa akiwemo ofisa wa polisi katika shambulio la risasi kwenye jengo la Serikali mjini hapa juzi.

Jengo hilo kawaida huwa na watu wapatao 400 wanaofanya kazi katika ofisi tofauti.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kames Cervera alisema mshambuliaji ambaye alikuwa mfanyakazi wa jengo la manispaa aliuawa baada ya polisi kuwasili katika eneo hilo na kumkabili.

Shambulio hilo lilitokea saa kumi jioni baada ya mshambuliaji aliyekuwa na silaha kuingia katika jengo hilo na kuanza kufyatua risasi holela. 

Watu wanne waliopata majeraha wamefikishwa hospitali karibu na eneo hilo.

Mtu mmoja aliuawa akiwa ndani ya gari lake, wakati wengine walikuwa ndani ya jengo hilo la ghorofa tatu.

“Kutokana na milio ya risasi, maofisa wa polisi wanne waliweza kujua mshambuliaji alikuwa ghorofa gani ya jengo alipokuwa akiendeleza mashambulizi. Haraka walianza kumshambulia, na naweza kusema yalikuwa ni mapambano ya muda mrefu.

“Wakati wa makabiliano hayo ya risasi, maofisa wa polisi walifanikiwa kumzuia mshambuliaji kuendeleza mauaji zaidi ndani ya jengo,” alisema Cervera.

Kulingana na Carvera, mapigano kati ya mshambuliaji huyo na polisi yalichukua muda mrefu.

Maofisa wa polisi hawakutaja jina la mshambuliaji huyo, na nia yake bado haitambuliki, lakini walisema alikuwa mfanyakazi wa muda mrefu katika jengo hilo, na aliuawa wakati wa makabiliano na polisi.

Miongoni mwa waliojeruhiwa ni ofisa mmoja wa polisi, ambaye alinusurika kwa kuvaa vesti ya kuzuia risasi. 

Eneo la kandokando ya jumba hilo, lenye majumba mengi ya Serikali lilifungwa na wafanyakazi wa Serikali kuondolewa.

”Tuliwasikia watu wakipiga makelele, wakiwataka watu kutoka ndani ya majumba hayo,” msaidizi mmoja katika jumba hilo, Megan Banton alikiambia kituo kimoja cha runinga – WAVY.

“Haya ni maafa mabaya kwa wakaazi wa Virginia beach,” alisema gavana wa Virginia, Ralph Northam katika mtandao wa Twitter.

Naye Meya wa Virginia Beach, Bobby Dyer aliwaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo ni baya zaidi katika historia ya mji huo.

“Huu ni mkasa wa kusikitisha zaidi mjini Virginia Beach, watu walioathirika na mkasa huu ni marafiki zetu, wafanyakazi wenzetu na majirani zetu,” alisema Dyer. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, maofisa wa ujasusi wa FBI walikuwa katika eneo hilo kuwasaidia maofisa wa Serikali za mtaa kuchunguza shambulio hilo. 

Rais Donald Trump aliarifiwa kuhusu shambulizi hilo na Ikulu imesema anafuatilia kwa karibu.

Kulingana na kundi la kufuatilia mashambulizi ya bunduki nchini hapa – Gun Violence Archive, hili ni shambulio la 150 mwaka huu la kuua watu wengi kwa kutumia risasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,183FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles