33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Mlinzi wa zamani wa Kagame auawa Afrika Kusini

CAPE TOWN

-AFRIKA KUSINI 

MLINZI wa zamani wa Rais Paul Kagame wa Rwanda,  Camille Nkurunziza, ameuawa na watu wenye silaha katika Jiji la Cape Town nchini hapa.

Nkurunziza ni mtu wa pili mwenye hadhi ya juu kuuawa nchini hapa baada ya mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa Ujasusi  nchini Rwanda, Kanali Patrick Karegeya mwaka 2014.

Waziri wa Nchi wa Rwanda anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Olivier Nduhungirehe, aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa Nkurunziza aliuawa na polisi wa hadhi ya juu baada ya kukataa kukamatwa akihusishwa na kitendo cha kuteka gari.

Taarifa nyingine zinaeleza kuwa gari hilo analohusishwa Nkurunziza kuteka ni aina ya Toyota Etios.

“Hivyo, Camille Nkurunziza, mfuasi wa kundi la kigaidi la RNC la Kayumba Nyamwasa na lile la FLN la Callixte Nsabimana (Sankara), alikuwa pia ni mtekaji nchini Afrika Kusini. Aliuawa jana (juzi) jioni na polisi wa hadhi ya juu wakati alipokataa kukamatwa akiwa na kisu. Unapokuwa mhalifu, ni mhalifu siku zote,” aliandika waziri huyo kupitia Tweeter Ijumaa.

Kifo cha Nkurunziza kimekuja siku chache baada ya Meja  Callixte Nsabimaana anayefahamika kwa jina jingine la Sankara, kiongozi wa waasi aliyekuwa akituhumiwa kupanga mauaji katika maeneo ya mipaka ya Rwanda kutiwa hatiani kwa kosa la ugaidi na mengine, na aliripotiwa kukiri kufanya kazi na Serikali za mataifa mengine dhidi ya Rwanda.

Inaelezwa Nkurunziza baada ya kumgeuka Rais Kagame na kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini, huko alikutana na Meja Sankara.

Tangu alipokimbilia huko na kukutana na Meja Sankara, inaelezwa alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Kagame, akimshutumu kuwa hana uvumilivu na maoni yanayompinga.

Meja Sankara alikamatwa mwezi uliopita akihusishwa na kundi la National Liberation Front (FLN), akishutumiwa kufanya uasi na zaidi mashambulio ndani ya Rwanda kutoka katika eneo la msitu karibu na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aliripotiwa kutiwa hatiani kwa makosa 16, ikiwamo ugaidi na mauaji, na kupewa masharti ya msamaha kwa uhalifu wake.

Desemba mwaka jana, Meja Sankara alidai kuwajibika kwenye tukio la kuchoma moto basi la abiria katika msitu wa Nyungwe – eneo ambalo ni maarufu kwa watalii wanaofika kutazama sokwe.

Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wawili na wengine wengi wakiwa wamejeruhiwa. 

Mashambulio hayo yalisababisha nchi za Magharibi zikiwamo Ufaransa, Ujerumani, Canada na Australia kuwashauri raia wake kutotembelea eneo hilo.

Ukiacha uhusiano wake wa karibu na Meja Sankara inaelezwa kuwa Nkurunziza pia ni ndugu wa Sajenti Innocent Karisa ambaye alitekwa nchini Uganda mwaka 2013 na kwa sasa yupo jela nchini Rwanda baada ya kutuhumiwa kuwa mfuasi wa kundi pinzani la Rwanda National Congress.

Wakati hali ikiwa hivyo, kwa upande mwingine inaelezwa Nkurunziza atakumbukwa kwa kuanzisha kampeni aliyoipa jina  la ‘Kipindi cha tatu cha Kagame’, ambayo ilijizoelea umaarufu mkubwa kwa wapinzani nchini Rwanda.

Mkuu wa Majeshi wa zamani wa Rwanda, Jenerali Nyamwasa naye pia aliwahi kunusurika majaribio mawili ya kuuawa.

Jenerali huyo alikimbilia uhamishoni Johannesburg mwaka 2010 baada ya kile kinachoelezwa kuwa ni kutofautiana na mshirika wake wa zamani, Rais Kagame.

Miezi michache baadaye alipigwa risasi mjini Johannesburg, lakini Rwanda ilikanusha kuhusika na shambulio hilo ambalo alipona.

Kundi alilomo Sankara la FLN linaloendesha harakati zake za kudai mabadiliko ya kidemokrasia likiwa na silaha, ni kundi la upinzani lililoanzishwa na Paul Rusesabagina, hotelia ambaye matendo yake wakati wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994 yalichezewa filamu huko Hollywood ikipewa jina la ‘Hotel Rwanda’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,079FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles