30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Watoto wa mitaani 6,300 wametambuliwa

Ramadhan Hassan

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, imesema jumla ya watoto 6,393 kutoka mikoa sita nchini wanaoishi na kufanya kazi mitaani wametambuliwa.

Mikoa hiyo sita ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha na Iringa.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Faustine Ndugulile aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomary Khamis (CCM).

Katika swali lake, mbunge huyo alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa mitaani jijini Dar es Salaam hali ambayo inakosesha watoto hao haki zao za msingi kama elimu na malezi bora, huku akihoji Serikali imechukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo la watoto wa mitaani.

Akijibu swali hilo, Dk. Ndugulile alisema katika idadi hiyo watoto wa kiume ni 4,865 na wa kike 1,528 na kwamba walikuwa wakiishi mitaani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kufiwa na wazazi, migogoro ya familia, kutengana kwa wazazi, vitendo vya unyanyasaji na ukatili na umasikini katika ngazi ya kaya na kusababisha ongezeko la watoto hao.

“Taarifa ya utafiti ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani uliofanywa na Wizara Mei mwaka 2018, ilihusisha mikoa sita nchini, ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha na Iringa na jumla ya watoto wapatao 6,393 wakiwemo wa kiume 4,865 na wa kike 1,528 wanaishi na kufanya kazi mitaani walitambuliwa,” alisema Dk. Ndugulile.

Aidha, alisema katika kipindi cha Oktoba mwaka 2018 hadi Machi mwaka 2019 jumla ya watoto 2,702 walipatiwa huduma mbalimbali ambapo Mkoa wa Arusha watoto (330), Dar es Salaam (475), Dodoma (337), Iringa (313), Mwanza (770) na Mbeya (447).

“Huduma zilizotolewa ni pamoja na huduma za afya, chakula, malazi, kurudishwa shuleni, stadi za ufundi, stadi za maisha, kuunganishwa na familia pamoja na msaada wa kisaikolojia na kijamii,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau, inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto wakiwamo walio katika mazingira hatarishi.

“Pia itaendelea kuwajengea uwezo wazazi na walezi kwenye eneo la stadi za malezi na ulinzi wa watoto,” alisema Dk. Ndugulile.

Alitoa rai kwa jamii kuhakikisha jukumu la matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto linatekelezwa ipasavyo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles