28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Shonza: Serikali haipendelei chombo chochote cha habari

Ramadhani Hassan

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema Serikali imekuwa ikichukua hatua bila kupendelea chombo chochote cha habari kinachobainika kukiuka sheria na taratibu ikiwamo kutoa habari za uongo. 

Hayo yalielezwa bungeni jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza wakati akijibu swali la nyongeza ya Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF).

Katika swali lake, mbunge huyo alidai kuwa ameshuhudia baadhi ya vyombo vya habari, hususani magazeti yakipewa adhabu ya kufungiwa kwa kutoa habari za uongo, lakini kuna mengine ambayo hayachukuliwi hatua zozote pamoja na kwamba yanadhalilisha na kuchafua watu.

Alihoji ni kwanini Serikali haichukui hatua kwa vyombo hivyo pamoja na wamiliki wake.

Akijibu swali hilo, Shonza alisema suala hilo halina ukweli kwa kuwa Serikali inafanya kazi kwa kusimamia sheria na kanuni zilizopo.

“Mara zote ndani ya Bunge tumekuwa tukifafanua kwamba wizara tumekuwa tukichukua hatua kwa magazeti yanayokiuka sheria.

“Si kweli kwamba hatuchukui hatua kwa magazeti ya Tanzanite kama alivyosema mbunge, tumeshajibu mara kadhaa humu ndani kwamba tumeshawaandikia onyo pamoja na mengine yaliyokuwa yanakiuka sheria,” alisema Shonza.

Alisema kuwa sheria ya habari inaeleza kwamba kabla ya kuchukua hatua yoyote kwa chombo chochote cha habari, cha kwanza wanapaswa kupewa onyo mara ya kwanza.

“Tunatoa nafasi kwa mara ya pili, pale ambapo tunaona kwamba hali hiyo inazidi ndio tunachukua hatua,” alieleza Shonza.

Alisema hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa bila upendeleo.

“Sisi kama wizara tumekuwa tukichukua hatua pale ambapo tunaona tumeshaonya mara kadhaa, lakini bado hawajajirekebisha,” alisema Shonza.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alisema ni kosa la jinai kwa mtu au vyombo vya habari kutoa, kuandika, kusambaza au kutangaza habari za uongo.

Alihoji Jeshi la Polisi linachukua hatua gani stahiki kwa watu au vyombo vya habari vinavyofanya makosa hayo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema jeshi hilo linao utaratibu unaotumika pindi mtu anapokuwa ametenda makosa ya jinai ambapo ushahidi hukusanywa kisha jalada huandaliwa kwenda kwa Mwanasheria wa Serikali na ushahidi ukijitosheleza mtuhumiwa hufikishwa mahakamani.

Alisema kuwa Serikali ina mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, ambapo inaelekeza kuchukua hatua kwa chombo cha habari kilichotoa taarifa za uongo, ikiwa ni pamoja na kufuta leseni au kusimamisha leseni kwa muda pale ambapo chombo cha habari kimekiuka masharti ya leseni hiyo. 

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles