23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Wasomi wamjia juu Profesa Ibrahimu

Profesa Ibrahimu Lipumba.
Profesa Ibrahimu Lipumba.

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

JUMUIYA ya Vyuo Vikuu ya Chama cha Wananchi (CUF) tawi la Mlimani (UDSM),  wamemtaka  Profesa Ibrahimu Lipumba kuacha kuchochea mgogoro ndani ya chama hicho.

Wamesema kufanya hivyo anaidhalilisha jamii ya wasomi wenye hadhi kama yake.

Kwa mujibu wa wasomi hao,  hatua yake ya kuendeleza migongano isiyo ya lazima ndani ya chama hicho inaonyesha  ana nia ya dhati ya kutaka kukivuruga.

Jambo hilo litasababisha hadhi yake aliyojijengea miaka mingi kushuka, walisema.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Razack Malilo aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa jumuiya yao inasikitishwa kuona Profesa Lipumba aliyewahi kushika uenyekiti wachama hicho  anakuwa mstari wa mbele kukivuruga na kukigawa chama.

“Sisi Jumuiya ya Vyuo Vikuu tunaokiunga mkono CUF tunamuomba Profesa Lipumba aheshimu uamuzi halali wa chama na kufuata Katiba kwa maslahi ya chama chetu na si yake binafsi kwa sababu  kwa sasa anachokifanya anadhalilisha wasomi wenzake,”alisema Malilo.

Malilo alisema kwa sasa ni wakati wa kukijenga chama na kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019 na uchaguzi Mkuu 2020.

Alisema jumuiya hiyo inaunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho  kuwavua uanachama viongozi wa juu akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya na Naibu Mkurugenzi  wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya, Profesa Lipumba na wengineo.

Malilo alisema hatua hiyo  imeonyesha chama kinaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria.

“Tunaliomba Baraza Kuu na mamlaka nyingine ndani ya chama chetu kuendelea kufanya uamuzi mgumu kwa ajili ya kukijenga chama  inapobidi kwa kuzingatia misingi na taratibu za chama hicho,”alisema Malilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Jidawi Chande alisema Profesa Lipumba hana nia njema na chama hicho.

Alisema Profesa Lipumba  anaonyesha dhahiri ana mpango wa kukivuruga kwa sababu tayari alikwisha kuamua kukaa pembeni  hivyo wanamsihi aendelee hivyo hivyo.

Chande alisema wanafahamu kuna baadhi ya wafuasi wa CUF wanatumika na Chama cha Mapinduzi (CCM) kukivuruga jambo ambalo hawakubaliani nalo.

“Kuna taarifa  zinazagaa eti wafuasi wa CUF upande wa Zanzibar na Bara  wana mpasuko mkubwa jambo ambalo ni uzushi na lina lengo la kukigawa chama,”alisema Malilo.

Alisema jumuiya hiyo inalaani vikali kauli za ubaguzi zinazolenga kuvuruga chama zinazofanywa na Profesa Lipumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles