25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WASIRA AOMBA MATOKEO BUNDA MJINI YAFUTWE

Mbunge wa jimbo la Bunda, Esther Bulaya

 

 

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania imeombwa kufuta matokeo ya uchaguzi Jimbo la Bunda Mjini na kuamuru uchaguzi urudiwe kwa sababu kulikuwa na kasoro nyingi.

Hayo yalidaiwa jana na wapiga kura wanne wanaopinga ushindi wa Mbunge wa jimbo hilo, Esther Bulaya mbele ya jopo la majaji watatu Mbarouk Mbarouk, Rehema Mkuye na Augustino Mwarija.

Wapiga kura hao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila, waliwasilisha maombi hayo kupitia wakili wao Constantine Mutalemwa, wakati rufaa yao ya kupinga matokeo ilipokuwa inasikilizwa.

Mutalemwa aliomba mahakama ifute uamuzi wa kukataa kesi ya uchaguzi uliotolewa na Mahakama Kuu Musoma kwa gharama na kesi hiyo ya uchaguzi ikubaliwe kwamba matokeo ya uchaguzi ya ubunge Bunda Mjini yafutwe na ielekeze uchaguzi wa jimbo hilo urudiwe.

Alidai wanaomba mahakama itoe uamuzi huo kwa sababu kulikuwa na kasoro kubwa, fomu ya mwisho ya matokeo ya ubunge yalionesha idadi ya wapigakura isiyo sahihi ya 164,794 badala ile iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya wapigakura 69,369.

“Kasoro hii kubwa iliathiri  matokeo ya uchaguzi wa jimbo zima kwa kigezo kwamba idadi halisi ya wapigakura iliyotolewa na NEC ndio msingi mzima wa utaratibu wa matokeo kabla ya kutangazwa,” alidai.

Alidai kutokana na mazingira hayo hawakubaliani na maelezo yaliyotolewa na jaji wa mahakama ya chini.

“Jaji wa mahakama ya chini hakuzingatia kifungu cha 115 cha Sheria ya Ushahidi, kwa sababu kulikuwa na malalamiko ya matokeo ya uchaguzi yafutwe kwa sababu Bulaya hakuzingatia matakwa ya sheria ya uchaguzi kwa kushindwa kueleza bajeti yake ya uchaguzi.

“Bulaya alikuwa na jukumu la kuthibitisha kama ametimiza masharti hayo, tofauti na jaji alivyohitimisha kwamba halikuwa jukumu lake bali la walalamikaji.

“Mgombea wa CCM, Steven Wasira, hakualikwa katika mchakato wa kujumlisha kura, hili linaathiri matokeo ya uchaguzi kwa kushindwa kumtambua mgombea wala chama chake,” alidai.

Mutalemwa aliendelea kuwasilisha hoja kwamba  jaji wa mahakama ya chini alikosea kwa kufuta kesi ya uchaguzi kwa sababu, hawezi kufuta matokeo ya uchaguzi huo kutokana na wananchi wa jimbo hilo kuwa masikini na itakuwa mzigo kwa walipa kodi kurudia uchaguzi.

Akijibu hoja hizo wakili wa Bulaya, Tundu Lissu, alikiri kuwepo kwa makosa ya idadi ya wapigakura katika fomu namba 24 B, hata hivyo alidai makosa hayo hayajitoshelezi kutengua matokeo ya uchaguzi.

Alidai mahakama ilielezwa mara nyingi katika kesi mbalimbali kuwa kanuni kuu ya kutengua matokeo ya uchaguzi ni kwamba si kila kosa linalofanywa katika Sheria ya Uchaguzi yanahalalisha matokeo kufutwa.

“Si kila dhambi chini ya sheria ya uchaguzi, mshahara wake mauti ya uchaguzi, kukosea kujaza fomu ya matokeo ya watu waliojiandikisha kupiga kura, kweli ilithibitishwa kulikuwa na makosa hayo lakini sio sababu ya kufutwa matokeo,” alidai.

Lissu alidai waleta maombi walikuwa na wajibu wa kuthibitisha iwapo mjibu rufani wa kwanza (Bulaya), ametimiza masharti ya sheria ya uchaguzi kwa kuwa taarifa zake zipo kwa msajili wa vyama vya siasa nchini ambaye ana taarifa za wagomea wote,  katibu tawala wa wilaya.

Alidai mgombea wa CCM alipewa taarifa ya mahali ambapo kura zitahesabiwa kwa kuwa ilipelekwa kwa ofisi cha chama hicho.

Kutokana na hoja hizo Lissu aliomba rufani itupwe kwa gharama na mteja wake apatiwe gharama zake za mahakama ya chini.

Kwa upande wa mawakili wa serikali Obadia Kamea na Angela Msagala, waliokuwa wanamwakilisha  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika shauri hilo na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, waliunga mkono uamuzi wa jaji wa mahakama ya chini na kuomba rufani hiyo itupiliwe mbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles