27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

Wasichana waliokimbia ukeketaji wapatiwa elimu kujikomboa

 MWANDISHI WETU-ARUSHA

UKEKETAJI ni miongoni mwa vitendo vinavyokiuka haki za binadamu, ambapo huathiri afya kimwili na kiakili kwa mamilioni ya wasichana. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wanawake waliokeketwa wanakabiliwa na hatari kubwa kiafya, ambapo uwezekano wa kupata maambukizi na kuvuja damu nyingi huwa ni mkubwa wakati wa kujifungua.

Pia wana uwezekano mkubwa wa kupata tishio la kupoteza maisha wakati wa kujifungua, pia kukabiliwa na magonjwa ya akili.

Wakati wa hedhi huhisi uchungu hasa wanapokwenda haja ndogo au wakati wa kujamiiana.

Takwimu za nchi 27 ambazo zina matukio ya ukeketaji zinabainisha kuwa ikiwa ukeketaji utatokemezwa katika nchi hizo, zaidi ya asilimia 60 ya gharama za kiafya kwa wanawake wanaokeketwa zingeweza kuokolewa na kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.

Tangu mwaka 1997, hatua zimepigwa katika kutokomeza ukeketaji ngazi za chini za jamii. Nchi 26 barani Afrika na mashariki ya kati zimeweka sheria ya wazi dhidi ya ukeketaji, pamoja na nchi 33 zilizo na wahamiaji kutoka nchi kunakofanyika vitendo vya ukeketaji.

Ukeketaji unatambulika kama ukiukaji wa haki za binadamu na hauna faida zozote za kiafya zaidi unasababisha madhara makubwa kwa wahusika. WHO inashikilia msimamo wake kwamba ukeketaji haupaswi kutekelezwa wakati wowote.

Wadau mbalimbali wapo mstari wa mbele kupinga ukatili, ukeketaji ikiwa ni miongoni, ambapo mkoani Arusha, wasichana zaidi ya 100 kutoka jamii za wafugaji wamekimbia ukeketaji na ukatili wa kijinsia kutoka katika jamii zao, wakiokolewa na shirika lisilo la kiserikali la Health Integrated Multisectoral Development (HIMD) liliopo jijini Arusha. 

Baadhi ya wasichana walikimbia ukeketaji na kusaidiwa na mashirika ya kupinga ukatili wa kijinsia wanasema kuwa wamepatiwa elimu na sasa wamekuwa msaada katika jamii zao.

Riziki Meijo, anasema wasichana waliokimbia ukeketaji wamepatiwa elimu na sasa wamekuwa mfano kwa wasichana wengine ambao walikuwa wakilazimishwa kukeketwa ili wapatiwe wachumba kwa mujibu wa mila na desturi za kabila zao.

Meijo anasema kukimbia ukeketaji kumewapa mwanga wa maisha na kutimiza ndoto zao za kuishi maisha bora. Leonia Shabani, na Anangai Saruni, mabinti waliokimbia ukatili wa kijinsia katika jamii zao na kukimbilia HIMD, wanasema suala la ukeketaji katika jamii zao ni mkubwa hivyo wanaiomba serikali na wadau wa haki za watoto na wanawake kunusuru mabinti wa kike.

Anasema Shirika la Health Integrated Multisectoral Development (HIMD) limemsaidia kumpatia elimu hivyo atakuwa mstari wa mbele kupinga ukeketaji na kutoa taarifa hizo kwa vyombo vya dola.

Mackrine Rumanyika, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa HIMD, na Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto Emayan, wanaokimbia ukeketaji na kuwapatia msaada wa elimu na makazi, anasema baadhi ya jamii bado zinafanya ukeketaji hivyo mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua stahiki kudhibiti ukatili huo.

Rumanyika anasema kuwa shirika hilo linapinga ukatili wa kijinsia, ukeketaji na kutoa elimu ya afya ya uzazi lengo likiwa ni kumkomboa mtoto wa kike.

Anasema wanasaidia wasichana wanaokimbia ukeketaj na wamefanikiwa kuwapatia elimu hadi vyuo vikuu ambapo sasa wamekuwa msaada kwa familia zao na jamii kwa ujumla.

“Baadhi ya jamii za wafugaji katika Mkoa wa Arusha bado wanafanyia ukatili watoto wa kike kwa kuwalazimisha kuwakeketa na sasa wamebadili mbinu wanawafanyia ukeketaji wakiwa wadogo, hapa tunahitaji wadau kushirikiana kuwakomboa,” anasema Rumanyika.

Rumanyika anabainisha kuwa wanaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji katika jamii hizo na kwamba wametengeneza kinyago kinachoeleza na kuonyesha jinsi ukeketaji ulivyo, lengo ni kuhakikisha wanakomesha suala hilo.

Wadau wa haki za binadamu bado wanajukumu la kupinga ukeketaji na ukandamizaji wa mtoto wa kike katika jamii ikiwa ni namna ya kuunga jitihada za Serikali kuwalinda wanawake na watoto wa kike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles