28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Wanyama atabiriwa makubwa

Victor Wanyama
Victor Wanyama

LONDON, ENGLAND

KOCHA wa Klabu ya Tottenham, Mauricio Pochettino, ameweka wazi kuwa kiungo wa timu hiyo, Victor Wanyama, atakuwa na mchango mkubwa katika kipindi hiki cha Ligi Kuu nchini England.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Kenya, amejiunga katika kipindi hiki cha usajili akitokea klabu ya Southampton na tayari amefunga bao moja katika michezo miwili ya mwanzo ya Ligi Kuu nchini humo.

Kutokana na uwezo ambao ameuonesha katika michezo miwili ambayo amecheza, kocha wake, Pochettino, amedai kwamba nyota huyo atafanya makubwa msimu huu.

“Wanyama ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika kikosi cha Tottenham, ameanza kuonesha uwezo wake kwa kufunga bao moja katika michezo miwili ambayo tumecheza na kila mmoja amekubali uwezo wake.

“Bado nitaendelea kumpa nafasi kutokana na kile ambacho amekionesha, amekuwa akifanya vizuri tangu kwenye mazoezi, hivyo ni wakati wake wa kuonesha uwezo,” alisema Pochettino.

Hata hivyo, mchezaji huyo amedai ni furaha kwa upande wake kuanza vizuri katika msimu mpya wa Ligi Kuu na kuisaidia klabu hiyo na amedai kuwa ataendelea kufanya hivyo kwa ajili ya kuisaidia timu pamoja na kulitangaza taifa la Kenya.

“Kufunga bao langu la kwanza katika klabu ambayo nimejiunga hivi karibuni ni jambo kubwa sana na lina maana katika soka la sasa, ninaweza kusema kwamba nimeweka historia kwangu na kupeleka furaha kwa familia yangu.

“Kikosi cha Tottenham kina wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa, hivyo kupata nafasi ya kufunga bao zinatakiwa zifanyike jitihada za hali ya juu, ninashukuru nimeweza kufanya kitu ambacho nilikuwa nakiwaza mara kwa mara, hii ni faida ya klabu pamoja na taifa langu kwa kuwa linazidi kujulikana,” alisema Wanyama.

Wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kuwika katika michuano ya Ligi Kuu nchini England ambao wanatoka Afrika ni pamoja na aliyekuwa nyota wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Steven Pienaar, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Sunderland chini ya kocha wa zamani wa klabu ya Manchester United, David Moyes.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles