30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

HAYA NDIYO MAISHA YA SHUJAA SIMBU

Alphonce Felix Simbu
Alphonce Felix Simbu

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

PENGINE isingekuwa rahisi kufikiria kwamba kuna kijana Mtanzania kutoka Mkoa wa Singida angeweza kuiletea heshima nchi ya Tanzania katika michezo ya Olimpiki mwaka huu, iliyomalizika jijini Rio de Janeiro, Brazil, akimaliza mbio ndefu (marathon) na kushika nafasi ya tano.

Hii ni kwa kuwa Watanzania wameshazoea kuona washiriki wengi wakitoka katika mashindano makubwa, wanarudi mikono mitupu na mkebe wa visingizio, hivyo kukata tamaa kuwafuatilia.

Alphonce Felix Simbu (24), anayetarajia kutua nchini kesho mchana, amewashtua watu ambao walikata tamaa, si tu wanamichezo, bali pia na ambao si wanamichezo, hasa majirani wa mwanariadha huyo, mkazi wa Sakina kwa Iddi, jijini Arusha, nao pia wamejikuta wakipigwa na butwaa baada ya kusikia habari hizo nzuri.

Kutokana na nafasi hiyo aliyoipata Simbu, MTANZANIA lililazimika kufunga safari hadi nyumbani kwake, Sakina kwa Iddi na kufanya mazungumzo na mke wake, Rehema Daud (22).

Rehema, mama wa mtoto mmoja, Abednego, mwenye umri wa miezi nane, yeye na mumewe wanaishi katika nyumba ya kupanga eneo hilo la Sakina, wakiwa ndani ya chumba kimoja walichokigawanya kwa pazia ili kupata sebule na chumba cha kulala.

Akizungumzia maisha yao binafsi na mumewe, Rehema anasema anamshukuru Mungu kumkutanisha na mume mpole na mtulivu ambaye tangu wameoana mpaka sasa wana takribani mwaka mmoja na miezi mitatu.

“Mume wangu tulikutana hapa hapa Arusha eneo hili la Sakina, tulipendana na kuamua kuishi pamoja, Mungu ametujalia mtoto wa miezi nane sasa,” anasema Rehema, huku akiingia chumbani kwake kumchukua mwanawe, aliyekuwa akimvalisha kabla ya ujio wangu nyumbani hapo.

Huku akiwa amembeba mtoto wake, Rehema anaelezea maisha ya kawaida ya mume wake Simbu kuwa hana aina nyingine ya kazi inayomuingizia kipato, zaidi ya kujishughulisha na ukimbiaji (riadha) katika mashindano tofauti anayoalikwa kushiriki.

Anasema katika kushiriki huko ndipo hufanikiwa kupata riziki yake ya siku inayomwezesha kuendesha maisha yake, mkewe na mtoto wao mmoja, ikiwamo kulipia kodi ya chumba kimoja.

“Hana kazi nyingine zaidi ya kukimbia tu, kila siku huwa anafanya mazoezi asubuhi na jioni kwenye maeneo haya ya jirani na nyumbani na hasa maeneo ya milimani.

“Lakini pia sijui maeneo yake mengine ambayo anapenda kufanyia mazoezi,” anasema Rehema, huku akionyesha baadhi ya vikombe alivyowahi kushinda mumewe.

Rehema anamshukuru sana Mungu, kwa kumjalia mumewe ambaye ni mwenyeji wa Kijiji cha Mampandu, mkoani Singida, kushika nafasi hiyo ya tano kwenye mashindano hayo makubwa kabisa duniani.

Mbali na kutegemea kazi ya kufukuza upepo anayoifanya mumewe, Rehema anaweka wazi kwamba amefanikiwa kufungua saluni kwa ajili ya kutengeneza nywele za wanawake, hivyo kumsaidia mumewe katika baadhi ya majukumu ya kifamilia.

“Namshukuru sana Mungu, kwani mume wangu ndiye alinipa mtaji wa kufungua saluni hapo kwa Iddi. Lakini kwa sasa nimelazimika kuifunga ili nipate kumlea vizuri mtoto wangu,” anasema Rehema.

Akiwazungumzia wanariadha wengine nchini, Rehema anawaomba waendelee kufanya mazoezi na kujipa matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika siku zijazo badala ya kukata tamaa mapema.

Wakati Simbu akifanikiwa kuandika historia ya mchezo wa riadha kwa hapa nchini kwa kuingia tano bora, majirani zao wameonyesha kushangazwa zaidi na ushindi huo.

Said Msuya (32), mkazi wa eneo hilo la Kwa Iddi, anasema kwa muda mrefu sasa amekuwa akimuona Simbu akifanya mazoezi ya kukimbia kila siku, lakini hakuwa anamuelewa.

“Unajua nini broo, huyu chalii (kijana) Simbu kwanza sijaamini kama ndiye yeye aliyeonekana huko Brazil akikimbia mbio, hebu angalia hapa nyumbani kwake anaishi maisha ya kawaida kabisa kwenye nyumba ya kupanga.

“Huwezi tegemea, kwanza mimi binafsi sikujua kabisa yuko wapi mpaka juzi kati hivi mtaani kwetu walipoanza kusema yule chalii mwanariadha ameshinda riadha Brazil,” alisema Msuya.

Simbu akiwa nchini Brazil alifanikiwa kukimbia kwa kutumia saa 2:11:15, sekunde 11 nyuma ya mshindi wa nne, Ghirmay Ghebreslassie.

Katika mbio hizo, Mkenya Eliud Kipchoge aliibuka mshindi na kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za marathoni upande wa wanaume.

Feyisa Lilesa wa Ethiopia alimaliza wa pili akiwa nyuma ya Kipchoge kwa sekunde 70 na  kushinda medali ya fedha, huku Mmarekani Galen Rupp akimaliza wa tatu na kujishindia medali ya shaba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles