Wanawake watakiwa kuwa na kiherehere cha maendeleo

0
613

CHRISTINA GAULUHANGA NA BRIGHT MASAKI -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amewataka wanawake kuwa na kiherehere cha maendeleo katika utendaji kazi wao wa kila siku ili mchango wao utambulike.

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa mkutano mkuu wa pili wa viongozi wanawake na utoaji tuzo kwa wanawake walioshiriki mafunzo ya mkakati wa kuwawezesha kiuongozi, inayosimamiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Jenista alisema anakerwa na unyonge wa wanawake.

Alisema hajui kama ni tamaduni au mila ndizo zinawafanya wawe hivyo, hivyo ni vyema wakaachana nazo kwa sababu hazitoi fursa.

Alishangazwa wanawake wakandarasi wanafanya kazi kubwa, lakini hawaonyeshi jitihada kama wanaume.

“Nilishangazwa kuona wakandarasi wanawake wamefanya kazi nyingi kubwa, wanasema wanaume wao ndio wana kiherehere, wanajitokeza zaidi kila tukio tofauti na sisi, jambo hilo silitaki, naomba tuwe na kiherehere cha kuelezea mazuri yetu,” alisema Jenista.

Alisema wakati sasa umefika wanawake kujipima mafanikio yao na kuangalia wanakosea wapi, pia wawe na kiherehere ili waweze kuheshimika ndani ya jamii.

Jenista alisema atahakikisha anasimamia mazingira ya wanawake kwa kuweka sera nzuri za jinsia wakati wa mapitio ya sera ya ajira ya mwaka 2008 ili kuinua ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali.

Alisema inasikitisha kuona takwimu zinaonyesha wanawake wanaofanya vizuri ni asilimia 5, jambo ambalo linahitaji mikakati thabiti kuwainua katika nyanja mbalimbali.

Jenista alisema watahakikisha wamesimamia vema masuala ya jinsia ili mshahara, kazi na ajira ziwe zinafanana.

Aliongeza lazima kuangalia wanawake wanakwama wapi wakati sera, mipango mikakati, sheria zipo na taratibu pia.

Aliwapongeza wanawake 20 ambao mwaka huu wameshiriki mafunzo ya programu ya uongozi  ambayo yatawasaidia kuwainua kiutendaji.

“Naomba ATE iwape nafasi zaidi wanawake, ikibidi fursa hii izidi kuongeza idadi ya wanawake, wasipungue hata 100, nadhani italeta mwamko mkubwa. Naomba pia majina ya wahitimu wa kozi hii tangu waanze yasambazwe katika Ofisi za Serikali na kampuni binafsi,” alisema Jenista.

Alisema zipo faida nyingi za kuwapa wanawake nafasi za uongozi, hasa kwenye bodi kwakuwa wamekuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja tofauti na wanaume ambao wakichanganya tu kazi basi moja wanaisahau.

Mwenyekiti wa ATE, Jayden Nyimbo alisema mafunzo hayo yatasaidia kuinua uwezo zaidi wa wanawake sehemu za kazi. Washiriki walikuwa 20 kutoka kampuni tisa.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni mustakabali wa ajira za wanawake kwa wakati wa sasa na ujao.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Aggrey Mlimuka, alisema programu ya kuwajengea uwezo wanawake ambao wapo katika ngazi za kati sehemu zao za kazi ilizinduliwa mwaka 2016/17.

Alisema hadi sasa wanawake 61 wameiva, 111 wamejiandikisha, watapitishwa katika kozi mwakani.

“Wanawake hawa wamepikwa vizuri, tuna imani wataenda kufanya kazi zao vizuri,” alisema Mlimuka.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la UN Grobal Compact, Simon Shayo, alisema wanataka kuona maendeleo ya wanawake kwa kutoa nafasi za uongozi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here