27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tabaka la ozoni latishia afya viumbe hai

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

KAIMU Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Faraja Ngerageza, amesema kuwa matokeo ya kuharibika kwa tabaka la ozone, ni kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani (UV-B) kufikia uso wa ardhi, hivyo kutishia afya ya viumbe hai katika ikolojia mbalimbali.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa maofisa forodha na wasimamizi wa sheria nchini, kuhusu udhibiti wa kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni.

Ngerageza alisema wanasayansi duniani wamethibitisha kuongezeka kwa magonjwa ya kansa ya ngozi, uharibifu wa macho kama mtoto wa jicho, upungufu wa uwezo wa mwili kujikinga na maradhi na kujikunja kwa ngozi, hivyo mtu kuweza kuonekana mzee kuliko umri wake na kwamba watoto wako katika hatari zaidi ya kupata madhara haya.

“Madhara mengine ni pamoja na kuharibu fiziolojia ya mimea na michakato ya ukuaji wake na kusababisha mabadiliko katika muundo wa spishi, hivyo kusababisha mabadiliko ya bioanuwai katika ikolojia mbalimbali,” alisema Ngerageza.

Alisema katika kuhakikisha kuwa jukumu hili chini ya Sheria ya Mazingira linatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo maofisa forodha, imekuwa ikijitahidi kujenga uwezo wa taasisi mbalimbali katika kusimamia kanuni za udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni za mwaka 2007.

Licha ya hilo, pia alisema hutoa vifaa katika mipaka ya nchi  vinayowezesha kutambua gesi hizi zinapoingizwa nchini.

“Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa na utaratibu wa mara kwa mara kuandaa warsha ya mafuzo kwa maofisa forodha na wasimamizi wa sheria nchini kuhusu udhibiti wa kemikali ambazo zinaingizwa hasa zinazoharibu tabaka la ozoni,” alisema.

Warsha hiyo imehudhuriwa na maofisa forodha wa mipaka yote nchini kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles