Wanaume waelimika kumilikisha wanawake ardhi

0
688

JANETH MUSHIMALINYI

NINA wake wawili, nilikuwa na mashamba manne kila mke nilim­milikisha shamba moja na mawili yaliyobaki tuna umiliki wa pamoja wote watatu.”

Hiyo ni kauli ya Mserengeti Mikembo (49), mkazi wa Kijiji cha Kipenyo, Kata ya Mtimbira, wilayani hapa, Mkoa wa Morogoro, akichangia mada katika kikao cha elimu ya sheria ya matumizi bora ya ardhi kwa wafugaji.

Kikao hicho kiliwashirikisha maafisa mifugo, ugani, kilimo, misitu, mtendaji wa kijiji na kata hiyo na wananchi wa vijiji vya Madibira, Kipenyo, Munga na Mtimbira.

Kikao hicho kilifanywa chini ya mpango wa urasimishaji ardhi (LTSP), unaotekelezwa kwa pamoja na asasi za kiraia zilizo chini ya mwamvuli wa Tanzania Land Alliance (TALA), kupitia mashirika ya wafugaji yakiongozwa na shirika linalojihusisha na utetezi kwa jamii za wafugaji na wawindaji wa asili (Pingo’s Forum).

Mikembo ambaye pia ni mfugaji kutoka kabila la Kisukuma, akichangia mada juu ya umuhumi wa mpango huo, anasema baada ya mradi kuanza kijijini kwao na kupewa elimu, aliona ni vema akaachana na mila na desturi potofu na kuamua kumilikisha wake zake ardhi.

Licha ya kuchekwa na wanaume wenzake walioshiriki kikao hicho ambao wengine bado hawajahamasika kuwamilikisha wake zao ardhi, anasema awali kabla ya elimu iliyotolewa chini ya mradi huo, mbali na kutokuwa na hati miliki za kimila za maeneo yao, hakuwa anaelewa umuhimu wa kummilikisha mwanamke mali ikiwamo ardhi.

“Nina wake wawili, nilikuwa na mashamba manne kila mke nikamilikisha shamba moja na yale mawili tuna umiliki wa pamoja ila wao niliwaachia wakamiliki mashamba yao kila mmoja.

“Ushauri wangu kwa wanaume wenzangu wale wake zetu tunapaswa kutambua ni familia zetu hakuna sababu

 zinazuia kummilikisha kwa maana mali ni yenu kwa pamoja, licha ya kijiji cha jirani kutoridhika na mpango huu sisi tumeupokea vizuri, tumerasimisha maeneo yetu na tumepewa hati miliki za kimila,” anasema.

Mfugaji huyo aliomba wadau mbalimbali kwa kushirikiana na serikali kuendelea kuwatembea na kutoa elimu juu ya urasimishaji makazi kwani mpango huo una manufaa ikiwamo kupanga matumizi bora ya ardhi ambayo yatawezesha jamii kutenga maeneo ikiwamo ya malisho na kuwa na uhakika wa maziwa na nyama bora ambazo zitawawezesha kujiongezea kipato.

Anasema katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo, yeye na wakazi wenzae wamenufaika na elimu na ujuzi juu ya haki ya ardhi, huduma ya msaada wa kisheria na namna ya kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

Naye Hassan Lukila, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mtimbira, anataja umuhimu wa mpango huo kuwa ni pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, ambapo pia anawataka wananchi wenzake kukubali mabadiliko kwani kwa namna yoyote lazima yaathiri upande mmoja kwa ajili ya kunufaisha pande zote.

Anataja faida nyingine ya mradi huo kuwa ni kuwaelimisha juu ya taratibu za umiliki wa ardhi ambayo kwa sasa inaweza kuwasaidia kupata dhamana na kukopeshwa na benki na taasisi nyingine za kifedha.

“Mradi umepokelewa kwa mazingira mawili tofauti, wapo walioukubali matokeo ya kupanga ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali kutenganisha malisho, kilimo na makazi, ambapo kutokana na uvamizi wa maeneo kuna watu wengine wameathirika kwa mpango huu baada ya kubadilishiwa matumizi kwa maeneo waliyokuwa wakiishi,” anasema.

Anaongeza: “Kwa mfano, kuna watu walizoea kuishi na kutumia eneo kwa ajili ya kilimo lakini eneo hilo awali lilitengwa kwa ajili ya malisho, sasa wanapotakiwa kuondoka, hii inaleta kidogo changamoto na inachangia kuonyesha kuwa kuna migogoro kati ya kijiji na kijiji, lakini haipo ila imejificha kwenye utekelezaji wa matumizi bora ya ardhi.

“Ushauri ni kwamba lazima tukubali mabadiliko kwa namna yoyote kwani hakuna mabadiliko yenye asilimia zote kwa faida ya kila mmoja, kuna watakaominywa wengine watakuwa na maslahi ya jumla kwa maana ya wananchi wote,”

Mtendaji wa kata hiyo, Samweli Milangasi, anasema suluhu ya mgogoro huo inaweza kupatikana kupitia wananchi wenyewe kukubaliana na kuwa hata mgogoro huo ukipelekwa kwa viongozi wa juu hautamalizika bila pande hizo kukubaliana.

“Ni muhimu vijiji vyote kuitwa na kukaa kwa pamoja na kushauriana juu ya eneo la malisho ikiwezekana tutenge eneo moja na hati miliki itolewe kwa vijiji vyote viwili.

Na ili tusikwamishe miradi mbalimbali ni vema wananchi mkashiriki mikutano ya vijiji ili tushirikiane kujadiliana masuala yanayotuhusu,”anasema.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kipenyo, Agness Mchele, anasema mpango huo umesaidia kuepusha migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji baada ya kupewa elimu mbalimbali.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Mtimbira, Kikwesha James, anasema wamepata elimu itakayowasaidia katika kuwashauri wakulima na wafugaji pale itakapotokea migogoro baina yao pamoja kuwaongezea uelewa wa kisheria.

“Mpango umetuweka pamoja na jamii na kwa kuwa nao wamepata elimu, itatusaida wakati wa utatuzi wa migogoro endapo itajitokeza, lakini hata wao kwa wao itawarahisihia kutatua migogoro na wanapotaka kumilikishwa ardhi watajua taratibu na wanapopanga mipango ya matumizi bora ya ardhi watajua umuhimu wa sekta ya mifugo katika uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla,” anasema.

Wananchi na watendaji hao pia waliweza kujadiliana kuhusu sheria zinazosimamia ardhi ambayo ni Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Namba 5 ya mwaka 1999, Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, uwapo wa sheria zingine muhimu katika uendeshaji wa mikutano ya vijiji pamoja na Sheria ya Matumizi bora ya Ardhi Namba 6 ya mwaka 2007.

Masuala mengine ni kufahamu taratibu zilizopo za utatuzi wa migogoro ya ardhi ndani ya vijiji na taratibu za utatuzi wa migogoro ya mipaka ya vijiji ambazo zimeanishwa na sheria ya ardhi ya vijiji na vyombo vya usimamizi wa ardhi nchini.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Pingo’s Forum, Emanuel Saringe, anasema katika Mkoa wa Morogoro, mpango huo unatekelezwa na TALA kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Arhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, katika wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero.

Anasema wakati wizara imefanya kazi ya kusaidia vijiji kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na hati za kimila, asasi za kiraia chini ya TALA nazo zimeshiriki kuhakikisha wananchi kupitia makundi mbalimbali wanapata elimu ya kunufaika na ardhi bila migogoro.

Anasema mradi huo wa miaka mitatu unaotarajiwa kuisha mwishoni mwa mwaka huu, wananchi hao wamepata elimu kuhusu ushiriki wao katika mchakato wa uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika utatuzi wa migogoro.

Saringe anafafanua kuwa ushiriki mpana, weledi na ujuzi kwa maeneo ya uelimishaji na uhamasishaji jamii, asasi hizo zilianza kutekeleza shughuli zao baada ya sehemu kubwa ya upimaji na umilikishaji ardhi kuanza, ambapo kumeongeza chachu ya uelewa wa wananchi.

CHANGAMOTO

Anataja baadhi ya zilizoainishwa wakati wa utekelezaji wa mpango huo kuwa ni pamojana na migogoro ya mipaka ya vijiji ikiwamo baina ya Kijiji cha Kipenyo na Madibira, ambao zimefikishwa katika mamlaka mbalimbali ya serikali bila kupatiwa ufumbuzi. “Mgogoro wa uvamizi wa eneo la malisho la kijiji cha Kipenyo na wahamiaji (wakulima) ambao wameanzisha kilimo na makazi na kusababisha kukosekana kwa malisho katika vijiji hivyo, hili limesababisha migogoro baina ya wafugaji na wakulima wa vijiji hivyo.

“Tumebaini pia kumeibuka tatizo la kukosekana kwa mapatio/njia za mifugo kufikia malisho na maji hivyo kulazimisha wafugaji kuswaga mifugo na kupita nayo katikati ya makazi au kwenye mashamba ya watu jambo ambalo limekuwa kichecheo kikubwa cha migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na watumiaji wengine wakiwepo wakulima,” anasema.

Mwezeshaji huyo anaiomba Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, kusaidia vijiji hivyo ili watatue migogoro hasa kutokana na eneo hilo kukosa malisho huku likiwa na wafugaji wengi pamoja na kupunguza vitendo vya watu kuruhusiwa kuishi maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho.

“Baadhi ya viongozi wa vijiji wamekuwa wakiwaelekeza watu kuhamia kwenye maeneo ya malisho hivyo yanakosa ulinzi wa kisheria na ulinzi wa usimamizi, halmashauri zisaidie vijiji kuunda taasisi za kisheria za kusimamia maeneo hayo lakini zitumie sheria ya ardhi kuyalinda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here