31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mdee wenzake waiangukia mahakama isiwafutie dhamana

Kulwa Mzee, Dar es Salaam

Wabunge wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaokabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi, John Heche, Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee na Ester Bulaya leo wameiangukia mahakama wakiomba isiwafutie dhamana.

Washtakiwa hao wamejieleza leo Jumanne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kufikishwa Mahakamani hapo kutoka Kituo cha Polisi Osterbay.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai mahakama ilitoa amri washtakiwa hao wakamatwe kwa kushindwa kufika Mahakamani  Novemba 15 mwaka huu na kwamba Jamhuri wanaomba dhamana ya washtakiwa hao ifutwe.

Wakijieleza kwanini wasifutiwe dhamana kwa nyakati tofauti akianza Msigwa aliomba radhi kwamba haikuwa nia yake kuidharau mahakama, tangu kesi ianze hajawahi kuchelewa, hajawahi kukaidi amri ya mahakama na kwamba anaheshimu kiti cha hakimu.

Amedai alitokea Dodoma alidhani kesi ni saa nne na nusu kama kawaida akiwa na Heche lakini walipofika walikuta kesi imeisha na jitihada za kumuona hakimu kumaliza tatizo hilo zilishindikana.

Kwa upande wake Mdee pia ameomba radhi, ameonyesha jinsi anavyoiheshimu mahakama na kwamba alichelewa kwa kuwa alipitia kupima presha zahanati na alipofika kesi ikawa imeisha na amri imeshatolewa na wadhamini wake waliwahi lakini hawakufanikiwa kumaliza tatizo hilo Novemba 15 kwa kuwa waliambiwa amri ilishatolewa.

Heche amedai aliomba asifutiwe dhamana, anadai anaheshimu mahakama, hajawahi kuidharau, siku ya kesi ilikuwa Dar es Salaam lakini alijua kama kawaida kesi yao inasikilizwa saa nne na nusu hivyo alipofika alikuta imeahirishwa.

Akijitetea Bulaya amedai Novemba 14 alienda msibani Singida kumzika mama yake mdogo lakini aliwapa taarifa wadhamini wake ambao siku ya kesi walikuwepo katika eneo la mahakama.

Baada ya washtakiwa hao kujieleza bado mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja kisha mahakama itoe uamuzi wa kuwafutia dhamana ama la.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na  wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles