23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Wanaorudisha mabilioni kwa DPP wakesha kortini

JANETH MUSHI-ARUSHA

WATUHUMIWA mbalimbali wa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, wanaendelea kupishana mahakamani kukiri makosa yao na kuomba msamaha kupitia nafasi iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP) huku baadhi ya kesi zikisikilizwa hadi usiku.

Jijini Arusha, kesi ya watuhumiwa wa kutorosha madini, juzi ilisikiliza hadi 4:40 usiku ambapo watuhumiwa watatu walitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Arusha, katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili na kuhukumiwa kulipa faini na fidia ya Sh milioni 210 au kifungo cha miaka mitatu kila mmoja.

Aidha mahakama hiyo ilitoa amri ya kutaifishwa madini ya aina nane tofauti yakiwemo Tanzanite, yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 958, yaliyokuwa yakitoroshwa kwenda nchini Kenya na gari aina ya Suzuki Swift lenye namba za usajili T 645 DBY.

Katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi, Rose Ngoka, watuhumiwa ni Josephat Shayo (dereva wa basi), Latifa Mwarengwa na Bakari Kunga ambao ni wafanyabiashara wa madini.

Kesi ilianza kusikilizwa saa 1:11 jioni na kuisha saa 4:40 usiku, ambapo watuhumiwa waliondolewa mahakamani hapo na kupelekwa mahabusu ya Gereza la Kisongo saa 4:50 usiku.

Upande wa Jamhuri katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 59 la mwaka huu, uliwakilishwa na Wakili Mkuu Martenus Marandu na Wakili Mwandamizi Abdallah Chavula huku washitakiwa wakiwakilishwa na Mawakili Arnold Ojare na Said Amri.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ngoka alisema mahakama imewatia hatiani watuhumiwa baada ya kukiri makosa yao wenyewe ambapo mshitakiwa wa kwanza na wa pili (Josephat na Latifa) walikuwa wakikabiliwa na makosa tisa ya kukutwa wakimiliki madini ya aina mbalimbali bila kuwa na hati miliki au leseni ya kujihusisha na shughuli za madini.

Alisema washitakiwa hao walisababisha hasara kwa kukwepa kodi katika mamlaka mbalimbali nchini ikiwemo kodi ya mrahaba.

Huku shitaka la 11 lililowakiwakabili washitakiwa wote ambalo ni kukutwa wakisafirisha madini ya aina mbalimbali yaliyokuwa na uzito wa kilo 31.159 yaliyokuwa na thamani  ya dola za Marekani 416,577.58, (Sh milioni 958) ,wakiwa na hawana vibali wala leseni.

Hakimu Ngoka alisema kwa kuzingatia maombolezo yaliyotolewa na upande wa utetezi na kwa kuwa watuhumiwa wameonekana kusababisha ukwepaji wa kodi, mahakama inaamuru mshitakiwa wa kwanza na wa pili, wanaokabiliwa na makosa tisa ya kukutwa na kumiliki madini bila kuwa na leseni kila mmoja kulipa faini Sh milioni 45 kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu.

“Mshitakiwa wa kwanza na wa pili kila mmoja anatozwa faini ya Sh milioni tano kwa kila kosa au kwenda jela miaka mitatu. Shitaka 11 linalowakabili wote watatu mshitakiwa wa kwanza na wa pili watatakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu kila mmoja,” alisema.

Alisema kwa mshitakiwa wa tatu anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 10 au kwenda jela miaka mitatu, faini wanazopaswa kulipa ndani ya siku saba kuanzia tarehe iliyotoka hukumu hiyo.

“Amri nyingine ya mahakama ni mshitakiwa wa tatu kulipa fidia ya kodi  Sh milioni 100 ya kukwepa kulipa kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya mrabaha, madini yote yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 958 na gari aina ya Suzuki Swift yanataifishwa na kuwa mali za Serikali,”alisema 

Awali kabla ya kuanza kwa shauri hilo, Wakili Marandu aliwasilisha hati mbili kwa niaba ya DPP ikiwemo ya Mahakama hiyo kupewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kueleza mahakama kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka matatu ikiwemo la kula njama ya kutenda kosa na makosa mawili ya utakasaji fedha haramu.

Awali Wakili Marandu aliwasomea watuhumiwa makosa yao na baada ya kusomewa na kukiri, aliomba kuwasomea maelezo ya awali ambapo alidai walijaribu kusafirisha madini toka Tanzania bila vibali wala leseni na  madini hayo yakakamatwa Namanga yakiwa katika basi la abiria aina ya Perfect Ltd Company.

Alidai mshitakiwa wa tatu ambaye anaendesha biashara ya madini ndani na nje ya Tanzania akiwa na wajibu wa kulipa kodi katika mamlaka mbalimbali lakini kwa makusudi alificha pakiti mbalimbali za madini hayo kwenye mfuko wa salfeti uliokuwa umejazwa mchele.

“Siku moja kabla ya kuyasafirisha kwa basi, alipakia madini hayo kwenye gari aina ya Suzuki Swift ambapo alishirikiana na Latifa kupeleka kwa mshitakiwa wa kwanza, tunaomba Mahakama ipokee gari hilo kama kielelezo namba moja,”alisema.

Kufuatia ombi hilo la Wakili Marandu, Hakimu Ngoka alisema mahakama haiwezi kupokea kitu kabla ya kukiona hivyo mahakama  kulazimika kuhamia nje ambapo hakimu huyo alizunguka na kukagua gari hilo kabla ya kurudi ndani kuendelea na kesi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles