30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Wananchi wamwapisha mwenyekiti wa mtaa

Pg 1NA OLIVER OSWALD, DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Kata ya Migombani, Jimbo la Segerea Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, jana walimwapisha Japhet Kembo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa mwenyekiti mpya wa Mtaa wa Migombani, wakidai ndiye mshindi halali wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana.
Sambamba na hilo pia wananchi hao waliwaapisha wajumbe watano wa kamati ya mtaa huo, ambao ni Rose Mhagama, Flora Nyangeta, Angelo Machunda, Paulina Mbalale pamoja na Ramadhan Rashid Seif wote Chadema.

Hatua ya wananchi hao imekuja baada ya mgombea huyo kushindwa kuapishwa kuwa mwenyekiti halali wa mtaa huo katika shughuli za jumla za uapishaji zilizofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Ilala hivi karibuni.

Wakizungumza na MTANZANIA katika eneo la Ofisi ya Katibu Mtendaji wa Mtaa wa Migombani, baadhi ya wananchi kutekeleza azma hiyo walisema wamekuwa wakipata shida kushughulikiwa matatizo yao kutokana na mtaa wao kutokuwa na mwenyekiti kwa muda mrefu.

“Sasa hivi mtu kama una tatizo la kutatuliwa na mwenyekiti unaambiwa hamna huduma kwani hawa watendaji wanadai si jukumu lao, kwa hiyo tumeona ni bora kumwapisha mtu tuliyemchagua wenyewe ili kutuongoza na tunaomba halmashauri iyatambue maamuzi haya vinginevyo vurugu zitatawala,”alisema Gango Boniventure mkazi wa mtaa huo.

Diwani wa kata hiyo, Azuri Mwambagi (CHADEMA), alisema awali shughuli hiyo ilipaswa kufanywa na mkurugenzi wa wilaya hiyo, lakini ilishindikana kutokana na sababu zisizojulikana.

Alisema katika uchaguzi wa kwanza wa serikali za mtaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana mgombea huyo alishinda kwa kura 547 dhidi ya kura 273 za mgombea wa CCM na 205 NCCR Mageuzi, lakini halmashauri ilishindwa kumtangaza kwa shinikizo la mmoja wa viongozi wa juu wa serikali ambao hawataki kuongozwa na wapinzani.

“Wananchi wa kata ya migombani tumeamua kumwapisha rasmi mgombea wetu kwani matokeo ya uchaguzi yapo wazi na hata mkurugenzi alishakiri mbele yetu kuwa Chadema ndo washindi katika jimbo hili lakini kutokana na ubabe wa baadhi ya viongozi ambao wanafahamika wazi mkurugenzi amegoma kumtangaza hadi sasa.

“Kwa hiyo kama kiongozi yeyote anataka vurugu na wananchi basi ajaribu kutengua matokeo haya, kwa kuwa hili jambo limetendeka kihalali kabisa, kwani hata sheria na kanuni za uchaguzi za serikali za mitaa zinaeleza kuwa mshindi anapaswa kuapishwa na mkurugenzi wa manispaa, makamishna wa viapo (wakili au hakimu),”alisema Mwambagi.

Mwenyekiti wa Chadema wa kata hiyo, Gango Kidera, alisema kwa mujibu wa sheria za chama hicho, wanachama wanahaki na wajibu wa kumwapisha kiongozi wao katika eneo walilomchagua.

Kwa upande wake Idd Msawanga, ambaye ni wakili wa kujitegemea aliyemwapisha mwenyekiti huyo, alisema kuwa tendo hilo si kosa kisheria kwani matokeo ya uchaguzi yapo wazi na halmashauri inayatambua.

Alisema endapo halmashauri isingeyatambua matokeo hayo, basi upinzani walipaswa kuweka pingamizi mahakamani baada ya uchaguzi.

Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Segerea, Justin Nyangwe alisema hana taarifa za kuapishwa kwa mwenyekiti huyo pamoja na wajumbe wake kwani halmashauri haikuwapa barua yoyote ya kumtaarifu.

Alisema ofisi yake haiwezi kumpokea na kufanya kazi na mwenyekiti huyo kwani haimtambui na jukumu hilo hufanywa na halmashauri pekee kupitia wanasheria na mawakili wake wanaotambulika.

Siku chache zilizopita mkurugenzi wa Wilaya ya Ilala alisema hakuwaapisha washindi wa Migombani kutokana na kuwepo shinikizo kutoka ngazi ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles