25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Wanafunzi kubaki nyumbani kwa muda usiojulikana

Mwandishi wetu-Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema agizo la kufungwa kwa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu, litaendelea kubaki hadi hapo Serikali itakapotoa tamko jingine.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilisema Rais Dk. John Magufuli pia amesitisha maadhimisho ya sherehe za Muungano zilizokuwa zifanyike Aprili 26 na Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ili kuepuka msongamano na kuendelea kuzuia virusi vya corona visisambae zaidi. 

Taarifa ilisema Majaliwa alisema hayo jana wakati wa kikao cha kamati ya kitaifa ya uratibu wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaotokana na maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Majaliwa alisema hadi jana idadi ya watu waliobainika kuwa na virusi vya corona nchini imefikia 53, ikiwa ni ongezeko la wagonjwa wanne ambao wote wapo Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ya Majaliwa inakuja wakati ambapo dunia hadi kufikia jana kulikuwa na wagonjwa takribani milioni mbili huku watu zaidi ya 120,000 wakiwa wamepoteza maisha.

 “Serikali bado haijatangaza kuhusu kufunguliwa kwa shule, vyuo na shughuli za michezo pamoja na misongamano isiyokuwa ya lazima, hivyo maeneo hayo yataendelea kusalia katika karantini na wanafunzi wote wandelee kubakia majumbani kwao,” ilisema taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ilisema pia Majaliwa alisema Rais Magufuli ameagiza Sh milioni 500 ambazo zilitengwa kwa maadhimisho ya miaka 56 ya Muungano zipelekwe kwenye mfuko wa kupambana na Covid-19 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kadhalika, Majaliwa alisema elimu ya tahadhari ni muhimu ikaendelea kutolewa kwa wananchi ili waweze kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

 “Kama si lazima kutoka, wananchi waendelee kutulia majumbani mwao,” alisema Majaliwa.

Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya waendelee kusimamia utoaji wa elimu ya kujikinga na virusi hivyo, hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao unaongoza kwa wagonjwa wengi ukifuatiwa na Zanzibar.

“Ni muhimu wananchi wake wakapewa tahadhari juu ya namna ya kujikinga,” alisema Majaliwa.

Aliagiza wataalamu wanaosimamia utoaji wa huduma katika maeneo yaliyotengwa kwa watu wenye maambukizi ya Covid-19, wakiwemo madaktari wapewe vifaa vya kujikinga ili kuhakikisha hawapati maambukizi ya ugonjwa huo.

Alisema watu waliokutana na wagonjwa waendelee kufuatiliwa kwa umakini na wahusika wawashirikishe viongozi wote hadi wa ngazi za chini na kwamba athari za kiuchumi zinazojitokeza kufuatia ugonjwa huo ziendelee kuchambuliwa.

Machi 17, 2020 na Machi 18, 2020, Serikali ilitangaza kuzifunga shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu kwa muda wa siku 30 na kwamba wanafunzi wa kidato cha sita waliopaswa kuanza mitihani Mei 4, nao wangepaswa kusubiri wizara ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.

Akitangaza uamuzi huo, Majaliwa alisisitiza kuwa mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii. 

Alizitaka wizara na taasisi zizitishe semina, warsha, makongamano na mikutano yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki toka nchi zenye maambukizi makubwa.

“Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” alisisitiza.

AONYA WAKAZI DAR

Mepama jana, Majaliwa aliwaonya wakazi wa Dar es Salaam na Zanzibar ambako kuna wagonjwa wengi.

Hadi kufikia jana, Dar es Salaam pekee wamegundulika wagonjwa 36, Zanzibar 12, Arusha watatu, Mwanza mmoja na Kagera mmoja, huku watatu wakiwa wamefariki dunia.

Majaliwa alisema hayo alipokuwa akipokea hundi ya mfano ya Sh milioni 500 kutoka Kampuni ya Export Trading Group (ETG) ikiwa ni fedha za kupambana na corona.

Alisema wakazi wa Dar es Salaam na Zanzibar lazima wachukue tahadhari zaidi.

 “Hatua tuliyofikia hivi sasa, maambukizi yameanza kuongezeka hasa kwa Dar es Salaam na Zanzibar. Tunajua kule kuna watu wengi na shughuli zote za kiuchumi zinaanzia pale, lakini hatuna budi kufuata masharti tuliyopewa ili kuzuia ugonjwa huu usisambae.

 “Serikali inatoa msisitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima. 

“Muhimu zaidi sote tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ili atupunguzie makali ya ugonjwa huu,” alisema Majaliwa.

Onyo la Majaliwa limekuja ikiwa siku chache tangu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alizungumza na viongozi wa dini na kusema kuwa hivi karibuni maambukizi ya virusi vya corona yataingia kwenye ngazi ya jamii na hivyo kuwa vigumu kujua mtu ameambukizwa na nani.

Alisema Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) lilikadiria kwamba itakapofika Aprili nchini kutakuwa na wagonjwa 1,000 lakini hadi sasa hatujafika huko.

“Hadi leo bado hatujafika huko, lakini  tunaendelea kuhimiza wananchi kuchukua hatua. Leo tunapoongea nanyi viongozi wa dini tumepata wagonjwa 25.

“Naomba niliseme hapa kwa sababu kama niposema nitakuwa siwatendei haki Watanzania, tumetoka kwenye maambukizi yanayoletwa kutoka nje ya nchi (imported cases), tuko kwenye (local transmission), ugonjwa tumeletewa kutoa nje, hivi sasa takwimu za jana na wiki iliyopita na ya juzi tumeanza kuambukizana wenyewe kwa wenywe.

“Hili viongozi wangu naomba niliweke wazi, it is no longer imported cases, tumeanza local transmission na ndani ya siku chache tutaingia kwenye community transmission, maana yake tutapata mgonjwa hatutajua ameupata wapi ugonjwa, sababu sasa hivi amekuja mtu akamwambukiza ndio maana tunafanya contact tracing (kutafuta watu ambao mgonjwa alikutana nao).

“Sasa tukitoka hapo unampata mtu hujui ameambukizwa na nani na ndani ya siku chache tutaweza kuingia katika hatua hiyo, kwa hiyo lazima niwaambie ukweli viongozi wetu wa dini.

“Nisiwafiche, soon (karibuni) tutaingia kwenye community transmission, hapo sasa ndo tunatakiwa kuendelea kuchukua hatua, tunaweza kuzuia maambukizi  yasiende kwenye jamii, lakini tunatakiwa tuongeze jitihada zaidi. “Kwa hiyo kubwa viongozi wetu wa dini ni kuendelea kuepuka kadiri inavyowezekana mikusanyiko ya watu wengi, na mategemeo yetu tupate ushirikiano wenu katika kuhakikisha ibada zinaendeshwa kwa namna ambayo si hatarishi,” alisema Ummy.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,540FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles