24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI 2,000 KARATU HAWAJUI KUSOMA, KUANDIKA

Mkuu wa wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo

Na JANETH MUSHI-KARATU


WANAFUNZI 2,002 wa darasa la kwanza hadi la tatu wilayani Karatu, hawajui kusoma, kuhesabu wala kuandika.

Kutokana na changamoto hiyo, Mkuu wa wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo amewataka wazazi wilayani hapa kuwaruhusu watoto kushiriki katika shughuli za usomaji katika kambi za usomaji zilizoanishwa katika maeneo yao ili kuongeza idadi ya wanaojua kusoma.

Hayo yamesemwa juzi wilayani hapa na Mkuu huyo wakati wa maadhimisho ya siku ya usomaji duniani, ambayo yaliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision na kufanyika katika kijiji cha Dumbechand, kilichopo Kata ya Baray. Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kati ya wanafunzi 22,015 wa darasa la kwanza hadi la tatu, wanafunzi 20,013 ambao ni sawa na asilimia 92 ndiyo wanajua kusoma,kuhesabu na kuandika.

“Leo ni siku ya usomaji duniani, kambi za usomaji zina faida kubwa, wale wanaohudhuria kila mara huweza kusoma vizuri, wazazi mnaokataza watoto mnataka wakachunge iwe mara ya mwisho, viongozi wa vijiji hamasisheni wazazi na watakaokaidi wachukuliwe hatua,” amesema.

Awali Kaimu Meneja Mradi wa Dream Village, unaotekelezwa na Shirika hilo katika Tarafa ya Eyasi, Richard Kitomari amesema katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kambi hizo, kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba katika eneo la mradi kimeongezeka.

Alisema katika shule zilizopo katika eneo la mradi ufaulu umeongezeka kutoka aailimia 40.1 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 54.7 mwaka jana na kuwa wanafunzi 3,867 na walimu 57 wamenufaika na mradi huo kuanzia mwaka 2014 hadi 2018.

“Moja ya changamoto ni mwitikio hafifu wa baadhi ya wazazi kuwaruhusu watoto kushiriki katika shughuli za usomaji katika kambi zilizoanzishwa na baadhi ya viongozi wa vijiji kutokuwa watekelezaji wa shughuli za uboreshaji wa miundombinu hasa uanzishwaji wa kambi za usomaji za watoto,” alisema.

Mratibu huyo amesema hadi sasa kuna kambi 16 za usomaji katika vijiji vinne, zinazohudumia shule tano na kuongeza kuwa wanaendelea kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kambi hizo za usomaji.

Naye mmoja wa Mwalimu wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mbuganyekundu, Athanasia Soka amesema kutokana na wingi wa wanafunzi darasani unachangia wanafunzi wengi kutokujua kusoma, kuhesabu na kuandika, hivyo kulazimika kuwafundisha kwa kutumia zana mbalimbali ikiwemo michoro.

“Nafundisha darasa lenye wanafunzi 123, kutokana na wingi wa wanafunzi kuna ambao hawawezi kusoma wanasaidiana na kutokana na zana za ufundishaji zilizopo darasani, wanazidi kujifunza kusoma,” amesema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles