29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

WALIOWEKWA ORODHA YA VYETI FEKI KIMAKOSA WASAFISHWE

 

 

Na TOBIAS NSUNGWE,

WATANZANIA wenzetu waliojikuta kwenye orodha ya wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi wamedhalilika sana, wamesononeka sana, wameaibika sana, wameumbuka sana, wamechekwa sana na zaidi ya yote, heshima ya watu hao katika jamii imeporomoka sana.

Serikali imetoa hivi karibuni orodha ya wafanyakazi karibu 10,000 wanaodaiwa kuwa na vyeti vya kughushi vya kidato cha nne au uhalali wa vyeti hivyo kujaa utata. Na pia Serikali ilikwisha toa agizo kwamba, wafanyakazi wote wanaojijua kuwa hawana vyeti halali vya sekondari wajiondoe wenyewe kwenye utumishi wa umma.

 Hivi karibuni Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, alikaririwa akiunga mkono na kuipongeza Serikali kwa kufanya zoezi hilo huku ‘akijilaumu’ kwa nini hakufagia watumishi wenye vyeti feki wakati wa utawala wake. Hata hivyo, Serikali iliwachefua wananchi wengi pale ilipotamka kwamba, zoezi hilo halitawahusu wanasiasa. Wanaona kuna undumilakuwili katika zoezi hili, kwani kuna wanasiasa wengi wanaodaiwa kuwa na vyeti vyenye utata.

Tayari sakata hilo limeleta adha kubwa kwa watu na familia nyingi hapa nchini, huku matangazo ya watu wanaodai kupoteza vyeti vyao vya kidato cha nne yakiendelea kujaza kurasa za magazeti mengi. Hata hivyo, katika orodha iliyotolewa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani Tanzania, imedhihirika kwamba baadhi ya wafanyakazi wameingizwa kimakosa. Hawa ndio yatupasa kuwatetea.

Gwiji la muziki wa Reggae duniani, Robert Nesta Marley, maarufu kama Bob Marley, ameimba nyimbo nyingi za kuhamasiha wanyonge kudai haki zao. Miongoni mwa nyimbo zake ni wimbo uliopewa jina la Vita. Katika wimbo huo kuna sehemu inasema: Hadi hapo mtindo wa kuwapo raia wa daraja la kwanza na raia wa daraja la pili katika nchi moja utakapokoma, kila sehemu kutaendelea kuwa na vita! Vilevile wimbo huo unasema hadi pale dhana ya kubagua watu kutokana na rangi zao itakapokoma, vita itaendelea pande zote za dunia! Alitumia neno vita akimaanisha mapambano ya wanyonge kudai haki zao.

Juzijuzi mwanasheria na Mbunge machachari nchini, Tundu Lissu, amewashangaa wafanyakazi wa Tanzania ambao badala ya kudai haki zao, wao huziomba kwa waajiri wao jeuri, hususan, Serikali. Kwa mujibu wa Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, adui mkubwa wa wafanyakazi nchini ni Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), kwani ndilo limejenga mtindo wa wafanyakazi kuomba badala ya kudai haki zao kwa waajiri.

TUCTA kupitia viongozi wake, ndio waliowataka wafanyakazi walioathirika na zoezi la kuchunguza vyeti feki ‘wawe wavumilivu’ wakati Serikali inaangalia jinsi ya kuwalipa mafao yao. Zoezi hili la vyeti feki limezua hisia tofauti.

Ni kweli katika orodha ile wapo ambao ni kweli waliajiriwa kwa kutumia vyeti vya kidato cha nne vya kughushi. Wanajua wenyewe walivyopenya hadi kufikia kuajiriwa bila kugundulika, huku wakiwa hawana vyeti halali vya elimu ya sekondari. Wale waliokuwa wameghushi kweli au kutumia vyeti vya marehemu ndugu zao basi wamevuna walichopanda. Hili ni fundisho kwa vijana wetu walioko shuleni sasa wasifikie kughushi, kwani watakuja kuumbuka kama wanavyoumbuka mama, baba, kaka na dada zao sasa.

Ukweli ni kwamba, elimu ni mchakato wa kutafuta maarifa na ujuzi ili kupata moja ya nyenzo za kuboresha maisha. Tatizo linaanza pale baadhi ya Watanzania wanapougeuza mchakato wa elimu kuwa mchakato wa kutafuta vyeti, ili kujipatia kazi nzuri au kupanda vyeo kwenye utumishi wa umma. Walioko mashuleni leo wajue kwamba, vyeti vizuri vya shule vinapatikana kwa kusoma kwa bidii. Basi.

Tabia ya kughushi nyaraka ni ugonjwa ulioikumba jamii yetu tangu siku nyingi na kwa kweli hali hiyo ilianza kukithiri miaka ya 90. Baadhi ya watu katika jamii wamekuwa na hulka ya kughushi vyeti vya shule, vyeti vya kuzaliwa, leseni na hata vyeti vya ndoa na vya kifo.

Wakati Serikali ikiwaadhibu watumishi wake waliobainika kughushi vyeti, jamii inalo jukumu kubwa la kubadili mtazamo wa machungu wanayoyapata wenzetu waliojikuta kwenye orodha ya aibu ya vyeti feki, Watanzania sasa tuache tabia ya kutaka kufanikisha mambo yetu yote kwa njia za mkato.

Nasema walioghushi vyeti walifanya makosa na mamlaka zina haki ya kuwachukulia hatua. Hata hivyo, mazingira ya rushwa na ufisadi katika mfumo wa uendeshaji mambo nchini kwetu pengine ndiyo yalishawishi watu wengi kuingia kwenye mkumbo.

Nasema tatizo la watu kufoji vyeti liliachwa limee kwa vile mfumo mzima uliachia mianya kwa hayo kutokea. Kwa hili la vyeti feki, mimi naona ilaumiwe jamii nzima. Kati ya waliojikuta wakifukuzwa kazi kwa kuwa kwenye orodha ya vyeti feki ni wafanyakazi waliokuwa wamebakiza miezi michache sana kustaafu kazi. Ingawa kwenye sheria hakuna kitu kinaitwa ‘ubinadamu’ mtu anapofanya kosa, wale wazee lazima wapewe haki zao zote, kwani ingawa wamekumbwa na ‘shetani’ wa vyeti feki, wengi wao wamelitumikia taifa hili kwa uadilifu mkubwa.

Kosa la Baraza la Mitihani kuwaweka hata wafanyakazi wenye vyeti halali kwenye orodha ya vyeti feki limewadhalilisha watu wasio na hatia. Serikali iliiweka orodha hiyo hadharani na hivyo kuenea kwa haraka kwenye mitandao ya kijamii. Jambo hili limewaletea usumbufu mkubwa hata wale wenye vyeti vyao halali.

Najiuliza, hivi ilikuwa lazima kwa mamlaka kuyaweka majina yale hadharani?  Kwa nini wahusika wasingeandikiwa barua za siri? Hata kama kuna baadhi ya wafanyakazi wameghushi vyeti, bado wana haki ya kuthaminiwa utu wao na mtu hawezi kuhukumiwa hadi ithibitike kwamba kafanya kosa. Iko wapi haki ya mtu aliyewekwa kwenye orodha ya walioghushi vyeti kimakosa? Ni kazi ya Serikali kuwasafisha watu hawa ambao majina yao yamechafuka sana katika jamii.

Menejimenti ya Utumishi wa Umma ifanye yafuatayo: Kwanza itoe tangazo la kuwasafisha wafanyakazi hao na tamko la kuwaomba radhi lililosainiwa na Waziri au Katibu Mkuu Utumishi, lisambazwe kwenye mitandao ya kijamii. Pili, Serikali iwape fidia ya fedha wafanyakazi hao waliodhalilika kwa makosa ya taasisi za umma na kwa hili, Lissu na wanasheria wengine wajitokeze kuwatetea.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles