23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU ATETA NA POLISI MAUAJI KIBITI

*Asema mauaji sasa basi, Wananchi walalamikia kipigo walazimika kulala saa 12 jioni

Na ELIZABETH HOMBO-KIBITI


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza wilayani Kibiti mkoani Pwani na kuteta kwa faragha na askari wa operesheni maalumu ya kuwasaka wauaji.

Alisema  mauaji sasa yametosha na Serikali haitikuwa tayari kuona vitendo hivyo vinaendelea   kama ilivyo nchini Somalia.

Ziara ya ghafla  imetokana na matukio ya mauaji ya mara kwa mara ya raia katika eneo hilo ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.

Akizungumza  wilayani hapa  baada ya kuwatembelea  polisi   katika kambi maalumu ya operesheni ya kusaka wahalifu katika Kata ya Bungu, Mwigulu alisema  Serikali haiwezi kuvumilia mauaji ya mara kwa mara kama yanayotokea Somalia.

Waziri alisema serikali  imejipanga kudhibiti hali hiyo kwa sababu kufuga wauaji na wahalifu kuna gharama.

“Tunaendelea kufuatilia kazi ambazo mnaendelea kufanya, mapambano ambavyo yameendelea, tuendelee kusonga mbele.

“Nikiziangalia takwimu na mwenendo, nazidi kupata maswali na naendelea kuona kuwa kuna kamchezo kanachezwa.

“Mauaji haya waliyoyafanya inatosha. Lazima tuwatie nguvuni, hatuwezi kuruhusu jambo hili likaendelea na kamchezo haka kakaendelea.

“Anayefanya mauaji haya, anayeshirikiana na anayeshangilia hiki kinachofanyika wote tunawaweka katika kundi moja. Kufuga wauaji na wahalifu kuna gharama.

“Kila nikitafakari naona kuna kamchezo kanachezwa, tusipoangalia kamchezo kanakochezwa tutatafuta adui ambaye hakuwapo na tutaacha adui ambaye anahusika.

“Tukamate wote waliohusika. Tusitafute adui kwa kuota au kwa kuwaza,”alisema Mwigulu.

Waziri   aliwataka polisi hao kukaa kimkamkati kuwakamata wauaji hao na waondokane na dhana kwamba wametokomea kusikojulikana bali wawakamate.

“Mwanzoni watu tofauti tofauti kila mmoja alitoa tafsiri yake na wengine wakasema eti ni mkaa, tukawa tunatafuta uhusiano wa mkaa na viongozi wa CCM, yaani ugomvi wa mkaa na CCM wapi na wapi!

 “Haya ni maswali yaliyoacha maswali mengi kuliko majibu; wengine wakasema misimamo mikali ya dini, tukahoji na CCM ni wapi na wapi kwa sababu CCM si dini hata viongozi wake wauawe?

“Likaja la ujambazi, hii nayo na CCM tofauti yake iko wapi hata watafute viongozi wa CCM waliostaafu miaka mitano iliyopita?

“Wengine wakasema tena ni ugaidi, sasa ugaidi na CCM ni wapi na wapi na yule anayeonyesha viongozi wa CCM ni nani na yuko wapi mpaka awaonyeshe waliostaafu,”alisema.

Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba, alisema Serikali inaamini na ndicho inachokisimamia, kwamba hakuna ruhusa ya aina yoyote ya mtu kumuua mwenzake kwa misingi ya kuwa na mtazamo tofauti wa dini, chama, kabila au asili.

“Tutalisimamia kwa nguvu zote. Hatutaruhusu mtu amwue mwenzake kwa sababu ana kabila tofauti, chama tofauti au dini.  Hatutaruhusu chama kitawale hata kitongoji kwa sababu wengine wanaogopa kuwa wa chama kingine kwamba ukiwa chama kile unauawa lakini ukiwa chama hiki unakuwa salama.

 “Hatutakamata mtu kwa ajili ya chama na hatutamwacha mtu kwa ajili ya chama. Hakuna chama kina thamani sawa na maisha ya mtanzania. Kamchezo haka kanakochezwa ni ka muda tu.

“Na naagiza kamati ya ulinzi tuweze kupata maana yake hasa kwa nini wengine wapige kifua mbele ukiwa chama fulani unakuwa salama ukiwa kingine unauawa.

“Tusonge mbele. Hatutawaacha wanaouwa na wanaoshirikiana na wanaoua. Hakuna chama cha siasa ambacho kina thamani sawa na maisha ya binadamu,” alisisitiza.  

Alisema majibu ya maswali wanayojiuliza ni wazi kwamba wahusika hao wako katika maeneo hayo hayo na kwamba hawawezi kutoka sehemu nyingine kwenda kuua.

“Mtu hawezi kutoka sehemu nyingine kuja kumwua mwenyekiti; anajuaje  kama sio watu tunaokutana, anajuaje?

“Hako ndiko kamchezo ninakosema kanaendelea humu. Hawezi akatokomea kusikojulikana, lazima tuliondoe hili,”alisema.  

Waziri alisema jambo hilo  lazima lifike mwisho na si kuwaomba waache bali kuwatia nguvuni pamoja na  wote wanaounga mkono uhalifu huo.

“Tutumie mbinu za macho na za  teknolojia. Wasitufanye wajinga, yaani anauawa mwenyekiti wa kwanza wa pili, tatu mpaka nne wote wa CCM! Nani anayewaonyesha? Na kwa nini CCM?

“Sisi tuna jukumu la kuwalinda wa CCM na wasio CCM, swali nalileta, huyu anayesema huyu wa CCM ndiyo anashambuliwa na hafanyi chochote anaua  tu.

“Nani anayewaambia huyu ni wa CCM na huyu si wa CCM na kuna ushirika gani huyu aliyepo wa CCM ashambuliwe?”alihoji.

Alisema raia lazima watimize wajibu wao kwa kuvipa ushirikiano vyombo vya dola  kuwabaini wahalifu.

“Haiwezekani watu wakafa, wakapotea halafu maisha yakaendelea kama kawaida. Kadiri usipotoa ushirikiano lazima tutakubananisha. Tuhakikishe tunabana mianya ya watu hawa,”alisema Mwigulu.

RC NDILIKO

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndiliko alisema lazima wananchi wawataje wahalifu kwa sababu wanashirikiana nao.

“Wananchi lazima watii maelekezo ya vyombo vya dola kinyume na hapo maisha hayawezi kuendelea kama kawaida,”alisema.

Alisema wapo wananchi ambao wamekuwa wakipeleka taarifa za wahalifu hao na kwamba imesaidia.

“Tunaendelea kuhimiza waendelee kutuletea taarifa, hatutawasaliti na tutaendelea kuwalinda,”alisema Ndikilo.

Aliwataka wananchi ambao wamekuwa wakitishwa waripoti kwenye vyombo vya dola  na   itawasaidia eneo la kuanzia kuwakamata wahalifu.

Aliomba kanda maalumu ambayo inaanzishwa, ianze mara moja na  wananchi wanaweza kuchangia vifaa vya ujenzi na rasilimali nyingine.

WANANCHI WALIA KUPIGWA

Baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA   katika kata hiyo ya Bungu, walisema ikifika saa 12 jioni, polisi wamekuwa wakiwapiga wanapowakuta barabarani.

Roman Munishi ambaye ni mfanyabiashara wa chips, alisema uchumi wao hivi sasa umeshuka na kwamba polisi wamekuwa wakiwapiga kila inapotimia saa 12 jioni.

“Kila ikifika saa 12 hawataki kutuona mitaani au barabarani, ukishajisahau ukafika muda huo unapigwa na wakati mwingine unakimbia mpaka unaacha biashara yako.

“Pia kitendo cha kutulazimika sisi tuingie ndani ya nyumba zetu tulale mapema  kumefanya uchumi wetu ushuke kwa sababu tulikuwa tukifanya biashara hadi saa 3.00 usiku,”alisema Munishi.

Naye Mapande Jamali ambaye ni fundi cherehani, alisema mbali na biashara yao kushuka,  watendaji wa serikali wote wameondoka na hivyo wananchi wakiwa na tatizo wanapata shida.

“Wenyeviti wote wa serikali za mitaa na watendaji wamekimbia, ofisi zimefungwa wamekimbia kwa sababu wanahofia maisha yao. Ukiwa na shida hivi sasa unaenda kituo cha polisi,”alisema Jamali.

  Mwanaharusi Lindeka ambaye ni mfanyabiashara wa supu, aliomba  waruhusiwe wafanye biashara zao mpaka saa 2.00 usiku ili angalau wapate fedha za kuwalisha watoto wao.

“Tuna hali mbaya ya uchumi.  Awali angalau ulikua unawalisha watoto lakini tangu watuambie mwisho ni saa 12 ,unarudi nyumbani huna hata kitu.

“Kwa kweli maisha yamekuwa magumu sana, wangetuachia kama zamani,”alisema mama huyo kwa masikitiko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles