23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waliopunguza mafuta ya kula washtukiwa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Kinondoni umewatoza faini baadhi ya wafanyabiashara baada ya kubaini wanauza mafuta ya kula yaliyopunjwa ujazo.

Hatua hiyo inafuatia ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na wakala huo katika maeneo mbalimbali yanayohifadhi bidhaa za vyakula ambao ulibaini mafuta ya kula yamepunguzwa ujazo wa kati ya milimita 750 hadi lita moja kwenye vifungashio vya lita 10 na lita 20.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Kinondoni, Charles Mavunde, akionyesha mafuta ya kula yaliyo kwenye vifungashio vya lita 10 ambayo yamepunjwa ujazo kati ya milimita 750 hadi lita moja.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo uliofanywa katika maeneo ya Kigogo, Usalama na Mwananyamala, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni, Charles Mavunde, amesema wamewakamata wafanyabiashara wawili ambapo baada ya kukiri kosa walitozwa faini.

“Tumefanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo mbalimbali yanayohifadhi bidhaa za vyakula ili kuona kama zina uzito sahihi.

“Tumebaini mafuta ya kula yamepunjwa ujazo hasa katika vifungashio vya lita 10 na lita 20, unakuta dumu la lita 10 wamepunja kwa wastani wa milimita 750 hadi lita moja,” amesema Mavunde.

Mavunde amesema kulingana na Sheria ya Vipimo sura 340, mtu anayekiri kosa adhabu ni faini kati ya Sh 100,000 hadi Sh milioni 20 na iwapo atarudia kosa adhabu ni faini kati ya Sh 300,000 hadi Sh milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka mitano.

Kaimu Meneja huyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo kwa kuhakikisha bidhaa zina uzito kama ilivyoandikwa kwenye vifungashio huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano pale wanapobaini bidhaa ina uzito pungufu.

“Shughuli zetu ni kumlinda mlaji kupitia uhakiki wa vipimo vinavyotumika katika biashara, tunahakikisha kwamba wananchi wanahudumiwa kwa kutumia vipimo vilivyohakikiwa na ambavyo ni sahihi ili waweze kupata bidhaa kulingana na thamani ya fedha husika. Tutaendelea kufuatilia kuhakikisha bidhaa nyingine zinazozalishwa viwandani zinafungashwa kwa mujibu wa sheria na zinauzwa zikiwa na kiasi kilichoandikwa kwenye vifungashio,” amesema.

Mwanzoni mwa Februari mwaka huu wakala huo pia uliwakamata baadhi ya wafanyabiashara baada ya kukutwa wakiuza sukari iliyopunguzwa uzito wa kati ya kilo moja hadi kilo moja na nusu kwenye vifungashio vya kilo 25 na kilo 50.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles