Waliokiri makosa kurejesha bilioni 107/-

0
1208

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameongeza siku saba kwa watuhumiwa uhujumu uchumi ambao bado barua zao hazijafika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutokana na vikwazo mbalimbali.

Alifikia uamuzi huo jana, muda mfupi baada ya DPP Biswalo Mganga kumwomba kuongeza siku kwa watuhumiwa kuwasilisha barua zao za kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya hivyo ndani ya muda alioutoa awali.

Septemba 22 mwaka huu, Rais Magufuli alishauri mahabusu wa makosa mbalimbali, hasa wale wa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha walizotakatisha wasikilizwe ndani ya siku saba.

Jana, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri huo ambayo alikabidhiwa na DPP Mganga Ikulu Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema ameongeza siku hizo saba ili watuhumiwa zaidi wajitokeze na wale ambao barua zao zilikwama ofisi ya DPP na magerezani pia wajitokeze.

Rais Magufuli alionya kuwa baada ya muda huo hakutakuwa na msamaha mwingine na kwamba kutolewa kwa msamaha huo hakuna maana kuwa makosa ya uhujumu uchumi yamefutwa.

Mbali ya kutoa siku hizo saba baada ya zile saba za awali kuisha, Rais Magufuli alieleza kufurahishwa na mwitikio wa washtakiwa wengi kujitokeza kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali wanazodaiwa kuhujumu.

Vilevile alisisitiza kuwa washtakiwa wote waliofanya hivyo waanze kuachiwa kutoka magerezani walikokuwa wanashikiliwa.

“Kama kweli wapo waliokwamishwa na DPP umeniomba siku tatu, mimi naona nikupe siku saba ili usije ukaniomba tena siku nyingine, nilitoa siku sita kwamba watuhumiwa wote wanaotaka kupata huu masamaha kwa kupitia taratibu za kisheria na wameitikia zaidi ya watu 467.

“Nimetoa hizi siku saba na sitatoa nyingine, lakini niwapongeze hawa 467 na mimi ningeomba ofisi ya DPP mharakishe ili watu waanze kutoka wakajumuike na familia zao.

“Kwa sababu waliingia kwa njia ya mashaka watatoka kwa njia ya mahakama, kwa hiyo muwafikishe kwenye vyombo vya sheria ili waweze kuachiwa isije tena mtakapochambua mkakuta wamebaki 300.

“Na fedha Sh bilioni 107.842 zitaokolewa na nina uhakika hawatarudia makosa yao, lakini nitoe tahadhari baada ya siku hizi saba kuisha wale wote watakaoshikwa kwenye makosa haya ya uhujumu uchumi sheria ichukue mkondo wake,” alisema Rais Magufuli.

Aidha alisema msamaha huo hautawahusu watuhumiwa wenye kesi mpya, ni kwa wale waliokwama tu.

“Watakaoshikwa na kesi za uhujumu uchumi leo, kesho na kuendelea wao waendelee na kesi zao za uhujumu uchumi, maana huu msamaha hauwahusu hata kidogo, kwani kuna wale ambao wana kesi mpya wao wapelekwe tu kwenye kesi,” alisema.

Vilevile aliwatoa hofu watuhumiwa hao kuepukana na dhana ya kuwa msamaha huo ni wa uongo kwa kuwa yeye ameutoa kwa dhati na kwamba hawezi kufanya hivyo kwa lengo la kuwatega.

“Hizi siku saba ni kwa ajili ya wale ambao wamekwama, inawezekana mwingine akawa amejifikiria zaidi katika siku ya leo hadi ya saba akatoa maamuzi yake, ninafahamu wapo wanaodanganywa huu msamaha ni wa uongo.

“Huwa hakuna msamaha wa uongo, huwezi ukatoa msamaha wa majaribio au wa kumtega mtu, msamaha ukishautoa ni msamaha la sivyo wewe uliyetoa utaibeba hiyo dhambi kwa Mungu.

 “Ninafahamu wapo wanaodanganywa na mawakili wao ili waendelee kuwachomoa pesa, wanawaambia ukiomba msamaha maana yake unakuwa umeshajishtaki mwenyewe, sasa hiyo ni shauri yao, waamue wanamsikiliza nani,” alisema Rais Magufuli.

Aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Magereza na Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na ofisi ya DPP katika utekelezaji wa kazi hiyo.

Rais Magufuli alisema fedha zitakazokusanywa kutoka kwa washtakiwa hao, zitalinufaisha taifa kwa kwenda kutumika katika maendeleo ya wananchi, ikiwemo ujenzi wa hospitali na barabara.

Awali wakati akiwasilisha taarifa yake, DPP Mganga alisema watuhumiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi wameandika barua za kuomba kukiri makosa na kurudisha fedha Sh bilioni 107.84.

Alisema kuwa kati ya fedha hizo wapo washtakiwa walio tayari kulipa hivi sasa Sh bilioni 13.60 pamoja na kukabidhi serikalini madini yakiwemo dhahabu ya Tanzanite yenye kilo 35.

Vilevile alisema wapo washtakiwa walio tayari kulipa Sh bilioni 94.24 kwa awamu.

DPP Mganga alisema pamoja na fedha hizo, wapo washtakiwa wengine wawili walioitikia zoezi hilo na kukiri makosa yao mahakamani ambapo mmoja wao alilipa Sh bilioni 1.3 na kukabidhi serikalini gramu 2,123.64 za madini ya vito yenye thamani ya Sh milioni 36.5.

Aidha DPP Mganga alimwomba Rais Magufuli kuongeza siku kwa watuhumiwa kuwasilisha barua zao za kuomba msamaha na kurejesha fedha na mali kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya hivyo kwa kipindi kifupi cha siku saba kutokana na sababu mbalimbali.

 “Mheshimiwa Rais, watu wameitikia ushauri wako na tumeufanyia kazi ushauri wako, kwamba kwa ndani ya siku saba ambazo ziliishia Jumamosi ya Septemba 28, mwaka huu ofisi yangu imepokea barua za washtakiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi walioomba kukiri makosa yao na kurejesha fedha walizowaibia Watanzania.

“Barua hizi zimeendelea kuja Jumamosi na mpaka jana (juzi) niliona zinakuja kwa kuwa zilichelewa kutoka mikoani kuja ofisini,” alisema DPP Mganga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here