27.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

WALIOHAMA CCM ITIKADI ZA VYAMA ZIMEWAYUMBISHA

                               Mwita Waitara

NA MARKUS MPANGALA                 |                       


GUMZO kubwa linaloendelea katika ulingo wa kisiasa nchini ni hamahama ya wanasiasa kutoka chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kujiunga na chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM).

Aina mpya ya kuhama kwa wanasiasa ni mwendelezo wa fitina za kisiasa, lakini kubwa zaidi kumekuwa na shutuma kwamba wananunuliwa kama bidhaa za mnadani.

Wakati hayo yakijiri takribani madiwani 90 wamevihama vyama vya Chadema, CUF na ACT-Wazalendo. Madai makubwa ya wanasiasa wanaohama vyama hivyo ni kukosekana kwa uhuru wa kujieleza ndani ya vyama hivyo, vita vya madaraka hasa ndani ya Chadema hususani nafasi ya uenyekiti inayoongozwa na Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro, pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Duru za kisiasa zinasema kuwa vitendo vya kuhama wanasiasa hao ni miongoni mwa mbinu na fitina za kisiasa zinazofahamika katika vyama vya siasa barani Afrika.

Hata hivyo wanasiasa wanaohama chama kimoja kwenda kingine wameshindwa kuthibitisha itikadi zao halisi, badala yake wameegemea kwenye sababu ambazo zinahojiwa na wengi.

Mathalani tangu mwaka 2017 hadi nusu ya mwaka 2018 Chadema kimepoteza majimbo matano, Miongoni mwa majimbo hayo wabunge watatu wamekihama chama hicho na kujiunga CCM.

Wabunge hao ni Mwita Waitara aliyekuwa Jimbo la Ukonga (Dar es Salaam), Julius Kalanga wa Jimbo la Monduli (Arusha) na Dk. Godwin Mollel wa Jimbo la Siha (Kilimanjaro.

Chadema wamepoteza J imbo la Buyungu ambalo hivi sasa lipo mikononi mwa CCM baada ya mbunge wa jimbo hilo Samson Bilango kufariki dunia, .

Aidha, Chadema wamepoteza mbunge Longido, Onesmo ole Nangole baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kutengua matokeo ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015 na kuamuru urudiwe. Baada ya marudio jimbo hilo limenyakuliwa na CCM.

Msingi wa hoja ya wanasiasa waliohama Chadema au vyama vya upinzani kwenda chama tawala wamedhihirika hawakuwa na itikadi yoyote inayowafungamanisha na chama hicho. Chadema kinaamini katika itikadi ya mlengo wa kati ikiwemo kukuza na kuimarisha uchumi wa soko huria. CCM kinaamini katika itikadi ya ujamaa na kujitegemea.

Katika kuliweka hili sawa ni vema kufahamu kwanza itikadi ni nini. Itikadi ni mkusanyiko wa imani unaotambuliwa na kikundi cha watu fulani. Itikadi ya kisiasa ni upangiliaji unaohusu mawazo ya kimaadili na vipi nchi itaendeshwa. Mfano, itikadi kubwa za kisiasa na kiuchumi ni ujamaa, ukomunisti na ubepari.

WALIOHAMIA CCM WANAKIPENDA?

Wanasiasa waliokihama chama kikuu cha upinzani Chadema kwenda CCM wana historia ya kuandaliwa na kupikwa katika itikadi ya ujamaa. Ingawaje itikadi hiyo inaweza kuruhusu kuwepo kwa itikadi nyingine ya ubepari, lakini pia vyama hivi viwili havina itikadi zinazofanana.

Katika siasa kuna imani fulani ya ‘wamekunywa maji ya bendera’ ambao humaanisha kuwa wanasiasa fulani huamini katika itikadi ya chama fulani hata kama akiwa nje ya chama chenyewe.

Mazingira ya kuondoka kwao CCM na kwenda Chadema ni dhahiri wanasiasa Kalanga, Waitara na Dk. Mollel hawakufuata itikadi ya ubepari inayohubiriwa na Chadema. Kwamba wanasiasa hao hawaamini katika uchumi wa soko huria, badala yake malezi na mafunzo ya itikadi ya ujamaa yamewafanya wawe wepesi kurudi chama chao kilichowalea.

Aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alihama CCM baada ya ugomvi wa kimadaraka ndani ya chama hicho alipokuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kinondoni, baadaye alipelekwa mkoani Tanga na kuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa UVCCM.

Julius Kalanga aliondoka CCM katika kipindi cha vuguvugu la uchaguzi mwaka 2015, akiwa mmoja wa wanasiasa wa karibu wa aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa (Waziri Mkuu Mstaafu)  Kalanga aliwahi kuwa diwani kupitia CCM.

“Uzuri wako wewe umelelewa na kukulia CCM kwa hiyo unajua namna ya kuishi nasi,” ilisemwa na mwanachama mwandamizi wa CCM,” amewahi kusema kada mmoja wa CCM akimsifu Julius Kalanga baada ya kutoa mchango wake bungeni Mei 7, mwaka huu wakati akizungumzia tatizo la maji nchini Tanzania na kuitaka serikali kupeleka mpango wa namna bora ya kupata fedha za kutekeleza miradi ya maji pamoja na kushauri  kuweka tozo la Sh 50 kwenye mafuta ya diseli na petroli ili kusaidia upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maji.

Ina maana CCM hadi sasa imewarudisha vijana wake watatu iliowapika na kuwapa itikadi ya ujamaa, yaani Dk. Mollel, Mwita Waitara na Kalanga, jambo ambalo lingewawia vigumu kudumu katika itikadi ya ubepari ya Chadema.

Dk. Mollel naye aliondoka CCM baada ya kuona hakuna uwezekano wa yeye kupata fursa ya kuwania ubunge. Hivyo uamuzi wake wa kuondoka CCM kwenda Chadema ulitokana na masilahi yake kama mwanasiasa ambaye aliona umuhimu wa kutumia fursa ya uchaguzi ya mwaka 2015. Mollel ni miongoni mwa vijana waliopigwa na CCM.

Mollel ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Siha. Mwaka 2012 alikihama Chama hicho kwa madai kuwa kulikuwa na purukushani za kisiasa na hujuma ndani ya CCM na kujiunga Chadema.

Nanukuu kauli ya Dk. Mollel aliyowahi kuitoa mwaka mmoja kabla ya kurejea CCM ALISEMA; “Siku zote tangu niingie kwenye siasa niliamini kwamba nchi inahitaji mabadiliko, na nilidhani unaweza kufanya mabadiliko ukiwa ndani ya CCM, ukweli hilo haliwezekani. Chachu ya kuhama ilikolezwa pale ilipofika mahali nikaonekana nataka kugombea ubunge ndani ya CCM.

Julius Kalanga

“Huku niliko (Chadema), kuna demokrasia ya vyama sana kwamba unaweza kuwa na mawazo yako binafsi usiingiliwe na Chama au mtu yeyote”.

Dk. Mollel mara baada ya kuondoka Chadema alibainisha kuwa hakuona namna nyingine ya kuendelea kuwa mwanachama wa Chadema, kwa sababu anaamini katika siasa za maendeleo na uongozi kuliko uanaharakati unaofanywa na Chama hicho. Ndiyo kusema hata Dk. Mollel alipofanya uamuzi wa kujiunga Chadema alitakiwa kufahamu jambo hili kuwa ni chama cha namna gani kuliko kutumia hoja hiyo kama kigezo cha kuhama.

Aidha, Dk. Mollel amewahi kusema kuwa ndani ya Chadema kulikuwa na mawazo ya aina moja tu; harakati. Kwamba hakukuwa na hali ya uhuru wa mawazo juu ya masuala mbalimbali, ambapo alidai kushambuliwa kwa maneno makali pale alipounga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli. Ni dhahiri Dk. Mollel hakuwa na itikadi yoyote ya ubepari inayopigiwa chapuo na Chadema.

MASILAHI NI KIPAUMBELE

Kinachowaunganisha wanasiasa hadi kuunda umoja wowote wa kisiasa ni masilahi ya pamoja. Iwapo masilahi hayo yanapokosekana ama wengine kupunjwa,kutengwa au uonevu lazima migogoro itaibuka ndani ya chama au muungano wa kisiasa. Mwita Waitara alijiengua CCM mwaka 2008 kisha kujiunga Chadema katikati ya kampeni za uchaguzi wa ubunge Tarime.Dk. Mollel hakuona mwanga wa fursa ya masilahi yake kisiasa. Kalanga naye hakuwa kwenye masilahi ya pamoja na Chadema, hivyo kupunjwa kwao kukawafanya watimke vyama vyao.

ITIKADI YA KISIASA INAANGUKA?

Kuhama hama kwa wanasiasa bila kujali itikadi za kisiasa kunazua mjadala juu ya umuhimu wa itikadi ya chama cha siasa. kwamba wanasiasa wanahama bila kujali itikadi zao, kati ya vyama wanavyojiunga au kuvihama. Kuhamia CCM maana yake mwanasiasa anaamini katika itikadi yao na vilevile kuhamia Chadema.

Wanasiasa wetu hawaonyeshi kuwa wanajali au kuona umuhimu wa itikadi. Augustine Mrema aliyehama CCM mwaka 1995 hakuonekana kuwa na itikadi nyingine zaidi ya ile aliyolelewa ya CCM. Kwahiyo alipohamia NCCR-Mageuzi hakukuwa na msingi wowote wa kiitikadi zaidi ya kasumba zilizoeleka.

Dk.Jonathan Floyd wa Chuo Kikuu cha Bristol katika kitabu chake cha “Is Political Philosophy Impossible?:Thoughts and Behaviour in Normative Political Theory,” anasema ni vigumu kwa mwanasiasa, chama cha siasa na siasa kukwepuka misingi ya falsafa na itikadi yake kwa sababu kuna kanuni na taratibu zinazowekwa na kufuatwa.

“Ni vizuri kupima pia tabia zao kuliko nini wanachokifikiri. Matendo ya wanasiasa yanazungumza zaidi kuliko sauti zao zinavyosikika kila mara mbele ya wananchi,” ameandika Dk.Jonathan Floyd katika kitabu hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,044FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles