29.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

WALIMU KITANZINI

*Sasa kutofanya kazi bila leseni, muswada waiva

*CWT wajichimbia, Kamati ya Bunge yatoa neno


Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

KIBANO kimewadia kwa walimu nchini kwa sababu  muswada wa kuanzishwa   bodi ya taaluma ya ualimu kama utapitishwa na kuwa sheria, mwalimu hataruhusiwa kufundisha mpaka awe na leseni.

Dalili za kuwadia kwa kibano hicho zimejidhihirisha baada ya muswada huo kuwasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo na Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kujadiliwa wiki hii.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, alikiri kuwa muswada huo ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa  katika ratiba yao.

“Ni kweli tutaujadili katika ratiba zetu lakini siwezi kuzungumza zaidi, uje kwenye kamati utasikia tunavyojadili,” alisema Serukamba.

MUSWADA ULIVYO

Muswada huo uliwasilishwa bungeni Mei 2 mwaka huu na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Ulisomwa kwa mara ya kwanza Juni mwaka huu ambako Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliiagiza Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuanza kuufanyia kazi  ujadiliwe katika mkutano ujao.

Pamoja na mambo mengine, utaanzisha Bodi ya Taaluma ya Ualimu ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia mambo yote ya taalamu ya fani hiyo.

Kama sheria hiyo ikipita, walimu wote wanatakiwa wawe wamejisajili kwa vile litakuwa  ni kosa la jinai kufundisha bila leseni na akifungwa anafutiwa usajili. Leseni hizo zitakuwa zikilipiwa ada kila mwaka.

Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) ni miongoni mwa wadau ambao walipelekewa wito wa kutoa maoni juu ya muswada huo.

Hata hivyo baada ya uchambuzi, mtandao huo ulisema umebaini mambo kadhaa ambayo yanahitaji maboresho ili ukidhi masilahi ya wadau husika.

Kwa mujibu wa mtandao huo, baadhi ya mambo yaliyobainika ni muswada kuweka vigezo vikubwa na visivyo vya lazima  kukidhi matakwa ya mwalimu kusajiliwa na kupewa leseni ya kufundishia.

Mengine ni ada wakati wa usajili, kusajili upya, faini na adhabu zisizo za lazima na muundo wa bodi kutowashirikisha baadhi ya wadau muhimu sekta ya elimu.

CWT

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Lea Ulaya, aliliambia MTANZANIA kuwa bado wanaufanyia kazi muswada huo.

“Naomba unipe muda baada ya kesho nitakuwa na kitu cha kuzungumza,” alisema Ulaya.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema mchakato wa kuwa na bodi ya taaluma ya ualimu ulianzishwa na chama hicho kwa kutunga muswada na kuupeleka serikalini mwaka 2013.

“Tulikutana zaidi ya watu 300… tulikaa na wataalamu wakatoa maoni tukaandika muswada na Profesa Abel Ishumi wa UDSM ndiye alikuwa mtaalamu elekezi.

“Baada ya kuupeleka serikalini ulipokelewa kisha utafiti ulifanyika ambako tulienda kujifunza Nigeria, Afrika Kusini na Kenya na baadaye wadau wakashirikishwa ikakubalika walimu wawe na bodi ya taaluma.

“Ilikuwa utungwe wakati wa awamu ya nne lakini tukiwa Ngurudoto Rais wa wakati ule, Jakaya Kikwete, alisema atashughulikia uundwe kabla hajaondoka lakini bodi ya walimu atamuachia mwenzake,” alisema Oluoch.

Alisema kwa kuwa muswada huo umeshatolewa ni jukumu la wadau kuuchambua na akawashauri walimu kuusoma na kuwasilisha maoni yao CWT au kupitia kwa wabunge wao.

Oluoch alisema muswada huo ni muhimu kwa sababu hadi sasa hakuna chombo chochote kinachoshughulikia taaluma ya ualimu.

Alisema  kwa kiasi kikubwa utazuia walimu wa kigeni katika shule binafsi nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,587FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles