24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Wakurugenzi watakiwa kutenga fedha za kutosha Idara ya Ardhi

MUNIR SHEMWETA, RUFUJI

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameeleza kukerwa na tabia ya wakurugenzi wa halmashauri nchini kuitengea fedha kidogo idara ya ardhi katika halmashauri na hivyo kuifanya idara hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Pwani jana, Dk. Mabula, alisema wakurugenzi wengi katika halmashauri nchini wamekuwa wakiifanya idara ya ardhi kwenye halmashauri hizo kama mtoto yatima.

“Ukienda katika halmashauri nyingi idara ya ardhi imekuwa kama mtoto yatima na ofisi zake haziridhishi kabisa ukilinganisha na zile ofisi za idara nyingine kama vile afya na elimu,” alisema Dk. Mabula.

Kwa mujibu wa Dk. Mabula, halmashauri nyingi alizotembelea bajeti ya idara ya ardhi haizidi shilingi milioni 4 ukiachilia mbali fedha za mapato ya ndani ingawa wakati mwingine hazipatikani zote na kubainisha kuwa tatizo linaloonekana ni wakurugenzi kutofahamu kama idara hiyo ina fedha nyingi na kuweka wazi kuwa iwapo halmashauri zitaamua kuisimamia sekta hiyo kikamilifu zitajikusanyia mapato mengi ukilinganisha na sekta nyingine.

Hata hivyo, Dk. Mabula, alisema katika ukusanyaji mapato ya Serikali, sekta ya ardhi inaweza ikawa sekta ya pili au ya tatu kwa kuingiza mapato mengi ya Serikali ikiwa nyuma ya taasisi zinazoingiza mapato mengi kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Awali Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mashaka Abdallah, alimweleza Dk. Mabula kuwa idara yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufinyu wa bajeti inayotengewa kwa ajili ya kutekeleza kazi za ardhi pamoja na vitendea kazi kama kompyuta, printer, shajara na usafiri.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema hali ya ukosefu wa vitendea kazi inawakatisha tamaa watendaji wa sekta hiyo lakini pia inachangia watendaji hao kutofanya kazi zao vizuri na wakati mwingine kuwalazimu kutumia fedha zao za mfukoni kufanikisha kazi walizopangiwa.

Katika mwendelezo wa ziara yake Mkoa wa Pwani katika halmashauri za wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga pamoja na Kisarawe, Dk. Mabula, alikuta kila halmashauri ikidai kiasi kikubwa cha fedha kwa wamiliki wa viwanja na mashamba tofauti na kiwango ilichowekewa kukusanya kwa mwaka.

Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halamashauri ya Wilaya ya Rufiji, Abdallah, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 halmashauri yake ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 15 na hadi kufikia Desemba 31, 2018 ilishakusanya shilingi milioni 16.7 ikiwa ni sawa na asilimia 111.6.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles