24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

UGAIDI KENYA: Mtoto wa mwanajeshi na mkewe wadaiwa kupanga njama


NAIROBI, KENYA

MIONGONI mwa watu wanaohisiwa kupanga njama za kutekeleza tukio la kigaidi la hivi karibuni nchini Kenya ni mtoto wa askari wa Jeshi la Kenya (KDF) pamoja na mkewe ambaye ana sifa za kutatanisha.

Taarifa za awali zinamtaja Ali Salim Gichunge, au kwa jina maarufu Farouk, ambaye aliaminika kufariki dunia kwenye shambulizi la kigaidi Januari 15 lililoua watu 21 baada ya makomandoo kufanya mashambulizi makali Riverside ili kuokoa wahanga.

Baba yake ni Abdala Salim, Sajenti wa jeshi la Kenya, ambaye jana amefunguliwa jalada la uchunguzi na Ofisi ya Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali ya Kenya, wakati mama yake, Sakina Mariam, alikamatwa huko Kaunti ya Isiolo na kurejeshwa jijini Nairobi kwa madhumuni ya kuhojiwa.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kaunti ya Isiolo, Raphael Wawire, amethibitisha kukamatwa kwa Sakina Mariam na kufunguliwa jadala la uchunguzi, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi juu ya suala hilo. Alisema suala hilo linashughulikiwa na ofisi ya Mwendesha Mashtaka makao makuu jijini Nairobi.

Aliongeza kuwa, Sakina Mariam aliripoti kupotea kwa Gichunge mwaka 2015, wakati akihisiwa kuvuka mpaka kuelekea Somalia.

Polisi wanachunguza ripoti za Gichunge kama amewahi kutembelea Mtaa wa Majengo huko Kaunti ya Nyeri wakati wa likizo ya mwezi desemba mwaka jana akihusishwa na mafunzo ya vijana wanayopata huko Somalia.

Inaaminika kuwa, alikuwa anatumia majina ya Farouk Juma na Idriss akiwa Nyeri. Kuhusishwa kwa Gichunge kwenye shambulizi la kigaidi kumewashtua watu wengi wa kitongoji cha Kulamawe Kwa Franco, ambacho ni jirani na mji aliokulia wa Isiolo.

Wakati hilo likielezwa, bado halishangazi kwa ndugu zake, akiwamo dada wa kambo wa Gichunge, Amina Sharrif, ambaye aliliambia gazeti la Nation kutoka Mombasa kuwa familia hiyo ilimshindwa kijana huyo.

“Nilitembelea nyumbani wakati wa msiba wa ndugu yetu wiki moja iliyopita, na mama yangu aliniuliza kama nimemwona. Nilimjibu tunapaswa kusahau habari zake, kifo kitatuambia yuko wapi,”

Gichunge anafahamika Isiolo kama Ali, kijana aliyesoma shule ya msingi Hekima hadi darasa la sita. Baadaye alihamia kambi ya Isiolo kuendelea na masomo.

Alipata cheti cha elimu ya msingi mwaka 2007 na kupata alama 335 kati ya 500. Dada yake, Amina Shariff anasema Gichunge aliondoka Isiolo mwaka 2015 mara baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Sekondari ya Wavulana ya Thuura, iliyopo huko Meru mwaka 2011. Baada kusoma vipindi vifupi katika shule za wavulana, Kibirichia na Muthambi, alipata alama daraja la tatu.

Inasadikika alihama sekondari ya Kibirichia kwa sababu ya baridi kali katika eneo hilo na alipohama shule nyingine ya Muthambi alisema ni kwa sababu ya kudhalilishwa na wavulana wakubwa.

“Alipata tatizo alipokuwa kidato cha kwanza na kukatisha ndoto yake ya kuwa mchezaji wa rugby, hapo ndipo akahamisha ndoto yake hadi kwenye kompyuta,” anasema Amina.

AJIRA

“Baada ya kumaliza kidato cha sita, Gichunge alisomea kompyuta, baadaye alipata ajira katika hoteli moja hapo hapo Isiolo kama msimamizi wa mkahawa wa Intaneti. Hapo ndipo alipoongeza kiwango cha matumizi yake ya intaneti. Baadaye akatuambia anataka kujiunga na masomo ya dini kwa njia ya mtandao.

“Baada ya miezi michache alinipigia simu na kuniambia anakwenda Meru kufanya usaili wa nafasi yake,” anasema Amina Shariff.

Saa chache baada ya Gichunge kuondoka Isiolo, maofisa wa Ofisi ya Makosa ya jinai walizingira mkahawa wa hoteli aliyokuwa anafanyia kazi kijana huyo wakiituhumu kuhusika na masuala ya ugaidi na kuchukua kompyuta.

KUTOWEKA

Mwanzoni mwa mwaka 2016, Gichunge aliiambia familia yake kuwa amehamia Mombasa kufanya kazi katika kampuni ya ujenzi baada ya kusaidiwa na rafiki yake, lakini mwezi mmoja baadaye, rafiki yake aliitaarifu familia ya Gichunge kuwa amepoteza mawasiliano naye.

Familia ilifanikiwa kuwasiliana na Gichunge, ambaye alimwambia mama yake kuwa amepata udhamini wa masomo ya dini ya Kiislamu katika nchi za Uganda na Tanzania.  

KEMUNTO

Wakati huo huo, msichana aliyekuja kuwa mke wa Gichunge, Violet Kemunto, ni mhitimu wa shahada ya kwanza ya uandishi wa habari na mahusiano ya umma katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST), mwaka 2015.

Rekodi katika taasisi hiyo zinaonyesha Violet amejikita kwenye uofisa habari. Kwa marafiki zake walitambua kuwa ameingia kwenye soko la ajira kutafuta kazi kwenye kampuni kubwa za habari.

Lakini kwake ilikuwa kazi ya muda mfupi tu. Alikuwa na mipango mingine, na mipango hiyo ndiyo ilitimia Jumanne ya Januari 15 kwenye tukio la kigaidi la Kenya. Jeshi la Polisi linaamini kuwa mwanamke huyo alivuka mpaka kuelekea Somalia saa chache kabla ya shambulizi hilo kutekelezwa.

Mashushushu wamechunguza maisha yake na kubaini kuwa ni mfanyabiashara ya ugaidi. Rafiki yake Kemunto anasema binti huyo alikuwa mkimya na rafiki mzuri, ambaye wakati wote akiwa darasani au kokote alikuwa anajitanda nguo mwilini huku kichwani akivalia Hijab ambayo huvaliwa na wanawake wenye imani ya dini ya Kiislamu.

“Hakukuwa na kitu cha kutilia shaka kwake, isipokuwa unaweza kuhisi ni Mkristu kwa jina lake. Mara nyingi alikuwa mkimya sana na rafiki wa kila mtu aliyekuwa karibu yake. Aliongea pale tu zinapokuwa kazi za kwenye makundi ya majadiliano chuoni. Wala hakuwa mnywaji wa pombe au kuvuta sigara,” anasema rafiki yake Masinde, Muliro.

MARAFIKI

Katika Chuo cha MMUST, ushindani mkubwa wa kupata chumba kwenye hosteli umechochea watu kujenga nyumba kandokando ya chuo hicho na kujipatia fedha kutoka kwa wanafunzi. Kemunto alipanga chumba kwenye hosteli binafsi kwa kipindi chote alichokuwa akiishi chuoni. Alifahamika kwa jina la Hadija, ambalo lilifupishwa kwa kuitwa “Didge” kwa wanafunzi wenzake.

Alikuwa na marafiki watatu wa karibu, na wa nne alikuwa mwandani wake ambaye wanafunzi wenzao waliwaita, “Gang of Four”, wakiwafananisha na kundi la wanasiasa machachari wa China, Jiang Qing, Zhang Chunqiao, Yao Wenyuan na Wang Hongwen, waliopambana na utawala wa Mao Zedong.

Mmoja wa marafiki zake wenye mawasiliano na ndugu zake Kemunto, walipopigiwa simu hawakuwa tayari kuzungumza lolote. Baadaye walizima kabisa simu zao.

Vilevile alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi mwenzake wa kiume ambaye alikuwa akisoma naye fani moja na walidumu hadi alipohitimu. Mara baada ya kuhitimu, Kemunto alivunja uhusiano huo.

Walikuwa karibu sana na walipanga kuoana, lakini mambo hayakwenda vizuri kama walivyopanga.

NDOA

Toka hapo, Violet alipata kazi kwenye kampuni ya simu jijini Nairobi. Kisha akapata mwanamume mwingine.

Baadaye alitoweka kwenye jamii. Marafiki hawakumsikia tena hadi alipokuwa anaandaa harusi yake mwaka jana. Majirani zake katika eneo la Guango huko Kiambu ambao walikuwa na uhusiano na Gichunge walisema ni mwanamke mkimya ambaye anapenda kutabasamu, lakini si mwongeaji.

Wakati wote alikuwa anavaa hijab. Akifunika uso wake wote kama wafanyavyo wanawake wa imani ya Kiislamu. Hakuwa anatoka nje bila mumewe, Gichunge. Kwenye akaunti yake ya mtandao wa WhatsApp anajitambulisha kama ‘Mke wa Al-Shabaab.’

SOMALIA

Mkuu wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Magharibi nchini Somalia, Rashid Yakub, amesema wanafanya uchunguzi dhidi ya madai hayo na shughuli nzima za mwanamke huyo, bila kutoa ufafanuzi wa zaidi.

Taarifa za usalama zinasema mwaka 2017 Gichunge alimpigia simu dada yake, Amina Shariff kwa njia inayoficha utambulisho wake kumjulisha kuwa alikuwa mjini Lamu njiani kuelekea nje ya nchi.  

Anasema simu hiyo ndiyo ilivunja uhusiano wake na kaka yake Gichunge, kwa sababu aligundua kuwa anaelekea Somalia. Hakumsikia tena kwa kipindi cha miaka miwili.

“Tulizaliwa katika familia ya Kiislamu na sielewi kwa jinsi gani alijitumbukiza huko. Baba yetu ni askari wa jeshi KDF, hilo linaweza kukueleza maisha yetu ya utotoni. Wazazi hawakushindwa kutulea vizuri, Gichunge amechagua njia yake mwenyewe kuelekea gizani,”

KUINGIA UGAIDI

Dada yake anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 na 2016, Kaunti ya Isiolo ilikuwa na ongezeko la vijana waliojiunga na ugaidi. Vijana wadogo walichukuliwa kujiunga na ugaidi, ikiwamo kundi la Al Shabaab. Mwaka 2016 pekee, vyombo vya dola vinasema takribani vijana 20 kutoka Isiolo walijiunga na Al Shabaab.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles