31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Wakulima walalamikia kushuka thamani ya mazao

yanga-kochaNA RAYMOND MINJA

-MAFINGA

KUSHUKA kwa thamani ya mazao na kukosa soko la uhakika, kumewalazimu wakulima wa mazao ya biashara Mkoa wa Iringa kuziomba taasisi za fedha kuangalia namna ya kuboresha  utoaji wa mikopo ili kumudu kulipa madeni.

Wamesema hatua hiyo itawasaidia kuondokana na adha ya kutaifishwa kwa vitu vyao ndani kwa kushindwa kurejesha mikopo.

Kauli hiyo waliitoa wilayani Mufindi walipokuwa wakizungumza katika mkutano wa saba wa mwaka wa wanahisa wa Benki ya Wananchi Mufindi (Mucoba), ambapo mmoja wa wanahisa hao,  Monika Ngelime, alisema wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya urejeshaji wa mikopo kutokana na kushuka kwa thamani ya mazao.

“Hebu tazama kwa sasa jinsi nyanya zilivyokosa soko, watu wanapata wendawazimu huko mashambani kwani hawana sehemu ya kupeleka nyanya zao, yaani kuna sehemu sasa imefika mahali tenga linauzwa hadi Shilingi 5,000 na hapo unakuta mtu amekopa benki kwa ajili ya kuandaa shamba ikiwemo na ununuzi wa pembejeo.

“Kwa hali hii ndipo mtu hulazimika kukimbia familia kwa hofu ya kukamatwa, tunaomba sana uangaliwe mfumo wa mikopo hasa kwetu wakulima ili tusiweze kuaibika kwa vyombo vyetu kutupwa nje,” alisema Ngelime.

Kwa upande wake Albert Muyinga, alisema changamoto ya masoko ya mazao kwa wakulima imekuwa kama ni janga kwa taifa kwani mara nyingi wakulima wamekuwa wakizalisha mazao mengi tofauti na mahitaji ya soko.

Alisema licha ya taasisi za fedha kuongeza nguvu katika kutafuta masoko, pia ni jukumu la Serikali kutafuta masoko ya uhakika kwa wananchi wake ili kuwa na uhakika wa ununuzi wa mazao yao pindi wanapoyavuna.

Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Benki ya Mucoba, Mkoa wa Iringa, Benny Mahenge, aliwataka wakulima wanaochukua mikopo kwa ajili ya kilimo  kuwa na tabia ya kulima mazao mchanganyiko ili zao moja linaposhuka bei jingine liweze kumsaidia  kulipa deni.

Alisema wakulima hupata hasara wanapolima zao moja kwa kufuata mkumbo badala ya kulima mazao yanayoendana na soko la wakati husika.

“Lakini bahati nzuri sisi benki yetu tunajua nini maana ya hasara na mkulima anapopata hasara hatuwezi kumkaba koo na kuanza kunyang’anya vitu vyake vya ndani.

“Lazima tumpe muda kidogo kwa kuwa msimu huu kapata hasara, basi tunampa msimu mwingine alime zao jingine ili aweze kulipa mkopo wetu kwa kuwa lengo letu si  kumkomoa mkulima ila ni kumkomboa,” alisema Mahenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles