23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Wakulima Buchosa walia na mfumo wa mbolea za ruzuku, halmashauri yajipanga

Na Clara Matimo, Buchosa

BAADHI ya wakulima wa kata za Nyakalilo, Kazunzu na Iligamba katika halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza wamelalamikia mfumo wa ununuzi mbolea ya ruzuku na huduma ya ugavi ambao hawaridhishwi nao huku idara ya kilimo ikijipanga kutatua changamoto zilizopo ili kuendeleza sekta hiyo.

Meneja miradi wa Shirika la TAHEA Mussa Masongo (aliyesimama) akizungumza kwenye kikao hicho.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na wakulima hao wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utafiti juu ya huduma za ugani na ruzuku ya mbolea halmashauri ya Buchosa kupitia mradi wa ‘Tufuatilie kwa pamoja rasilimali ya umma kwenye halmashauri hiyo katika kata za Iligamba, Kazunzu na Nyakalili ili kutoa mwelekeo wa wananchi wanavyoshiriki kusimamia maendeleo yao kupitia miradi inayotekelezwa na Serikali.

Baadhi ya malalamiko yaliyotajwa ni pamoja na uchache wa mawakala ambao wanapatikana mbali na wakulima, baadhi ya mawakala kuwa wadanganyifu kwani wakulima walikuwa wanatumiwa jumbe za kupokea mbolea wakati hawajafanya malipo wala kupata bidhaa hiyo na mbolea hiyo kufika muda tofauti na maandalizi ya mashamba.

Baadhi ya washiriki wa kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya utafiti juu ya huduma za ugani na ruzuku ya mbolea katika halmashauri ya Buchosa kupitia mradi wa Tufuatilie kwa pamoja rasilimali ya umma unaosimamiwa na Shirika lisilo la serikali TAHEA.

Mjumbe wa kamati hiyo, Aisha Salim alisema wakulima wanapaswa kupunguziwa gharama ya mbolea hiyo kutoka Sh 70,000 kwa mfuko mmoja hadi Sh 50,000 na bidhaa hiyo ipatikane kwenye maeneo ambayo ni rahisi wao kuipata huku akiwashauri wakulima kuwafuata wataalam na kusisitiza kuwa mradi huo umeleta chachu na kuwafumbua macho wakulima.

“Mbolea inachelewa kuwafikia wakulima kwa sababu msimu wa kilimo maandalizi yanaanza Juni lakini mbolea imekuja Agosti na upatikanaji wake ni mchakato mrefu tunaomba iwe inakuja kwa wakati ikidhi mahitaj. Mradi umenisaidia kuongeza ufahamu wa hatua za uandaaji wa shamba kisasa na watu gani wa kuwaona,” alisema.

Naye, Boniphace Maseswa ambaye ni mkulima na diwani kata ya Kazunzu alisema “Mbolea ya ruzuku ni mwarobaini lakini upatikanaji wake ni mdogo tunaomba wapatikane mawakala ngazi ya kata kurahisisha upatikanaji wake na wataalam wa kilimo waambatane na wakulima kuwafundisha kilimo cha kisaa na mbinu zake, mradi huu umenijengaea uelewa mkubwa wa kilimo cha kisasa na chenye tija,”

Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Buchosa, Grace Machunda alisema wataendelea kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi washiriki, wajitokeze, wafuatilie, kusimamia na kutoa changamoto kwenye mikutano ya hadhara na vikao vya kujadili maendeleo kwani kwa sasa kuna mwitikio mdogo.

Naye, Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, Obwago Sospeter alisema mpango wa mbolea ya ruzuku umewapa fursa wakulima wengi kununua na kufanya kilimo cha tija na kuongeza uzalishaji kutoka gunia 10 kwa hekari moja hadi gunia 15 mpaka 17 huku wananchi wakiongeza kipato na usalama wa chakula lakini uwepo wa kituo kimoja cha kununulia mbolea hiyo kumeleta usumbufu wakulima wengi kushindwa kuipata.

“Tumeomba serikali awamu inayokuja kuwepo uwezo wa kutafuta mawakala ngazi ya kata na serikali iongeze fedha kusafirisha kwenda kwa mawakala wa kata, pia tunashukuru mashirika yameongeza uelewa kwa wakulima kuhusu kanuni za kilimo bora, masoko, kuwaunganisha na wanunuzi na uwezo wa kujitambua,” alisema Sospeter.

Akizungumzia changamoto hizo, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi halmashauri ya Buchosa, Nestory Mjojo alisema wameanza mchakato wa kuitafutia ufumbuzi ambapo wameshakubaliana na makampuni matatu kuingia makubaliano na mawakala wa Buchosa hivyo kuanzia msimu ujao tatizo hilo halitokuwepo, huku akiwataka wakulima kuzitumia mbolea hizo ipasavyo ili kuongeza uzalishaji.

“Changamoto ilikuwa namna ya kupata mawakala kwa wakati kwa msimu huu tutalifanyia kazi, tunashukuru kamati ya ufuatiliaji imetusaidia kuibua changamoto hii mradi ukienda kwa kasi hii utawasaidia wakulima kujua bajeti zinavyoandaliwa, wajibu wao katika kufuatilia na kujua mipango ya maendeleo,”

“Msimu huu tulilenga kuwafikia wakulima wa mahindi 15,000 lakini mpaka sasa tumewafikia wakulima 6,000 kwahiyo asilimia 70 wamenufaika na mfumo huu wa mbolea ya ruzuku na tani 98 za mbolea hii zimeuzwa ndani ya halmashauri yetu na imetusaidia tumevuna kwa wingi,” alisema Mjojo.

Akizungumzia mradi huo, Afisa mradi wa Ufuatiliaji kwa pamoja rasilimali za umma (SAM), Bundala Ramadhan alisema lengo la mradi ni kuwaelimisha wananchi waelewe wajibu wao katika kushiriki kwenye sekta ya kilimo na kushirikiana na serikali kuiendeleza sekta hiyo kwani wengi hawajui wajibu wao na hawatambui njia sahihi za kuendeleza kilimo.

“Pia maofisa kilimo na ugani wanapewa nafasi finyu kwenye mikutano ya wananchi nashauri kuwa endapo nguvu ya wananchi itafanyiwa kazi na kila mmoja kujua wajibu wake malengo yatafikiwa kwani maoni hayo yamechukuliwa na halmashauri ii kuona jinsi ya kuyafanyia kazi,” alisema Ramadhan.

Kwa upande wake, Meneja Miradi wa taasisi ya Tanzania Home Economics Organization (TAHEA) Mwanza inayosimamia mradi huo, Mussa Masongo, alisema kuna haja ya miradi kupangwa kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa ili inapoletwa iwe ni ya wananchi wenyewe na iwe rahisi kufanya ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji wake kwani kupitia utafiti wao, sehemu kubwa ya wananchi walikuwa hawashirikishwi kwenye maamuzi mengi ya miradi inayowahusu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles