31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

WAKALA WA USAJILI ZANZIBAR YAFANIKIWA KUHAMASISHA MATUMIZI YA KITAMBULISHO CHA MKAAZI

 

 

|Mwandishi Wetu, Zanzibar



Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar, imefanikiwa kuwahamasisha wananchi na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali kutumia vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Hatua hiyo imetajwa kuchangia kulinda usalama wa nchi na pia kuwatambua Wanzibari wenye makaazi ya kudumu visiwani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii, Dk. Hussein Khamis Shaaban, amesema hayo leo Jumatatu Agosti 20, visiwani humo.

Pamoja na mambo mengine, amesema Wakala pia umefanikiwa kufanya mabadiliko ya kiutendaji kwa watumishi wa wakala kwa lengo la kuleta ufanisi na matokeo chanya ikiwamo kuanzisha mchakato wa kutumia mifumo mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma za kijamii na kudhibiti upotevu wa maduhuli ya Serikali.

“Licha ya mfanikio hayo, Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo uchakavu wa miundombinu na vitendea kazi, kutokuwapo kwa mifumo inayosomana katika vituo vyote vya wakala.

“Changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa ofisi kwenye baadhi ya wilaya na kuwepo kwa vyeti feki vya kuzaliwa na baadhi ya vyeti hivyo vinatoka nje ya Zanzibar ambapo hali hiyo imesababisha baadhi ya vyeti hivyo kushindwa kuthibitishwa uhalali wake na utitiri wa maombi ya vyeti hivyo,” amesema.

Aidha, Dk. Shaaban amesema mfumo uliopo ulishindwa kuwatambua baadhi ya wananchi wageni waliojifanya kuwa ni Wazanzibari wakaazi hali inayosababishwa na kutokuwapo na umiliki wa mifumo na kutokuwapo kwa mifumo ya teknolojia inayowaunganisha na wadau wengine ili kubadilishana taarifa kwa haraka.

Hata hiyo, amesema kutokuwepo na mfumo mzuri wa ukusanyaji wa taarifa za awali na uhakiki wa taarifa hizo kutoka katika ngazi ya Shehia ulisababisha baadhi ya raia wa kigeni kufanikiwa kupata vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi.

“Wakala pia unatarajia kuimarisha mfumo wa Usajili wa Matukio ya Kijamii na muunganiko wa mifumo ya usajili wa vizazi na vifo na mifumo ya vitambulisho vya mzanzibari mkaazi ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kuhifadhi taarifa na kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kijamii.

“Kupitia mfumo huo, Wakala inatarajia kutoa kitambulisho kipya cha Mzanzibari Mkaazi cha kielektroniki (e-ID Card) na vyeti vya kuzaliwa vipya, lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha utoaji huduma za kijamii kwa Wazanzibari na wageni wakaazi wanaoingia na kuishi Zanzibar kwa madhumuni mbalimbali,” amesema Dk. Shaaban.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles