24.1 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

WAJAWAZITO WAGOMA KUJIFUNGULIA HOSPITALINI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amemwomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kuangalia upya namna ya kuwapanga wauguzi wenye umri mdogo kutokana na wajawazito kugoma kujifungulia katika vituo vya afya.

Ndugai aliyasema hayo juzi katika uzinduzi wa zoezi la kusambaza vitanda, mashuka, magodoro kwa halmashauri nchini uliofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa.

Spika Ndugai alisema Halmashauri ya Kongwa changamoto kubwa ni kinamama kugoma kujifungulia katika vituo vya afya ambapo katika uchunguzi wake aligundua sababu ni umri mdogo wa baadhi ya wauguzi.

“Nilifanya utafiti wangu wa chini kwa chini kwanini kinamama hawataki kujifungulia katika vituo vya afya, moja ya sababu kubwa niliyogundua ni wauguzi wanaopangwa katika maeneo ya vijijini kuwa na umri mdogo, hivyo kinamama kuona aibu kuzalishwa na wauguzi hao na kuamua kujifungulia nyumbani.

“Ninachokuomba hawa wenye uzoefu ambao wapo mjini na umri wao umesogea basi tuwatangulize vijijini ili hawa wenye umri mdogo tuwapange hapa mjini ili wazoee pamoja na kupata uzoefu,” alisema.

Spika Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa (CCM), alisema ramani zinazochorwa na watu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya zimekuwa kubwa, hivyo kugharimu fedha nyingi wakati wa ujenzi.

Kwa upande wake Waziri huyo alisema Serikali imegawa jumla ya vitanda vya kawaida 3680, vitanda vya kujifungulia 920, magodoro 406 na mashuka 902 ambapo vyote kwa pamoja vina thamani ya Sh bilioni 2.9.

“Pamoja na mambo mengine, Serikali itasimamia kuanzishwa kwa mfuko wa dawa ili kuwarahisishia wananchi waweze kupata huduma hiyo kirahisi,” alisema.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi, alisema halmashauri hiyo imekuwa ikikakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi katika sekta ya afya ambapo waliopo ni 391 wakati mahitaji ni 1228.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,644FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles