24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Waitara akutana na sekeseke la wananchi

 PETER FABIAN– MWANZA

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara, amenusurika kipigo kutoka kwa wananchi wa Mtaa wa Mahina Kati, Kata ya Mahina Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, wakipinga hatua yake ya kufanya mkutano wa hadhara ambao walidai ulilenga kuibua upya kero ya mgogoro wa ardhi, wakati suala hilo liko mahakamani.

Katika eneo lanye mgogoro, Halmashauri ya Nyamagana ilikuwa kampuni ya Nyamwaga inayomiliki kituo cha Michezo Alliance, imelipora kwa wananchi huku wao wakisema wamelinunua kihalali kwa wananchi hao ili kujenga hospitali ya kisasa itakayotoa huduma kwa wananchi hao na wamaeneo ya jirani.

Waitara alipotafutwa baada ya kuondoka eneo la tukio, alisema hana cha kuzungumzia bali atafutwe Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Dk Phillis Nyimbi ama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela. 

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk.Nyimbi alipotafutwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao.

“Nipo kwenye kikao siwezi kusema chochote naomba tu uniache,”alisema Nyimbi.

Alipotafutwa Mongela alisema taarifa aliyokuwa nayo awali ilikuwa ni kwamba Waitara ameomba kwenda kutembelea Zahanati ya Mtaa wa Mahina Kata ya Mahina kukagua ujenzi wa chumba (wodi) wanawake uliokamilika.

“Najua alikuwa anaenda kutembelea Zahanati lakini hayo ya vurugu sijapata taarifa zake kwa kuwa sikuwepo Mwanza, nilikwenda kuhudhulia mazishi ya baba mzazi wa Waziri wa Madini, Dotto Biteko, yaliyofanyika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita hivyo zaidi sijui kama kulitokea shida kwa Waitara alipokwenda Mahina,”alisema.

Diwani wa Kata ya Mahina, James Bwire ambaye ni Meya wa Jiji la Mwanza alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema hakuwa na taarifa za ujio wa Waitara kufanya mkutano wa hadhara katika kata yake.

Alisema taarifa za Waitara kunusurika kupigwa na wananchi wa Mtaa wa Mahina alizipata kutoka kwa Mtendaji wa Kata hiyo Mafuru.

“Nimesikitika na kutokea kwa vurugu hizo lakini pia nimlaumu Mkurugenzi wa Jiji kwa kumpangia Naibu Waziri ziara kwenye kata yangu na kutonishirikisha hata kama alikuwa na nia njema ya kutembelea miradi ya maendeleo na kukagua ni vyema wakatushirikisha madiwani ili kuepusha yaliyotokea,”alisema Meya.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomon Kibamba alipotafutwa, simu yake haikupatikana na alivyofuata ofisini kwake hakupatikana.

HALI ILIVYOKUWA

Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Mahina, Felician Blakali, Alisema Waitara alifika eneo hilo saa 4:30 asubuhi na kupokelewa na Mtendaji wa Kata hiyo Ally Masatu kisha kumuomba kutembelea chumba cha kulazwa wagonjwa wanawake katika zahanati ya mtaa huo.

Blakali alisema baada ya kumaliza kutembelea Chumba hicho akamwambia mtendaji awaambie wagonjwa na wananchi wasogee kwenye eneo la kivuli ili wafanye mkutano wa hadhara.

Baada ya muda Waitara alisema kuna kero ya mgogoro wa ardhi katika eneo hilo hivyo alitaka kuwasikiliza akisema anayo barua ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mery Tesha, aliyeamuru kuvunjwa kwa majengo jirani na zahanati.

Blakali alisema Waitara alisoma barua hiyo na baada ya kuisoma ndipo wananchi wakaanza kumzomea huku wengine wakidai amefika hapo kumchafua Meya Bwire kutokana na mambo ya kisiasa ya wilayania Tarime.

“Ilibidi mtendaji kwa kushirikiana na Vijana wa UVCCM aliokuja nao toka Tarime wamuondoe ili kumuepusha na kipigo na kumuingiza kwenye gari,”alisema.

 Akizungumzia eneo hilo Blakali alisema eneo hilo siyo mali ya umma kama awali ilivyodaiwa na Mkurugenzi wa Jiji, Kiomon Kibamba. “Mkurugenzi Kibamba ndiyo alianzishaga hili suala la Bwire akidai alipora eneo la umma na kuwa halmashauri ilikuwa imelipa fidia kutoka kwa wamiliki wa kienyeji (wananchi) jambo ambalo lilikuwa ni uongo na kutaka kumpunguza ukali Bwire juu ya msimamo wake wa kusimamia haki na kutoyumba katika kusimamia fedha na mapato ya halmashauri ya Jiji,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles