30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Ada mpya marufuku

 RAMADHAN HASSAN DODOMA Na AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM

IKIWA zimebaki siku mbili kabla ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini na kidato cha sita kurudi darasani, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amepiga marufuku kwa vyuo na shule kutoza ada mara mbili kwa wale ambao walikuwa wamemaliza karo ya muhula.

Pamoja na hali hiyo waziri huyo amepiga marufuku michango yote isiyo kwenye utaratibu ikiwa ni pamoja na kuagiza wanafunzi waende na malimao na tangawizi akisema corona isitumike kama fursa ya kujipatia fedha.

Mei 21, Rais Dk. John Magufuli, alitangaza kufungua vyuo vyote nchini na kidato cha sita Juni mosi, mwaka huu ikiwa ni baada ya kupungua kwa maambukizi ya corona.

Itakumbukwa kuwa Machi 17, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule, vyuo, kusitisha warsha mbalimbali pamoja na michezo ikiwa ni siku chache baada ya corona kuthibishwa kuwa imeingia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Profesa Ndalichako, alitaka watu aache kutumia corona kama kitega uchumi na kuonya wale ambao wanaanza kuagiza wanafunzi kutoa michango ya ziada.

“Watu wanaanza kuagiza hela za ziada, za kazi gani? wanafunzi walikuwa wameshalipa ada kabla ya kufunga shule, walienda nyumbani kwasababu kulikuwa kuna changamoto ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (homa kali ya pamafu).

“Sasa baada ya kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali hali ya maambukizi imepungua, Serikali imeona kwamba inaweza ikafungua shule na taasisi (wanafunzi) wanakwenda kuendelea pale walipoachia kwa fedha zao zilezile walizolipa, hakuna malipo ya ziada.

“Kwa hiyo nitumie nafasi hii kukemea shule ambazo zinataka kutumia corona kama kitega uchumi, hapa hakuna kitega uchumi. Kama taifa tumeunga pamoja, tumeweka na maombi Mungu wetu ametusikia sasa tusianze kuumizana kwasababu ambazo hazina msingi wowote.

“Wizara itafuatilia shule ambazo zinataka kutumia corona kama kitega uchumi, kuweka michango ambayo haina uhalali wowote, wizara itachukua hatua ikiwamo hata kuzifutia shule usajili kwasababu tumekuwa tunawaambia kila mara watu wanaoendesha shule wanatoa mafunzo kwa Watanzania, wasiwe na ile roho ya kukomoana.

“Sasa imekuja changamoto ya corona watu wanaona ni fursa, hili jambo halikubaliki, naomba niwasisitize wale wanafunzi ambao walikuwa hawajakamilisha ada zao hao ndiyo wafanye malipo ili kuziwezesha shule kufanya kazi yao vizuri.

“Kwa hiyo hapa kuna pande mbili, wale ambao walikuwa hawajakamilisha malipo ya ada wakamilishe ili shule ziweze kufanya kazi yao vizuri, lakini wale ambao walikwisha kamilisha na walifunga kwa sababu kulikuwa na tatizo, warejee shuleni kuendelea na masomo kama vile ambavyo waliachia bila kuwa na michango ama ada za ziada,” alisema Prof. Ndalichako.

ONYO NA HOFU

Alisema Rais Magufuli, amekuwa akisema mara kwa mara watu waondoe hofu, hivyo kuagiza wanafunzi michango ikiwamo malimao na tangawizi ni sehemu ya kupandikiza hofu.

“Unavyowaambia kwa mfano mtu aende na kilo moja ya malimao ya unga, mimi kwanza ukiniuliza malimao ya unga yanauzwa duka gani sijui, kwa hiyo unavyotangaza vitu ambavyo hata upatikanaji wake ni mgumu utakuwa unatengeneza hofu na kila mara kiongozi wa nchi amekuwa akisema tusitumie corona kutengeneza hofui.

“Hata tangawizi ya unga kilo moja, mtu anaipata wapi? Kwanza kilo moja ni nyingi mtu anakwenda kukaa shuleni mwezi mmoja na wiki mbili na kilo moja ya tangawizi, koo litabaki salama? 

“Tuangalie pia na afya za watoto, tunachoshauri shule tuendelee kuwapa (wanafunzi) vyakula ambavyo vinakuwa na vitamin C kwa sababu huu ugonjwa unakuwa unaambatana na mafua, kwa hiyo tuwape vyakula ambavyo vina zinki ambayo hata kwenye maboga inapatikana.

“Tungetumia zaidi vyakula vya asili badala ya kuwatuma wanafunzi wapeleke vitu ambavyo ni vya kutengeneza, wataalamu wanasema vinaweza kuleta magonjwa mengine kama kansa,” alisema Profesa Ndalichako.

Katika hatua nyingine, aliwataka wazazi wawape watoto wao barakoa ambazo zimeshonwa kwa vitambaa, ambazo mwanafunzi anaweza akafua, kupiga pasi na kumuwezesha kuzitumia mara kwa mara.

“Lakini vilevile wanafunzi wanavyoenda shuleni wazingatie umbali baina ya mtu na mtu, waepuke msongamano, iwe ni katika majadiliano, darasani, bwenini, iwe ni katika kula, waendelee kuzingatia taratibu ambazo zinatolewa na Wizara ya Afya,”alisema Profesa Ndalichako.

WIZARA YA AFYA NA MWONGOZO

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetoa mwongozo ambao unalenga kuweka mazingira wezeshi ya kudhibiti maambukizi ya corona katika taasisi za elimu.

Mwongozo huo umezingatia maeneo makuu manne ambayo ni maandalizi ya mazingira ya taasisi ya elimu kabla ya shule kufunguliwa, uchunguzi wa afya, usafiri wa kwenda na kurudi na mazingira ya kujifunza.

Akitoa mwongozo huo jana Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema wamezingatia utoaji wa elimu ya corona shuleni, vyuoni ikiwemo dalili na hatua za kuchukua ili kujikinga.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais Tamisemi na wizara zote zinazosimami vyuo na taasisi elimu wanatakiwa kuhakikisha uwepo salama ya shule, vyuo na taasisi kabla ya wanafunzi kurejea ili kudhibiti maambukizu ya Covid-19.

“Moja ya maandalizi ni kutakasa mazingira yote ya shule, chuo au taasisi kwa kuzinagatia miongozo ya utakasaji iliyotolewa na Wizara ikihusisha taasisi ambazo zilitumika kutunza washukiwa au wagonjwa wa corona.

“Kuhakikisha kuwepo kwa vifaa vya kunawa mikono yenye maji tiririka na sabuni katika kila eneo la shule au vyuo,uongozi wa shule uhakikishe kuwa unavitakasa mikono yenye ubora unaotakiwa kwa wanafunzi na wanavyuo,” alisema Waziri Ummy.

Kutokana na hali hiyo aliutaka uongozi wa shule na vyuo kuhamasisha wanafunzi, waalimu na wafanyakazi kuvaa barakoa za vitambaa huku wazazi wakichukua jukumu la kuwanunulia watoto barakoa hizo.

“Shule, vyuo na taasisi vyenye vituo vya kutolea huduma za afya watumishi wapewe elimu ya kuwahudumia wanafunzi, waalimu na wafanyakazi watakaoshukiwa kuwa na Covid-19 ikiwemo kuwapa msaada wa kisaikolojia na kuondoa unyanyapaa.

“Shule za bweni zihakikishe kuwepo kwa nafasi kati ya kitanda kimoja na kingine na kudhibiti uchangiaji wa vifaa,uongozi uhakikishe utaratibu mzuri wa upatikaji wa barako na unapaswa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kuhifadhi taka zinazotokana na barakoa,” alieleza .

Waziri huyo wa Afya, alisema kuwa wanafunzi wanaohisiwa kuwa na dalili za Covid-19 wafanyiwe vipimo kabla ya kurudi shule au vyuoni huku watakaobanika kuwa na maambukizi wabaki nyumbani hadi afya zao zitakapo imarika.

“Kwa wanafunzi watakaobainika kuwa na dalili wakiwa shuleni uongozi wa shule, chuo utoe taarifa kituo cha afya kilicho karibu,” alisema 

Katika mwongozo huo Waziri Ummy, aliwataka wamilikiwa wa magari za shule kuweka vitakasa mikono na kuhakikisha wanafunzi wamevaa barakoa za vitambaa na kutumia vitakasa mikono kabla ya kupanda gari.

Waziri Ummy pia aliwataka wataalamu wa afya wa mikoa na halmashauri kushurikiana na uongozi wa shule au chuo kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya barakoa, hatua za unawaji mikono na utumiaji sahihi wa vitakasa mikono.

“Uongozi wa shule unapaswa kuhimiza kanuni za usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara katika kila eneo muhimu aidha vitakasa mikono zinaweza kutumika kama mbadala.

“Uongozi wa shule au vyuo uhakikishe kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu, kuzingatia matumizi ya Tehama wakati wa kufundisha ili kupunguza uwezekano wa maambukizi,”alisema Ummy .

Aliwataka wataalamu wa afya wa halmashauri zote nchini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara shuleni, vyuoni na katika taasisi za elimu ili kuhakikisha tahadhari zote zinazingatiwa.

Hata hivyo Waziri Ummy, alishauri kuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wanafunzi na waalimu wenye magonjwa ya moyo, selimundu na magonjwa ya mfumo wa hewa kama pumu kutokuvaa barakoa.

“Kwa shule na vyuo vyenye wanafunzi wenye mahitaji maalum, waalimu wanapaswa kuvaa barakoa maalum zitakazoruhusu mwanafunzi mwenye matatizo ya usikivu kuwasiliana na mwalimu,” alibainisha.

Alisema mwongozo huo utakuwa ukiboreshwa mara kwa mara ili kukidhi nahitaji ya wakati husika.

KIKWETE UDSM

Katika hatua nyingine, Rais mstaafu ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete, aLIsema hosteli za chuo hizo zilizokuwa zikitumika kama karantini kwa watu wanaotoka nje ya nchi, sasa zipo salama baada ya kukaguliwa na wataalamu wa afya.

Kikwete alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana baada ya kukagua mazingira ya hosteli hizo kabla ya kuanza kuwapokea wanafunzi ambao wanatarajiwa kuendelea na masomo Juni Mosi mwaka huu.

“Baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kwamba vyuo vitaanza kufunguliwa Juni Mosi, nikamwuliza makamu mkuu wa chuo kuwa tumejiandaaje akaniambia wameshajiandaa vya kutosha.

“Ndio tukakubaliana leo (jana) tukutane tujue tumejiandaa kweli kuanza tarehe 1, lakini makamu akaniambia maandalizi yamekamilika na wanafunzi wengine wameshaanza kuja kujidaili kwa ajili ya kuanza masomo.

“Pia nikamweleza kwamba kama hivyo basi wale waliochukua ile Hostel za Magufuli watangaze rasmi kwamba wameshafanya yale yote waliyoahidi. Tukasema kauli hiyo hatutakiwi kutoa sisi, watoe wenyewe waliochukua hizo hostel na waeleze walichokifanya,” alisema.

 Vilevile alisema wakati ule corona ilipoibuka hapa nchini, walikutana kujadili suala hilo lakini bahati nzuri na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akatangaza kufungwa vyuo.

“Hofu yetu kubwa tulipokutana ilikuwa ni tunajipanga vipi na maisha yangu yote na malezi yangu siku zote nimekuwa lazima niwe mbele ya kile kitu kinachotokea,” alisema.

Kikwete alisema baada ya vyuo kufungwa hofu kubwa ilikuwa ni watafanyeje endapo janga la corona ingeendelea hadi Oktoba lakini imekuwa bahati nzuri.

“Kwa hiyo pako salama likitokea la kutokea tujue je wamekujanao au wameupatia hapa,” alisema Kikwete.

Awali akizungumza Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Dar es Salaam, Neema Kweba alisema Hostel za Magufuli ni salama baada ya wao kumaliza zoezi la utakasaji.

“Magufuli Hostel ni salama kwa ajili ya wanafunzi kuja kukaa kwa sababu sisi tumemaliza zoezi la utakasaji na tumefanya kwa kila chumba, kitanda, godoro katika jengo nzima,”alisema Kweba.

Aprili 5, mwaka huu Serikali ilitangaza kwamba wasafiri wote kutoka nchi za nje zilizoathirika na ugonjwa wa Corona watalazimika kukaa karantini kwa muda wa siku 14 katika hosteli hizo za Magufuli.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles