29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

WAHADZABE WAOMBA SERIKALI KUWAPELEKEA TANI MBILI ZA BANGI

Na ELIYA MBONEA-KARATU


JAMII ya Wahadzabe wanaojishughulisha na uwindaji, kurina asali na kukusanya matunda porini, wameomba kupelekewa msaada wa bangi angalau tani mbili watakayoitumia kwa mwaka mmoja.

Wahadzabe wanaokadiriwa kufikia 500 ni jamii inayoishi porini maeneo ya Endamaghan, Kandeni Tarafa ya Eyasi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Jamii hiyo, bado inakabiliwa na umasikini licha ya kuwa kivutio cha watalii katika Ziwa Eyasi.

Ombi hilo walilitoa juzi katika Kijiji cha Endamaghan, wakati walipotembelewa na timu ya wataalamu kutoka serikalini iliyoteuliwa kuandaa mapendekezo ya muundo wa kipindi cha pili cha mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Akizungumza na MTANZANIA katika eneo la makazi yao yenye nyumba za asili za nyasi zilizoonekana kuwa wazi kutokana na kufunikiwa na nyasi kidogo, Mwenyekiti wa jamii hiyo, Julius Ndaya alizitaja sababu alizodai ni za msingi za kuomba wapelekewe bangi.

Alisema shughuli za kutembea kutafuta wanyama kwa ajili ya kitoweo huwalazimisha kutembea umbali mrefu kiasi cha kilomita 50, kazi ambayo huwa ni sehemu ya majukumu ya mwanamume katika jamii hiyo.

“Kiasi hiki cha tani mbili kinaweza kututosha watu kama 100 au 200  kwa miezi 6, tunavuta bangi si kama ambavyo wengine au Serikali wanafikiria kwamba tunaweza kusababisha vurugu, kuvunja nyumba za watu, kuiba wala kugombana na jamii nyingine, hapana.

“Mmea huu tumeukuta babu zetu wakiwa wanauvuta wameturithisha, tunaendelea kuvuta bila kuwa na madhara yoyote. Hii ni sehemu ya kiburudisho kwetu, huku porini hatunywi pombe hii ndio pombe yetu. “Ikiwezekana turuhusiwe kulima angalau bustani za bangi lakini changamoto kubwa tunayokutana nayo ni pale Serikali inapopiga marufuku zao hili kwa madai kuwa ni sehemu ya dawa za kulevya,” alisema Ndaya.

Kiongozi wa jamii hiyo alikwenda mbali na kueleza pindi wanapovuta bangi huchangamsha akili na miili yao, hivyo hujikuta wakipiga hadithi za matukio ya uwindaji porini au namna walivyokabiliana na au kukurupushana na wanyama wakati wa uwindaji.

Katika eneo la jamii hiyo lenye nyumba za asili za nyasi zikiwa zimezungukwa na mafuvu ya wanyama pori na miti mikubwa, lilikuwa na wanawake watu wazima walionekana wamekaa kwenye makundi pamoja na vijana wa kiume wakiendelea kuvuta bangi.

Akifafanua kuhusu maombi ya Wahadzabe kuomba tani mbili za bangi, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo alisema Serikali haiwezi kukubaliana na maombi hayo.

“Hata sasa walikuwa wakiniomba, majuzi tuliteketeza kiasi kama cha hekari tano za bangi maeneo ya milimani, kwa hiyo kwa sasa hawaipati inawaumiza zaidi.

“Kikubwa tunaendelea kuwapatia elimu kwamba bangi kwao si kitu kizuri, tutatafuta mbadala na kwa vile wameniomba nikutane nao hilo nalo tutaliweka vizuri.

“Naamini vipo vitu mbadala wanavyoweza kutumia badala ya bangi, mnawaona wanalalamika kwa sababu hawaipati. Tunajua ni wawindaji wanakimbia na kupita maeneo magumu ndio maana wanaihitaji ili iwatoe nishai, ukweli ni kwamba jambo hilo hatuwezi kuliruhusu,” alisema.

Wakati watu hao takribani 200 kutoka jamii ya Kihadzabe wakiomba kupelekewa tani mbili za bangi, katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge waliomba zao hilo liruhusiwe kuwa la kibiashara ili kuwaongezea kipato zaidi wakulima na wauzaji wa bangi.

Chakula kikuu cha jamii hiyo ni mizizi, matunda pori, asali na nyama huku asali ikiwa ni miongoni mwa vitu vinavyopendwa zaidi na jamii hiyo.

Namna wanavyoitumia mizizi hiyo kwa chakula; wanakula kama ilivyo au kuichoma na ladha yake ni kama muhogo au viazi na mizizi hiyo huwa na ukubwa kama wa mguu wa mti mzima.

Matunda yao makuu ni kwantlanabe, kalahar, kongolobi na ubuyu ambayo husagwa kwenye jiwe na unga wake husongwa kama ugali na kuchanganywa na asali.

Vyakula vyao vinavyotegemea asili yao haviwapi fursa ya kutumia mafuta, nyanya, kitunguu, sukari au kutumia vinywaji vya viwandani, isipokuwa chumvi.

 

Wanyama wanaopendwa zaidi na Wahadzabe ni pofu, nyani, tumbili, digidigi  na twiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles