JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limewatia mbaroni wahamiaji haramu 83, raia wa Ethiopia, waliokuwa wakisafirishwa na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T478 DFE mali ya Frola Mwambenja, ambao walikuwa wakitokea Kongowe jijini Dar es Salaam kuelekea Kyela mkoani Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema jeshi hilo linamshikilia pia dereva wa gari hilo, Hans Mwakyoma (28) mkazi wa Tukuyu Mbeya na msaidizi wake Alex Adam (32) mkazi wa Mbeya mjini, kwa tuhuma za usafirishaji wa watu hao.
Kamanda Kakamba alisema gari hilo lilikamatwa na askari wa doria wa jeshi hilo saa 3.30 usiku katika Kijiji cha Mahenge, barabara kuu ya Iringa Mbeya likiwasafirisha watu hao kuelekea Kyela ambako ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.
“Lilipokamatwa roli hilo, dereva alisema halina mzigo, lakini askari wetu walipolifungua walikuta watu hao wakiwa wamelaliana, baadhi yao wakiwa na hali mbaya na wengine wakiwa wagonjwa,” alisema.
Alisema baada ya kuwakamata, wahamiaji hao walipewa chakula na wale walioonekana wagonjwa wamepatiwa matibabu wakati taratibu zingine za kuwafikisha katika vyombo vya sheria zikiendelea.
“Jambo la kushangaza ni kwamba watu hao walipakiwa katika gari hilo Kongowe jijini Dar es Salaam. Kila mtu anajua Kongowe si Ethiopia kwa hiyo kuna swali la kujiuliza ni namna walivyofika Kongowe hadi wakapata huduma ya kusafirishwa kuelekea wanakoelekea,” alisema.
Alisema biashara haramu ya usafirishaji watu ni jipu kubwa linalohitaji nguvu ya pamoja katika kulitumbua kwani inahusisha mtandao wa watu wengi ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kupambana na biashara hiyo, taarifa za kiintelejensia za jeshi hilo zinaelekea kuunasa mtandao wa biashara hiyo na mkakati huo utakapofanikiwa wahusika wake watatumbuliwa majipu hadharani.
Alisema watu hao wamekuwa wakiitia gharama kubwa serikali, kwani baada ya kuwakamata imekuwa ikilazimika kuwahudumia na kuwasafirisha hadi walipotoka.