23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Nape aeleza sababu ya kufungiwa Mawio

Nape NnauyeNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ameeleza sababu za Serikali kulifungia gazeti la Mawio, sambamba na kutangaza rasmi kulifuta katika orodha ya daftari la msajili wa magazeti nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema sababu za kulifuta gazeti hilo ni kutokana na mwenendo usioridhisha wa uandishi wa habari wa gazeti hilo linalomilikiwa na Kampuni ya Victoria Media Service Ltd.

“Serikali imeamua kulifuta kutoka katika daftari la msajili wa magazeti, gazeti lijulikanalo kama Mawio,” alisema Nape nakuongeza:

“Serikali kwa masikitiko makubwa, imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo usioridhisha  wa kuandika na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi yetu,” alisema.

Aidha alisema hatua hiyo pia inazuia gazeti la Mawio kuchapishwa katika njia nyingine yeyote ikiwa ni pamoja na mitandao (Online Publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta, Sura ya 306.

Waziri huyo alisema hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa za kukemea aina ya uandishi wa gazeti hilo, ambapo  mara kadhaa Msajili wa Magazeti, tangu Juni 2013 hadi Januari 2016, amekuwa akimtaka mhariri wa gazeti hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala katika gazeti lake bila mafanikio.

“Msajili wa Magazeti kwa juhudi zake alifanya mawasiliano na mhariri wa gazeti hilo mara nane kwa lengo la kutaka afanye marekebisho ya mtindo wa kutoa habari zake lakini mhariri hakuzingatia ushauri aliopewa na msajili,” alisema Nape.

Alienda mbali zaidi na kusema gazeti hilo kila lilipoandikiwa barua za kuonywa, mhariri alikuwa akitoa majibu ya kuudhi, kejeli na mzaha.

“Serikali imekuwa ikiwaonya mara kadhaa lakini wameshindwa kujirekebisha na zaidi ya hapo wamekuwa wakitoa majibu ya kuudhi, kejeli na mzaha,” alisema Nape na kuongeza: “Tumeshindwa kuvumilia,” alisema.

Amri ya kulifungia gazeti la Mawio ilitolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 55 la Januari 15. Uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 Sura ya 229, kifungu 25(1), ambapo Nape alisema akiwa kama waziri mwenye dhamana anaitekeleza bila kujali kama ni nzuri au mbaya.

“Nikiwa kama waziri niliapa kuilinda Katiba na kutekeleza wajibu wangu kwa mujibu wa sheria na madhali hii ndio sheria iliyopo lazima niitekeleze kama ilivyo hata kama ni mbaya ndiyo iliyopo,”alisema Nape.

Kifungu kilichotumika kufungia gazeti la Mawio cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, sura ya 229 kipengele cha 25.-(1) kinampa mamlaka waziri ikiwa anaona inafaa kutoa maamuzi wa kufungia gazeti lolote kama ataona ni kwa manufaa ya umma au kwa manufaa ya amani ya jamii.

“Kwa upande mwingine ninatoa pongezi kwa vyombo vyote vya habari nchini vinavyozingatia maadili, weledi na sheria zinazosimamia taaluma ya habari na sheria nyingine za nchi.

“…Kwa namna ya pekee Serikali inawapongeza wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari ambavyo vinapofanya makosa vikielekezwa hujirekebisha na kutoa ushirikiano kwa Serikali na pia kubadili mwenendo wao, hawa ni pamoja  na wahariri wa magazeti ya Mwananchi, MTANZANIA, The East African, Magazeti ya Daily News, Habari Leo, Uhuru na mengineyo,” alisema Nape.

Kufutwa kwa gazeti la Mawio kumekuja siku moja baada ya kuwapo kwa taarifa ya wahariri wa gazeti hilo kutafutwa na Jeshi la Polisi, ili kusaidia uchunguzi kuhusu habari ambazo zimekuwa zikiandikwa na gazeti hilo.

Juzi Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro, alithibitisha taarifa hizo na kusema  ni kweli kwamba wahariri hao wanatafutwa na polisi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kinanda, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema ameshtushwa na vitendo kama hivyo na kusema kuwa watakutana kwa dharura kujadili suala hilo.

Sahara Media

Wakati huo huo, Kampuni ya Sahara Media Group inayomiliki kituo cha televisheni cha Star Tv na vya redio vya Kiss FM Redio Free Afrika (RFA), imesema hajapokea barua ya kutakiwa kuzima vituo hivyo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles