24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa wa sasa corona wafikia 284

Nora Damian -Dar Es Salaam

WAGONJWA wapya 30 wamethibitika kuwa na virusi vya corona nchini na kufanya hadi sasa kuwa wagonjwa 284 tangu janga hilo liingie nchini, Tanzania ikiwa ya pili Afrika Mashariki kuwa na wagonjwa wengi.

Kati ya wagonjwa wapya waliotangazwa jana Dar es Salaam wapo 10, Zanzibar  tisa, Mwanza wanne, Pwani wawili, Kagera mmoja, Dodoma wawili, Manyara mmoja na Morogoro mmoja.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza jana wakati wa maombi ya kitaifa dhidi ya janga la corona, alisema kati ya wagonjwa waliothibitika nchini, 256 wanaendelea vizuri, 7 wako kwenye uangalizi maalumu, 11 wamepona na 10 wamefariki.

Alisema pia watu 2,815 waliokuwa karibu na wagonjwa wamefuatiliwa afya zao nao kati yao, 1,733 hawana maambukizi na kwamba12 walikutwa na virusi hivyo  na kufanya jumla ya wagonjwa nchini kufikia 284.

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria kuwa ifikapo mwisho wa Aprili, nchi yetu ingekuwa na wagonjwa 524,716.

“Lakini tunamshukuru Mungu kwa kuwa kadirio hilo hatujalifikia. Serikali inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa huu zikiwemo za kutoa elimu ya namna ya kujikinga, kuunda kamati za kitaifa kwa ngazi za mawaziri, makatibu wakuu, timu ya wataalam wa afya pamoja na kutoa maelekezo kwa kamati za ulinzi na usalama.

“Tumetenga maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huu, tumenunua vifaa vya kukabiliana na ugonjwa huu hususani kwa watoa huduma wa afya,” alisema Majaliwa. 

Alisema pia wameimarisha maabara kwa lengo la kupanua wigo wa kufanikisha upimaji wa sampuli na kwamba vituo zaidi ya 7 nchini ambapo upimaji wa awali unaanzia huko na kwenda kuhakikishwa katika Maabara Kuu ya Taifa.

Aliwaasa Watanzania kuepuka matumizi mabaya na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii juu ya ugonjwa huo na badala yake waendelee kuisikiliza Serikali na wataalam ambao watatoa maelekezo thabiti.

“Jiji la Dar es Salaam ndio lina maambukizi makubwa hivyo, nawasihi wananchi kama huna jambo lolote la kufanya huna sababu ya kuzurura na kwa wafanyabiashara si lazima kuja Kariakoo, unaweza kufanyia katika eneo lako,” alisema.

Aliwashukuru viongozi wa dini kwani wameshiriki tangu tatizo hilo lilipoingia nchini na akawataka waendelee kuomba kwani maombi yao yana uzito na nguvu kwenye jamii.

Alisema waumini waendelee kusisitizwa kujiepusha na maambukizi na kufuata masharti ya kujikinga.

“Tupunguzue uwezekano wa mtu mmoja kumuambukiza mwingine, tuhakikisha kwamba waumini wanaweza kukaa umbali wa mita moja, maji sabuni, vitakasa mikono viwepo.

“Matukio mengine ya nyongeza muyaangalie upya, kuna mikusanyiko ya vijana wadogo, vikundi vya kina mama, madrasa, ‘Sunday School’ nayo yaangaliwe ili kupunguza misongamano.

“Vipaza sauti, mikeka muhakikishe vinatumika kwa usahihi ili visisambaze ugonjwa huu, kama kuna uwezekano wa kupuliza dawa tupulize,” alisema Majaliwa.

MFUNGO WA RAMADHANI

Alitoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha vyakula muhimu katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan vinauzwa kwa bei ya kawaida huku akisisitiza kwa wakuu wa mikoa na wilaya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye masoko ili kuhakikisha bei ni ile ile.

“Wafanyabiashara kote nchini wahakikishe vyakula muhimu vinauzwa kwa bei ya kawaida, hakuna sababu ya sukari kupanda, ipo tena ya kutosha, bei itaendelea kuwa ile ile, yeyote anayeuza kilo Sh 4500 chukueni hatua kali dhidi yake,” alisema Majaliwa.

VIONGOZI WA DINI

Viongozi wa dini walioongoza maombi hayo Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir, Mwakilishi wa Mufti wa Zanzibar, Kiongozi wa Madhehebu ya Shia Tanzania, Sheikh Hemed Jalala, Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Thadeus Ruwa’ich na Dk. Alex Malasusa kwa niaba ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Wengine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora Tanzania, Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania, Mwenyekiti wa Makanisa ya Kisabato Tanzania, Mark Malekana.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, aliyekuwa akiratibu hafla hiyo alisema nchi zilizosikiliza Serikali zimefanikiwa vizuri hivyo akawaasa viongozi wa duni kuendelea kusikiliza Serikali na maelekezo yanayotolewa na wizara ya afya.

UKUBWA WA TATIZO

Hadi sasa duniani kuna zaidi ya wagonjwa milioni 2.55 na waliofariki dunia wakiwa zaidi ya 177,00 wakati waliopona ni zaidi ya 696,00.

Nchi yenye wagonjwa wengi ni Marekani yenye wagonjwa 819,000 na kati yao waliofariki ni 45,00 na waliopona ni 82,000.

Kwa Afrika nchi yenye wagonjwa wengi ni Misri yenye wagonjwa 3,490 kati yao waliofariki ni 260 na waliopona ni 870, huku Afrika Mashariki nchi yenye wagonjwa wengi ni Kenya yenye wagonjwa 296 ambapo waliofariki ni 14 na waliopona ni 74, Rwanda ina wagonjwa 147 na Uganda 61.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles