23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi Pemba watakiwa kukabidhi vitambulisho vya kura

Omar Khamis OthmanNA KHELEF NASSOR, ZANZIBAR

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaagiza wafanyakazi wa umma wote kuwasilisha vitambulisho vyao vya kupigia kura na vile vya u-Zanzibari kwa mamlaka husika.

Agizo hilo limetolewa na baadhi ya wakuu wa mikoa Kisiwani Pemba, ambao wamesema kila mfanyakazi anapaswa kutii agizo hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, alisema wafanyakazi watakaokataa kutii amri hiyo katika mkoa wake watachukuliwa hatua.

Alisema hatua hiyo haina uhusiano wowote na masuala ya kisiasa, isipokuwa wanataka kutambua watendaji na wafanyakazi wa Serikali waliomo ndani ya mkoa wake.

“Mimi mkuu wa mkoa natamani niwajue wafanyakazi wote waliomo ndani ya mkoa wangu, nimewaagiza walete vitambulisho vyao ili ninapowahitaji iwe urahisi kwangu na kufanya hivi ni haki yangu.

“Tunawaambia wafanyakazi watii amri halali ya Serikali, wasifuate milengo ya kisiasa maana wanaendeshwa na wanasiasa.

“Kuna taarifa hivi sasa walimu wanaambiwa wasishiriki uchaguzi, msikubali, tukiwajua tutawachukulia hatua,” alisema.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na MTANZANIA, walisema wanasikitishwa na agizo hilo kwa sababu ineonekana kuna jambo limejificha nyuma ya pazia.

Mmoja wa wananchi hao, Ahmada Mahfoudh Zuberi, alisema mkazo wa sheria hiyo upo zaidi Kisiwani Pemba kutokana na kuwapo wafuasi wengi wa vyama vya upinzani.

“Hilo halitaki tochi, mbona kila kitu wanakimbilia zaidi Pemba kutokana na kuwapo wafuasi wengi wa upinzani?

“Mimi nakwambia hakuna jambo jingine wanalotaka, kama anataka kujua idadi ya wafanyakazi vitambulisho vya kupigia kura vinahusika vipi hapa? Kila mtu ana hiari yake kushiriki au kutoshiriki kwenye uchaguzi, sasa wanataka kutulazimisha kwani huu ni utawala wa kidikteta?” alihoji.

Kwa upande wake, mwanasheria Masoud Faki Masoud alisema hakuna sheria yoyote inayompa mamlaka mkuu wa mkoa kujua ana wafanyakazi wangapi katika mkoa wake.

Juhudi za kuwapata maofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuelezea kadhia hiyo hazikuzaa matunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles